Walemavu wanaweza kuendesha miradi mikubwa

Muktasari:

  • Walemavu kama wanajamii wengine wana nyenzo moja muhimu katika maisha yao. Na hii ni ile ya udhaifu wanaozaliwa nao au kuupata maishani kutumika kama kitu cha kuwapatia huruma na mapenzi ya ziada kutoka kwa wanajamii wenzao.

Katika dunia hii ambayo mashine ikiwemo roboti sasa zinatumika kufidia upungufu wowote wa mwanadamu sioni ni kwa nini walemavu Tanzania washindwe kujipanga na kuendesha miradi mikubwa kuliko ilivyo kwa hivi sasa.

Ili kufikia huko ipo haja ya wasamaria wema na wale wote wanaohusika na masuala ya walemavu kuangalia ni kwa namna gani walemavu hapa nchini wanaweza kwenda kujifunza kutoka kwa wenzao kwenye nchi mbalimbali duniani.

Kwa yakini, kwa kuanzia tu ningeliwashauri ndugu zangu hawa kutoka bara waende awali ya yote kujifunza kutoka kwa wenzao wa Zanzibar. Ninaamini angalau kwa kuona tu wenzao walivyojipanga huko, wakirudi watakuwa na mwamko na mtazamo mpya katika kutazama mambo yao.

Hivi leo walemavu hapa nchini kama watawezeshwa hawashindwi kufanya kazi kama zile za uunganishaji au uundaji mitambo mbalimbali, uendeshaji kompyuta na vifaa vinavyoendana navyo; umakenika au kutengneza magari katika karakana zinazojengwa kiurafiki kwa walemavu; ushonaji na ufumaji nguo za aina mbalimbali; ualimu na uhadhiri. Vilevile baadhi ya shughuli za udaktari na shughuli mbalimbali za utamaduni na sanaa zilizo ndani ya uwezo wao. Kinachonekana kuwarudisha nyuma ndugu zetu hawa, kwa maoni yangu, ni kukosa uwezeshaji wa kuanzia, uwepo wa taasisi imara kwa walemavu nchini na vikorombwezo vyake ikiwemo SACCOS au benki maalumu kwa ajili yao; uongozi wa kuwafungua macho walemavu na kile wanachoweza kuwa sawasawa na wanadamu wengine; umoja na ushirikiano wa kweli katikakujiendeleza wao wote kwa pamoja na siyo mtu mmoja mmoja.

Pia mipango mikakati ya kujiendeleza kufikia kile ambacho kila mmoja wao anatakuwa; mifumo na oganaizesheni za shughuli zao kwa njia au mbinu za kisasa. Pia matumizi mwafaka ya teknohama; taratibu na kanuni wanazoweza kuzifuatilia au kuzidhibiti hivyo kujua na kuona kila kinachoendelea. Kuwa na elimu au maarifa katika ujasiramali, kanuni bora za menejimenti na utawala au uendeshaji mambo kisayansi bila kusahau uwepo wa ushirikiano wa kuwawezesha kiuchumi na kijamii na siyo kuwapa msaada kama msaada tu.

Walemavu kama wanajamii wengine wana nyenzo moja muhimu katika maisha yao. Na hii ni ile ya udhaifu wanaozaliwa nao au kuupata maishani kutumika kama kitu cha kuwapatia huruma na mapenzi ya ziada kutoka kwa wanajamii wenzao.

Msaada huo unaweza kutumika kwa watu kujilegeza na kukubali au kujiona wao ni watu wa kusaidiwa tu siku zote, au ukatumika katika kuwawezesha wao wenyewe kuendesha shughuli ndogo kwa kubwa za kiuchumi.

Hata ikawa kwamba wao hawahitaji msaada toka kwa mtu bali wako katika nafasi ya wao kama wanajamii wengine pia kutoa msaada kwa wanajamii wenye dhiki zaidi. Kwa kuanzia ningelipenda kutoa wito kwa viongozi wa ndugu zetu hawa kuangalia uwezekano wa wao wenyewe kuwa na ushirika au jumuiya au chombo chochote kiwacho kitakachowawezesha kuunganisha nguvu zao ili waweze kuwezeshwa kiurahisi zaidi. Wazo la haraka haraka ni kuwepo kwa mfuko wa jengo la walemavu kwa kuanzia hapa jijini kisha kwenye miji na majiji mengine hapo baadaye.

Walemavu wakiweza kuchangishana wakapata angalau asilimia ya kuridhisha ya fedha zinazohitajika ninaamini benki zitagombania kuwakopesha kiasi kilichobakia kwa ulaini tu na kazi kubwa ni kuweza kuichora ramani hii ya jengo la makao makuu ya walemavu nchini, kiasi kwamba walemavu wote waafiki kuwa ni kitu muhimu katika maisha yao ya baadaye kujitolea na kuhakikisha kwamba linakuwepo na linaendeshwa kwa faida yao. Ni lazima waanze wao wenyewe na viongozi wao na siyo rahisi wapita njia pembeni kujitokeza papo kwa hapo na kuwasaidia kulifanya hili kuwa kweli.

Jengo hilo ambalo itakuwa vizuri liwe la ghorofa litaweza kuwa na pango kwa ajili ya taasisi kama benki ikiwemo ya walemavu wenyewe. Upo umuhimu mkubwa sana wa walemavu kupata fursa ya kushiriki kikamilifu katika uchangiaji mawazo juu ya Katiba Mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Lakini, ninaamini uwezeshwaji wenywe wa namnahii utaipa sauti jamii hiyo. Ili kufikia huko ipo haja ya kuwa na mpango mkakati wa kikundi utakaoanza kwa wanataaluma mbalimbali na viongozi wa kikundi kuzungumzia nini iwe dira ya kikundi na wanachama wake.

Kisaikolojia kumwambia mlemavu kwamba yeye anaweza kujitegemea pasipo kumtegemea mtu mwingine katika maisha yake ni mtihani mgumu kwelikweli. Lakini, huko ndiko makala haya na mkakati unaopendekezwa hapa unakotaka kuwasaidia walemavu kuelekea. Ninaamini ni kitu kinachowezekana siku moja tukawa hapa Tanzania na walemavu wanaojitegemea na kuiendeshea maisha yao bila kutegemea huruma au hisani ya raia wenzao.

Katika kutunga mpango mkakati wao lazima pia sayansi ya mawasiliano na ustadi wa kikundi na wanakikundi kujiuza vitumike kwa mapana na marefu. Mbia muhimu sana katika kufanya mpango mkakati utakaotengenezwa uwe na ufanisi na tija ya kuridhisha ni vyombo vya habari kama vile magazeti, televisheni, redio na tovuti. Hivi vikitumika kwa ukamilifu wake vitakuwa na mchango mkubwa katika kuhakikisha kwambawalemavu wanafanikiwa katika kila wanachopanga na kukusudia kukifanya.