Ubadhirifu nchini, unatia kichefuchefu

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Ludovick Utouh

Muktasari:

Ingawa hulka ya binadamu ni kutaka zaidi na kujipendelea, lakini hulka hiyo hushamiri zaidi katika mfumo wa ubepari, ambao hauangalii masilahi ya jamii kwa upana wake, bali masilahi ya mtu mmoja mmoja.

Rushwa na ubadhirifu ni uozo ulioota mizizi nchini. Hali hizi hazikuwa maarufu wakati ambapo kweli Tanzania ilikuwa ikifuata siasa ya Ujamaa na Kujitegemea kwa sababu, siasa hiyo haikuruhusu ubinafsi.

Ingawa hulka ya binadamu ni kutaka zaidi na kujipendelea, lakini hulka hiyo hushamiri zaidi katika mfumo wa ubepari, ambao hauangalii masilahi ya jamii kwa upana wake, bali masilahi ya mtu mmoja mmoja.

Leo hii, kila mtu anajaribu kutafuta mbinu ya kujitajirisha hata kama ni kwa gharama ya watu wengine na ndiyo maana imekuwa ni jambo la kawaida kwa mtu kuiibia Serikali au shirika au kampuni anayofanyia kazi.

Ubadhirifu wa mali ya umma au mali ya mwajiri umekuwa jambo la kawaida kabisa, kiasi cha mtu kutoona aibu, wala fedheha kufanya hivyo na mbaya zaidi ni pale jamii inapomsifu mtu mwizi na mbadhirifu wa mali ya umma.

Hali hiyo imekwenda mpaka katika miradi midogo midogo au miradi inayofadhiliwa na wahisani. Wakati wafadhili wanapotumia fedha za walipa kodi wa nchi zao kujaribu kuwakomboa Watanzania ili angalau waondokane na matatizo ya kiuchumi na kimiundombinu waliyonayo, Watanzania wenyewe hata habari hawana, wako tayari kuifisidi hata miradi hiyo wanayopelekewa ili iwakomboe.

Hivi karibuni Shirika la New Yearly Meeting la Marekani limesitisha ufadhili wa wanafunzi wanaosoma elimu ya juu na ujenzi wa nyumba za walimu wilayani Serengeti kutokana na kugundua udhaifu katika usimamizi wa fedha inazotoa.

Taarifa inasema kuwa wafadhili wamegundua ubadhirifu na fedha wanazozitoa kutofanya kazi iliyokusudiwa. Huu ni ubadhirifu unaotia kichefuchefu.

Huo ni mfano mdogo tu, lakini ni mara ngapi taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali imekuwa ikiibua madudu kuhusu matumizi ya fedha za umma?

Kila mara ripoti inapotoka tunaona madudu katika matumizi ya fedha za umma katika sekta za afya, elimu, halmashauri na hata ujenzi wa miundombinu. Tunachopaswa kujiuliza kwa pamoja ni je, tunamkomoa nani, wakati ukweli ni kwamba tunajichelewesha wenyewe katika kufikia maendeleo tunayoyatarajia?

Kiini cha tatizo hili ni udhaifu wa mfumo uliopo. Mfumo tulionao humfanya kila mtu kupigania kujiongezea kipato kwa gharama yoyote, bila ya kujali lolote.

Kwa upande wa wahudumu wa umma, kwa kuwa wengi hulipwa mishahara duni, huku gharama za maisha zikipaa juu, nao hutumia fursa yoyote waipatayo kufanya mashambulizi katika mali ya umma.

Kwa upande mwingine, mfumo tulionao umeshindwa kuhudumia raia kwa dhati, hivyo husababisha raia kuzikosa huduma za msingi  wanazostahili kuzipata.Matokeo yake hulazimika kutoa rushwa ili kuzipata huduma hizo kwa haraka katika kutatua matatizo yao ya kila siku.

Kwa upande wa wanasiasa katika mfumo huu wa kibepari wapo kujaza matumbo yao kwa kushirikiana na mabepari kwa kipindi chote cha kushikilia nafasi zao. Kwa hivyo, hutumia kila fursa waipatayo katika kufanya ufisadi, rushwa, ubadhirifu ili kutunisha mifuko yao haraka iwezekanavyo.

Pengine yawezekana kujiondoa katika lindi hili la uozo kwa kubadilisha mifumo ya matumizi ya fedha za umma na uwajibikaji.

Lakini pia suala la maadili ni la kuzingatiwa zaidi kwa jamii nzima kwani, jamii isiyokuwa na maadili, isiyotaka kujua hili ni baya na linapaswa kuachwa, hiyo ni jamii muflisi.