Kauli ya ‘tutawapoteza’ ilaaniwe, hatua zichukuliwe

Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Faris Buruhan

Kauli ya Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Faris Buruhan, inayotaka Jeshi la Polisi lisitafute vijana wanaotukana viongozi mtandaoni baada ya kutoweka, ni kauli yenye hatari na yenye kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani.

Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi akitoa kauli inayopotosha umuhimu wa haki za binadamu na uhuru wa kujieleza.

Sisi hatuungi mkono wala kupigia chapuo tabia ya kutukana viongozi, lakini tunatambua kwamba kwa tafsiri za wanasiasa, kuna mstari mwembamba kati ya kutukana na kuwakosoa viongozi.

Katika jamii yoyote, ni muhimu kwa viongozi kuwa mfano wa kuigwa katika kudumisha heshima, utawala bora na kuheshimu uhuru wa watu kujieleza.

Kauli kama hizi za Buruhan zinaweza kutoa ishara mbaya kwa umma na kuhatarisha misingi ya demokrasia na utawala wa sheria, hasa katika kipindi ambacho kuna matukio mengi ya watu kupotea au kuchukuliwa na watu wasiojulikana.

Ukweli ni kwamba kila mmoja ana haki ya kutoa maoni yake na kujieleza bila vitisho au hofu ya kulipiza kisasi kutoka kwa vyombo vya dola au kwa watu wengine wenye mamlaka. Kujenga mazingira ya hofu na ukandamizaji kunaweza kuharibu demokrasia na kusababisha mgawanyiko katika jamii na hatimaye kuhatarisha amani pale ambapo wanaodhani wananyanyasika wataamua kupigania haki zao.

Vyama vya siasa na viongozi wa kisiasa wanapaswa kuhimiza mazungumzo ya amani, heshima na kuepuka matumizi ya lugha na vitisho au vya ukandamizaji.

Badala yake, wanapaswa kuweka mfano wa uongozi unaoheshimu haki za kila raia na kuzingatia misingi ya utawala wa sheria, kwamba kila anayekosea anawajibishwa kwa mujibu wa sheria badala ya kushambuliwa, kuteswa au kupotezwa.

Ni bahati mbaya kauli hii imetolewa wakati baadhi ya Watanzania hawajapata majibu ya mahali walipo wapendwa wao waliodaiwa kupotea kiutata au kuchukuliwa na watu wasiofahamika.

Kama wachambuzi walivyolieleza tukio hilo, kauli ya Buruhan inaweza kuongeza migogoro, kutishia uhuru wa kujieleza na usalama wa watu.

Ni jukumu la Serikali na vyombo vyake vya dola kuchukua hatua madhubuti kuzuia vitisho kama hivi na kuhakikisha kila mtu anaheshimu sheria na haki za binadamu.

Wito wetu ni kuwa kiongozi huyu wa vijana ahojiwe na vyombo hivyo ili aeleze alikuwa ana maana gani na aliwahi kuhusika vipi na watu wengine waliopotea.

Kwa hiyo, kwa kuanza na huyu, ni muhimu kwa mamlaka husika zichukue hatua za haraka na za moja kwa moja kwa kiongozi ambaye anatoa kauli za kuchochea vurugu na uvunjifu wa amani.

Ingawa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi amekemea kitendo hicho akisema ni kauli ya kijinga, tunadhani hatua zaidi za kisheria zinapaswa kuchukuliwa ili kudumisha amani na utulivu katika jamii.

Hatupaswi kuvumilia vitisho au lugha za chuki zinazoweza kuhatarisha maisha na haki za watu; amani na haki vinapaswa kuwa vipaumbele vya juu kwa nchi yetu.

Hata hivyo, kama ambavyo imewahi kutokea siku za nyuma, haitakuwa ajabu kukuta kijana huyo anapata uteuzi wa nafasi nono zaidi, hali inayochochea vitendo hivyo kutokukomeshwa.

Ni wajibu wa viongozi wa kisiasa na kijamii kujitolea kwa dhati katika kukuza kauli zenye tija na kudumisha misingi ya amani na haki za binadamu.