Adhabu USM Alger hizi hapa, fainali ni Berkane vs Zamalek

USM Alger itatozwa faini ya Dola 50,000 (Sh 130 milioni) na kufungiwa kushiriki mashindano yote ya klabu yaliyo chini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (Caf) baada ya jana kugomea kucheza mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane katika Uwanja wa Manispaa wa Berkane huko Morocco.
Timu hiyo ya Algeria iliamua kutocheza mechi hiyo baada ya Berkane kuvaa jezi ambazo zilikuwa na bendera na ramani ya Morocco yenye eneo lenye mgogoro kwa nchi hizo mbili, kitendo ambacho kilisababisha hata mechi ya kwanza baina ya timu hizo iliyopaswa kuchezwa Algeria, Aprili 21 kutofanyika.

Kanuni ya 11 ya mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika inafafanua kuwa timu ambayo itashindwa kucheza mchezo wa hatua ya robo au nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itatozwa kiasi hicho cha fedha pamoja na kifungo lakini itaondolewa kwenye michuano husika.

"Kujitoa kwa timu ambako kutaripotiwa katika hatua ya robo fainali au nusu fainali kutaenda sambamba na kupoteza haki ya kuingia katika mashindano na faini ya Dola 50,000," inafafanua ibara ya nane ya kanuni hiyo.

Sababu za kisiasa ndizo zineoana kuchangia kwa kiasi kikubwa mechi mbili baina ya timu hizo kutochezwa licha ya timu zote mbili kuwepo katika vituo vya mchezo.

Mechi ya kwanza haikuchezeka kwa vile serikali ya Algeria iliizuia RS Berkane kutumia jezi zenye bendera na ramani ya Morocco jambo ambalo lilikuwa kinyume na taratibu za mchezo na kupelekea timu hiyo ya Morocco kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao 3-0 huku USM Alger ikiamriwa kwenda Morocco kwa ajili ya mchezo wa marudiano.

Na jana Jumapili, USM Alger ilisusia mechi kwa vile haikuwa tayari kucheza na RS Berkane ikiwa imevaa jezi kama zile ambazo zilifanya mechi ya kwanza isichezwe.
Algeria imekuwa na mgogoro wa kisiasa na Morocco chanzo kikiwa na eneo la Saharawi.

Hii ina maana kwamba, Caf wameiondoa USMA na kuipeleka fainali Berkane ambayo itavaana na Zamalek kwenye mchezo wa fainali ya kwanza Mei 12 huku zikirudiana Mei 19 kutafuta bingwa wa michuano hiyo.

Zamalek imefuzu kwenye hatua hii baada ya kuichapa Dreams FC ya Ghana kwa jumla ya mabao 3-0


Kiini cha mgogoro:

Morocco na Algeria zimekuwa na mgogoro wa kidiplomasia baada ya Morocco kulaani vitendo vya “uchochezi” na “uvunjaji sheria” katika ufunguzi wa mashindano ya kandanda ya kikanda nchini Algeria ambapo mjukuu wa Nelson Mandela alitoa hotuba na kutoa wito kwa Sahara Magharibi kuachwa “huru”.

Kwa muda mrefu, Morocco imekuwa ikiitawala Sahara Magharibi licha ya msukumo kutoka jumuiya ya mataifa kuitaka nchi hiyo kuacha kuikalia Sahara Magharibi, jambo ambalo wamekataa wakiichukulia kama sehemu ya nchi yao.

Majirani hao wa Afrika Kaskazini wako katika mgogoro mkali kuhusu eneo hilo linalozozania ambapo vuguvugu la Polisario huko Sahara Magharibi, linaloungwa mkono na Algeria, linataka ifanyike kura ya maoni ili wananchi waamue hatima yao.

Algeria inaunga mkono vuguvugu la Polisario huko Sahara Magharibi ambayo Morocco inaliona kama sehemu ya eneo lake. Mpaka kati ya Algeria na Morocco umefungwa tangu mwaka 1994.

Agosti 2021, Algeria ilikata uhusiano na Morocco, ikiishutumu kwa “vitendo vya uhasama”, lakini Morocco ilijibu kwa kusema “haikuwa na haki kabisa”.
Mwaka huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Algeria, Ramtane Lamamra alitangaza kukata uhusiano wa kidiplomasia na Morocco kutokana na kile alichokitaja kama

“mfululizo wa vitendo vya kichokozi”. Morocco ilijibu ikisema shutuma hizo ni za “uongo” na kwamba inajutia uamuzi huo.

Julai 2022, Mfalme Mohammed VI wa Morocco alitoa wito wa kurejeshwa kwa uhusiano wa kidiplomasia na Algeria. Hata hivyo, hadi sasa uhusiano baina ya mataifa hayo bado siyo mzuri kutokana na kila upande kushikilia msimamo wake kuhusu udhibiti wa Sahara Magharibi.

Siyo mara ya kwanza mataifa hayo kuingia kwenye mzozo, yalianza kuingia kwenye mgogoro wa mpaka mwaka 1963, mwaka mmoja baada Algeria kupata uhuru. Mwaka 1969 na 1972, walitiliana saini mkataba wa kumaliza mgogoro huo.
Mgogoro huo umekuwa ukitatuliwa na kurejea tena kwa miaka tofauti.