Arteta ahamishia nguvu Ligi Kuu England

Muktasari:

  • Kocha huyo amesema wachezaji wake wanahitaji faraja kwa sasa na hakuna neno ambalo anaweza kuwaeleza wakamwelewa kwa kuwa kila mmoja aliamini kwenye kutwaa ubingwa huu.

Kocha wa Arsenal, Mikel Arteta amesema hana maneno mengine ya kuwaambia wachezaji wake baada ya kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Arsenal imeondolewa kwenye michuano hiyo mikubwa baada ya juzi kuchapwa bao 1-0 na Bayern Munich na kutolewa kwenye michuano hiyo kwa jumla ya mabao 3-2 baada ya sare ya mabao 2-2 nchini England.

Kocha huyo amesema wachezaji wake wanahitaji faraja kwa sasa na hakuna neno ambalo anaweza kuwaeleza wakamwelewa kwa kuwa kila mmoja aliamini kwenye kutwaa ubingwa huu.

"Wachezaji wangu walikuwa hawana nguvu kwenye vyumba vya kuvalia nguo, lilikuwa pigo kubwa kwetu na hakuna namna nyingine yoyote zaidi ya kukubaliana na jambo lilotokea.

"Tulijaribu kwa kila namna kuhakikisha kuwa tunaibuka na ushindi, lakini mambo hayakuwa mazuri kwetu, tumecheza na timu yenye uzoefu wa kutosha kwenye michuano hii.

"Tulikaribia kutimiza lengo letu, lakini tukafanya makosa kwenye eneo la ulinzi na kuondoka kwenye michuano hii mikubwa, lakini lazima tuamke na kumaliza msimu vizuri kwa kutwaa Ligi Kuu England.

"Tulikuwa na muda mrefu hatujaingia kwenye michuano hii, lakini nataka kuwahakikisha kuwa tumefanya vizuri kufika hatua hii na tunakaribia kufikia mafanikio miaka kadhaa ijayo.

Arsenal ilikosa hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya kwanza baada ya kupita miaka sita.

Sasa timu hiyo inarejea kwenye Ligi Kuu England ikiwa inawania ubingwa pamoja na Manchester City na Liverpool, yenyewe ikiwa nafasi ya pili na pointi 71 mbili nyuma ya Man City.

Timu zilizofuzu nusu fainali ni Bayern Munich, Borrusia Dortmund, PSG na Real Madrid.