Aziz Ki ajiweka pazuri Bara

Muktasari:

  • Aziz Ki ambaye juzi alifunga bao moja kwa mkwaju wa penalti wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu, ameendelea kukaa kileleni akiwa amehusika kwenye mabao 22 ya timu yake ambayo imefunga jumla ya mabao 54, baada ya kucheza michezo 22.

Nyota wa Yanga, Stephane Aziz Ki ameendelea kujiwekea ufalme wake kwenye Ligi Kuu Bara baada ya kuongoza kwa kuhusika kwenye mabao mengi mbele ya mzawa Feisal Salum  ‘Fei Toto’ wa Azam.

Aziz Ki ambaye juzi alifunga bao moja kwa mkwaju wa penalti wakati Yanga ikiibuka na ushindi wa 2-1 dhidi ya Simba kwenye mchezo wa Ligi Kuu, ameendelea kukaa kileleni akiwa amehusika kwenye mabao 22 ya timu yake ambayo imefunga jumla ya mabao 54, baada ya kucheza michezo 22.

Hii ina maana kuwa, Ki amekuwa na wastani wa kutengeneza bao moja kwenye kila mchezo ambao timu yake imecheza msimu huu, ikiwa ni zaidi ya wengine waliopo kwenye timu 16.

Staa huyo raia wa Burkina Faso, amefanikiwa kufunga mabao 15 na kutoa pasi saba za mabao, anafuatiwa na Fei anayeitumikia Azam FC ambaye amehusika kwenye mabao 19, baada ya kufunga 13 na kutoa pasi sita za mabao, timu yake ikiwa imefunga mara 49 kwenye michezo 23 kabla ya mechi ya jana dhidi ya Ihefu.

Ki, ameonyesha kuwa yupo kwenye kiwango cha juu akiwa amebakiza mabao mawili tu ili kufikia idadi ya yale waliyofunga wafungaji bora wa msimu uliopita, Fiston Mayele na Saido Ntibazonkiza ambapo kila mmoja alifunga 17 na kupewa kiatu cha dhahabu.

Staa huyo mwenye uwezo mkubwa wa kupiga mipira ya faulo, amebakiza michezo minane tu ya ligi dhidi ya JKT Tanzania, Coastal Union, Mashujaa, Kagera Sugar, Mtibwa, Dodoma, Tabora United na Prisons ili aweze kufikia rekodi ya mfungaji wa msimu uliopita na kuipita kama ataendelea na kiwango hiki kwenye michezo iliyobaki.

Nyota anayefuata ni Kipre Junior wa Azam ambaye naye amehusika katika mabao 16 baada ya kufunga manane na kuchangia mengine manane kabla ya mchezo wa jana.

Clatous Chama wa Simba anafuata kwa wachezaji waliohusika na mabao mengi baada ya kufanya hivyo mara 13, akifunga saba na kuchangia sita huku Marouf Tchakei aliyechezea Singida Fountain Gate na Ihefu kwa sasa akifunga manane na kuchangia matatu jumla yakiwa 11.

Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua amehusika kwenye mabao 11, akifunga saba na kuchangia manne kama ilivyokuwa pia kwa nyota wenzake, Maxi Mpia Nzengeli aliyehusika na 11, baada ya kukifungia kikosi hicho mabao tisa na kusaidia mawili.

Hii ina maana kuwa kwenye listi hiyo mchezaji mzawa anayepambana na wageni kwenye ligi hiyo ni Fei pekee, jambo linaloonyesha ubora wa kiungo huyo wa zamani wa Yanga.

Msimu wa 2021-2022, akiwa Yanga alicheza dakika 2044, katika michezo 26 kati ya 30 ya Ligi Kuu Bara ambapo alifunga mabao sita na kuchangia manne ‘asisti’ huku msimu uliopita wa 2022-2023, akifunga pia sita.

Akizungumzia na Mwananchi, Feisal alisema sababu kubwa ya kufanya vizuri ni kufuata maelekezo ya benchi la ufundi anayopewa.

“Mimi sishindani na mtu kwa sababu ikitokea nafasi ya kufunga au kutoa asisti nitafanya hivyo, malengo yangu ni kuona timu yetu inafanya vizuri na kuleta ushindani,” alisema.

Akizungumzia hilo kiungo wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema sababu kubwa ya nyota huyo kufanya vizuri ni kutokana na kutokuwa na presha.

“Ki anafanya vizuri. Lakini Fei anaonyesha ubora wake kwa kuwa yupo kwenye timu ambayo haimpi presha kubwa ya matokeo,” alisema.