Rungwe: Ikibidi Rais Samia aongezewe muda tupate Katiba mpya

Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe katika mahojiano maalumu na mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Imani Makongolo. 

Wakati Taifa likitarajia kuwa na uchaguzi wa serikali za mitaa baadaye mwaka huu na uchaguzi mkuu wa mwaka 2025, wito wa kuwa na Katiba mpya bado umekuwa ukisisitizwa na wadau wa demokrasia, wakiamini kwamba ndiyo njia ya kuwa uchaguzi huru na wa haki.

Tayari Rais Samia Suluhu Hassan ametoa hakikisho la kuwapatia Watanzania Katiba mpya na anatambua kwamba wanaihitaji ndiyo maana Serikali yake imetenga bajeti kwa ajili ya kuanza mchakato huo utakaoanza na utoaji wa elimu ya Katiba kwa wananchi.

Hivi karibuni, Rais Samia ametia saini Sheria ya Tume ya Uchaguzi na sasa jina la Tume hiyo litakuwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, jambo ambalo limeibua mjadala mpana wa kitaifa, wadau tofauti wametoa maoni yao kuhusu mabadiliko hayo.

Mwananchi limefanya mahojiano maalumu na mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma), Hashim Rungwe kuhusu mambo mbalimbali, ikiwemo uchaguzi mkuu ujao, Katiba mpya na mabadiliko ya jina la Tume ya Uchaguzi.

Rungwe anaamini kwamba hakuna sababu ya kwenda kwenye uchaguzi mkuu mwakani bila kuwa na Katiba mpya.

Anasema haamini kama Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi pekee inatosha kuufanya uchaguzi kuwa huru na wa haki kama Katiba haitarekebishwa.

Amesema Katiba mpya ndiyo itamaliza sintofahamu ya upande mmoja kuona uchaguzi hautakuwa huru na haki, licha ya Rais Samia mara kadhaa kuwahakikishia Watanzania kwamba uchaguzi utakuwa huru na wa haki.

Wakati kukiwa na pande mbili zenye mitazamo tofauti kuhusu uchaguzi huo, Rungwe anasema bado imani ya chama chake kwenye Tume huru ya uchaguzi ni ndogo na kitakachomaliza sintofahamu hiyo ni kupatikana kwa Katiba mpya kabla ya kwenda kwenye uchaguzi.

“Uchaguzi ujao ufanyike kwa kutumia Katiba mpya, hicho ndicho kitamaliza sintofahamu inayoendelea sasa,” anasema Rungwe katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika ofisini kwake, Makumbusho, Dar es Salaam.

Rungwe anasema kama changamoto ya kupatikana kwa Katiba hiyo ni muda, basi vyama vya siasa wakubaliane Rais Samia aongezewe muda, Bunge liridhie, ili muda huo utumike kukamilisha upatikanaji wa Katiba mpya, ndipo uchaguzi ufanyike.

Anasema hapingi suala la mpango wa Serikali kutoa elimu kwa miaka mitatu, hata hivyo anasema nchi isiende kwenye uchaguzi bila kuwa na Katiba mpya kwa sababu hakutakuwa na tofauti yoyote.

“Kama tatizo ni muda, bora tukubaliane na Bunge liidhinishe Rais aongezewe muda, lakini kwa masharti kwamba katika kipindi hicho kitakachoongezwa tuwe tumepata Katiba mpya, ndipo twende kwenye uchaguzi,” anasema Rungwe.

Alipoulizwa kuhusu kauli ya Rungwe, wakili wa kujitegemea, Fredrick Kihwelo anasema haiwezekani kusogeza mbele uchaguzi kwa sababu upo kwa mujibu wa Katiba na sheria, kwamba kila baada ya miaka mitano uchaguzi lazima ufanyike.

“Kama mtakubaliana kwamba kwanza mkamilishe mchakato wa katiba ndiyo muingine kwenye uchaguzi, hilo halitakuwa suala la kikatiba, litakuwa ni suala la kisiasa, lakini watakuwa wamevunja sheria, watakuwa wamevunja Katiba.

“Katiba haitakiwi kusimamishwa, wala sheria haiwezi kusimama. Tumekuwa na muda mrefu tu wa kujiandaa, kama tungekuwa na nia njema ya kuhakikiha tunapata sharia ambazo ni nzuri au kama tunataka Katiba, tulikuwa na muda mrefu tu, shida ni utashi wa kisiasa,” anasema.

Rungwe anaongeza kuwa nchi ikienda kwenye uchaguzi ikiwa na Katiba mpya, hakutakuwa na maneno, hofu na sintofahamu ambazo zimeanza kuonekana mapema, ikiwamo chama chake kutokuwa na imani kama utakuwa huru na wa haki.

Pamoja na hivi karibuni kufanyika mabadiliko ya Sheria ya Tume ya Uchaguzi na Tume hiyo kuitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, Rungwe anasema, Chaumma hakina imani kama kuna uhuru kwenye Tume hiyo.

“Tumeletewa barua leo (Aprili 15) ikitueleza kuhusu Tume ya Uchaguzi kuitwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, bado hatuna imani kama itakuwa ni Tume huru kwa kuwa watu ni wale wale, muundo wake ni ule ule. Chaumma tunaona hakuna kitakachobadilika.

“Jambo pekee ambalo litatupa imani ya kuamini uchaguzi utakuwa huru na haki ni kuwa na Katiba mpya, uzuri kwenye maoni ya Rasimu ya Jaji Joseph Warioba (aliyekuwa mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba), Watanzania wameeleza wanahitaji Katiba ya aina gani,” anasema.

Mwanasiasa huyo mkongwe anasema hakuna sababu ya kwenda kwenye uchaguzi bila kuwa na Katiba mpya, akishauri kama tatizo ni muda, basi Taifa likubaliane Rais aongezewe muda wakamilishe mchakato wa Katiba mpya, ndipo wafanye uchaguzi.

“Kinachohitajika ni mabadiliko ambayo hayawezi kupatikana bila kubadilisha Katiba yetu, wananchi wanahitaji Katiba mpya, Serikali inadai muda ni mdogo, mara inabidi watu wote kwanza waisome, kama tatizo ni hilo, tusifanye uchaguzi, tuyakamilishe hayo tupate Katiba mpya ndiyo tuitumie kwenye uchaguzi ujao.

“Tukiliweza hili, basi hakutakuwa na maneno maneno tena, tukikubaliana tuweke na masharti kwamba katika kipindi hicho ambacho tumemuongezea muda, tupate Katiba mpya,” anasema Rungwe.

Mwenyekiti huyo wa Chaumma anasema Tume ya Jaji Warioba ilikuwa inakwenda vizuri na rasimu yake ilikuwa inazungumzia mambo ya mabadiliko ambayo yalikuwa ni maoni ya wananchi, lakini mchakato huo ukavurugwa.


Katiba sio ya mtu

Rungwe anasema kuna baadhi ya watu wanaiona Katiba kama mali yao, jambo ambalo halifai kwani Katiba ni ya wananchi, siyo ya mtu wala chama.

“Hatuhitaji kuwa na ugomvi ili tupate Katiba mpya, Katiba ndiyo msingi wa nchi, japo kuna watu tunapotaka Katiba mpya wao wanalazimisha ugomvi, wanaifanya kama hiyo ni mali yao wakati nchi ni yetu sote,” anasema.

Anaeleza kwamba Rais Samia kwa kiasi kikubwa ameonyesha mwanga wa kutaka Watanzania wapate Katiba mpya, lakini kuna watu wamekuwa wakiiona kama Katiba ni mali yao na kupinga kila hatua za mabadiliko yake.

“Wananchi wengi wanataka Katiba mpya, ni haki yao, sijui kinachoshindikana ni nini? Kama tukipata Katiba mpya kila kitu kitakwenda sawa, tutashiriki uchaguzi bila sintofahamu, tofauti na tukiamua twende na Katiba ya sasa.

“Bila shaka wasimamizi watakuwa ni walewale, mwenyekiti wa Tume ni yuleyule, wajumbe wake ni walewale, hatabadilisha kitu gani?” anahoji Rungwe.


Apinga Tume huru

Licha ya kubadilishwa kwa jina la Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi hivi karibuni, Rungwe anasema haina vigezo vya kuitwa huru kwa kuwa Chaumma inaona haina tofauti na ile ya zamani (Tume ya Uchaguzi).

“Muundo wake bado ni uleule, wajumbe na mteuaji wao ni yule yule, tulieleza tulipotoa maoni yetu, lakini hatujasikilizwa.

“Tunaposema Tume huru, sio refa ndiyo anajiamulia kwamba yeye ndiyo atachezesha mpira na yeye huyo huyo anachagua wachezaji, kwa utaratibu huo, sio rahisi kusema ni huru.”

“Ili iwe huru ingekuwa ni Tume ambayo haina uhusiano na Serikali iliyopo madarakani, haina nguvu na wale watu waliowachagua,” anasema.

Anasema kama ingekuwa hivyo, kitu ambacho kingefuata ni kuangalia matendo na utendaji kazi wa Tume hiyo ambayo kwa sasa bado hawajayaona, ingawa kwa muundo wake wanaona imebadilika jina, lakini matendo ni yale yale. “Chaumma imani yetu ni ndogo sana, hatuoni kama ni Tume huru, japo tunalazimishwa tukubali hivyo,” anasema.

Anasema watazungumza kwenye chama ili kuona watafanya nini baada ya kupokea barua kutakiwa kuitambua kama hiyo sasa ni Tume Huru ya Uchaguzi.

“Kama wajumbe au wachezaji ni walewale na wamepatikana kwenye njia zilezile, maoni yetu tulitoa ya nini?” anahoji mwanasiasa huyo maarufu kama “Mzee wa Ubwabwa”.


Kuja na ubwabwa tena

Rungwe alijipatia umaarufu kwenye kampeni zake katika uchaguzi mkuu uliopita alipowania urais kwa tiketi ya Chaumma na kuwa na sera ya kuwapatia wananchi ubwabwa, anaamini bila kushiba hakuna kinachofanyika.

Anasema kama atapewa ridhaa kwa mara nyingine na chama chake, kipaumbele chake cha kwanza kwenye uchaguzi wa mwaka 2025 kitakuwa hicho cha “ubwabwa” kwa maana ya wali, chakula pendwa.

“Bado nina nguvu ya kugombea tena, lakini ni mchakato na itategemea kama chama kitanipa ridhaa hiyo, ikiwa ni mimi tena kwenye uchaguzi ujao, ubwabwa (wali) ni lazima, hospitali zote za umma na shule za umma kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita, watakula bure.

“Siyo kuwaambia wachangie, hiyo itakuwa ni bure, itakuwa ni menyu ambayo itabadilika kila siku, hadi kuku watakula. Inawezekana, kwani hata sisi wakati tunasoma tulikuwa tunakula shuleni, hadi maziwa tulikuwa tunakunywa, nini kinashindikana sasa?”

Anasema lazima kuwajali watoto wanaosoma shule za umma, akibainisha kwamba wengi wamekuwa wakiteseka kwa njaa.

“Huwezi kusoma kama una njaa, hawa waheshimiwa tusiwasikilize, watoto wao wala hawasomi shule za kata, wanaoteseka ni watoto wa wananchi wa kawaida, kama Chaumma itapewa dola, ndani ya siku 100 za kwanza hili tutalitimiza,” anasisitiza Rungwe.

Rungwe anasema kipaumbele chake kingine ni ajira, watawarudishia wananchi viwanda, miundombinu na kutakuwa na soko huru na Serikali itajikita kukusanya kodi.

“Serikali huwa haina hasara, hata kwenye shirika letu la ndege, litaendeshwa na watu, watatumia jina na kote huko tutakusanya kodi, kikubwa ni kuwa na mfumo wa kuwa-control (kuwadhibiti) hawa watu,” anasema.


Wanachojivunia Chaumma

Rungwe anasema tangu wamepata usajili wa kudumu, Juni 4, 2013, Chaumma kinajivunia mambo mawili makubwa ambayo ni kuelewana na kusikilizana.

“Hatujawahi kuwa na migogoro isiyokuwa na msingi, tumepevuka kwenye hilo, Chaumma kimeanzishwa kwa lengo moja na hatujatoka kwenye mstari huo, huku Bara na Zanzibar.

“Lengo letu ni kupata dola, wananchi wakiamua watupe ridhaa ili sisi tusimame na kuwatengenezea Serikali nzuri ambayo watajivunia na kuwa na uhuru, sio ya kuwabambikizia mambo,” anasema Rungwe, bila kuanika mikakati ya chama, akisema hilo siyo la kulianika hadharani kwa madai kuwa mara nyingi wanasiasa wanawindana katika mazungumzo.