Arsenal, Barcelona kitaeleweka leo

Muktasari:

  • Arsenal ambayo ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Porto kwenye mchezo wa kwanza ugenini, leo itakuwa nyumbani kuhakikisha inapindua matokeo hayo ili iweze kufuzu kwenye hatua hiyo muhimu.

Barcelona, Hispania. Barcelona na Arsenal, leo zitatakiwa kufanya kazi kubwa ili kuhakikisha zinatinga hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal ambayo ilipoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Porto kwenye mchezo wa kwanza ugenini, leo itakuwa nyumbani kuhakikisha inapindua matokeo hayo ili iweze kufuzu kwenye hatua hiyo muhimu.

Kwa upande wa Barcelona ambayo ilionyesha kiwango cha juu kwenye mchezo wa kwanza ugenini na kutoka sare ya bao 1-1 dhidi ya Napoli, leo inarejea nyumbani kuhakikisha inapata ushindi na kufuzu.

Mabingwa watetezi wa michuano hiyo mikubwa Ulaya Manchester City pamoja na mabingwa wa kihistoria Real Madrid tayari zimeshafuzu sawa na Bayern Munich na Paris Saint-Germain.

Timu zote zinazocheza leo na kesho zina nafasi ya kufuzu kutokana na matokeo ya michezo ya mkondo wa kwanza kwa kuwa hakuna iliyopoteza kwa zaidi ya bao moja.

Barcelona ambao ni mabingwa watetezi wa La Liga, itavaana na bingwa mtetezi wa Italia Napoli, ambapo timu itakayoshinda itafuzu hatua inayofuata.

Licha ya kuchukua ubingwa kwenye ligi zao kwa msimu uliopita timu hizi hazifanyi vizuri msimu msimu ambapo kwa, Barcelona inashika nafasi ya tatu kwa pointi 61 kwenye La Liga, ikiwa tofauti ya alama nane dhidi ya vinara Real Madrid.

Napoli yenyewe ipo nafasi ya saba kwenye Serie A, ikiwa nyuma ya vinara Inter Milan kwa pointi 31, jambo ambalo litawafanya leo watumie nguvu ya ziada kuhakikisha wanaitupa nje Barcelona ikiwa nyumbani kwao.

Kocha Xavi Hernandez, ambaye ameshatangaza kuwa mwishoni mwa msimu anaondoka kwenye timu hiyo amesema matokeo mabaya kwenye Ligi ya Hispania yasiwaondoe wachezaji wake kwenye ndoto za kutwaa Ligi ya Mabingwa.

Xavi amesema anaamini bado Barcelona inaweza kutwaa ubingwa huo msimu huu kama itafanikiwa kuvuka hatua hii.

Xavi ambaye anaonekana hana uhusiano mzuri na mabosi wa Barcelona atataka kuondoka kwenye timu hiyo akiwa ameiachia kombe la sita la michuano hiyo mikubwa Ulaya.

Hata hivyo, haiwezi kuwa kazi rahisi kwa kuwa Napoli ambayo imetimua makocha wawili hadi sasa msimu huu kwa ajili ya kutafuta mafanikio imefanikiwa kufanya vizuri kwenye Ligi ya Mabingwa kuliko kwenye ligi ya ndani.

Timu hizo katika michezo yote tisa ambayo imekutana, Barcelona imeshinda marai tano huku Napoli yenyewe ikishinda mmoja tu na sare mara tatu.

Katika michezo hiyo Barcelona imefunga mabao 21, huku Napoli ikifunga nane, huku kwenye michezo mitano iliyopita ya hivi karibuni, Barcelona imeshinda tatu, imetoka sare michezo miwili.

Kwa upande wa Napoli yenyewe imeshinda michezo miwili na kutoka sare mitatu kwenye ligi ya ndani ya Italia.

Kwa upande wa Arsenal ambayo ipo chini ya kocha kijana Mikel Arteta, imekuwa kwenye kiwango bora kwenye ligi na sasa timu hiyo inaongoza ikiwa mbele ya Manchester City na Liverpool.

Hata hivyo, ili kuonyesha kweli timu hiyo imepania kufanya mambo makubwa msimu huu itatakiwa kuhakikisha inashinda kwa zaidi ya bao 1-0 leo ili iweze kwenda robo fainali sehemu ambayo haijafika kwa miaka ya hivi karibuni.

Arsenal imerudi kwenye Ligi ya Mabingwa msimu huu kwa mara ya kwanza baada ya kuwa nje kwa miaka saba na ilionyesha kiwango cha juu sana kwenye hatua ya makundi na kufuzu 16 bora.

Timu hiyo ambayo imekuwa na kiwango kizuri cha kupachika mabao mashabiki wake watakuwa na furaha kuiona inatinga robo fainali jina lao kuonyeshwa kwenye droo itakayopangwa Ijumaa,  Nyon nchini Uswisi.

Inaonekana pia itakutana na wakati mgumu kwa kuwa Porto imekuwa na safu bora ya ulinzi kwenye ligi ya ndani ikiwa imeruhusu mabao 17 tu ikiwa ndiyo timu iliyoruhusu mabao machache kwenye ligi hiyo hadi sasa.

Lakini itatakiwa kuwa makini na washambuliaji wa Arsenal ambao wamefunga mabao 37 kuanzia mwaka huu umeanza yakiwa ni tisa nyuma ya mabao yote ya Porto msimu huu mzima.

Kwa ujumla Arsenal na Porto zimekutana mara saba kwenye michuano ya Uefa ambapo zimetoka sare mara moja, huku Porto ikishinda tatu na Arsenal tatu.

Mechi zote ambazo Arsenal imeshinda ni zile ambazo ilicheza nyumbani kwenye Uwanja wa Emirates, huku Porto ikishinda michezo yote kwenye Uwanja wa Estádio do Dragão.

Kwa ujumla kwenye michezo hiyo, Arsenal imefunga mabao 12, huku Porto ikifunga matano kabla ya mchezo wa leo saa 5:00 usiku.


Matokeo mechi tano za nyuma Arsenal vs Porto:

Arsenal 4-0 Porto

Porto 2-0 Arsenal

Porto 2-1 Arsenal

Arsenal 4-0 Porto

Porto 1-0 Arsenal.


Mechi tano za Barcelona vs Napoli

Napoli 1 – 1 FC Barcelona

Napoli 2 – 4 FC Barcelona

FC Barcelona 1 - 1Napoli

FC Barcelona 3 – 1 Napoli

Napoli 1 – 1 FC Barcelona