Bayern, Real Madrid kitaumana leo

Ujerumani. Vigogo wa soka barani Ulaya, Bayern Munich na Real Madrid wataonyeshana kazi usiku wa leo Jumanne katika mchezo wa kwanza matata kabisa wa hatua ya nusu fainali kwenye mikikimikiki ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Wakati miamba hiyo ikitarajia kuonyeshana kazi huko Allianz Arena usiku wa leo, kesho Jumatano kutakuwa na shughuli nyingine pevu, ambapo Borussia Dortmund itakuwa nyumbani kuikaribisha Paris Saint-Germain. Kazi ipo.

Kipute cha Bayern na Madrid kitashuhudiwa vita ya ndugu wawili wa England, straika Harry Kane na kiungo Jude Bellingham, wakati kesho itamshuhudia Ousmane Dembele akirudi kuwakabili waajiri wake wa zamani akiwa na kikosi cha PSG.

Vita ya huko Allianz Arena usipime, ambapo Bayern na Madrid kati yao zimebeba ubingwa mara 20 wa mikikimiki hiyo, Los Blancos ikinyakua mara 14 na The Bavaria, ikinyakua mara sita zikiwa ni timu zilitwaa mara nyingi. Mashabiki wengi wanaamini huenda mmoja atakayevuka kwenye mechi hiyo, ndiye atakayekwenda kunyakua taji hilo la ubingwa wa Ulaya.

Kwenye hatua iliyopita, Bayern iliitupa nje Arsenal kwa jumla ya mabao 3-2, wakati Madrid yenyewe ilishinda kwa mikwaju ya penalti dhidi ya waliokuwa mabingwa watetezi, Manchester City.

Kwenye suala la mbinu za uwanjani, kocha Carlo Ancelotti anapewa nafasi kubwa mbele ya Thomas Tuchel, ambaye kwa msimu huu taji alilobakiza la kuwapa Bayern ni hilo la Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Real Madrid wao mambo yao si mabaya huko kwenye La Liga, ikiongoza msimamo wa ligi hiyo kwa tofauti ya pointi 10, hivyo inapewa nafasi kubwa ya kunyakua ubingwa huko Hispania. Lakini, kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, wanaamini huu ni wakati wao mzuri wa kwenda kubeba taji la 15 la michuano hiyo.

Harry Kane tayari ameshafunga mabao saba kwenye michuano hii akishika nafasi ya tatu kwenye chati ya ufungaji, huku Jude ambaye ameonyesha makali yake kwenye La Liga akiwa amefunga mabao manne, wakiwa ndiyo mastaa wanaopewa nafasi kubwa ya kuwika kwenye mchezo huu mkubwa Ulaya.

Kipute cha Dortmund na PSG kina mambo matamu, ambapo timu hizo zilipokutana kwenye hatua ya makundi, PSG ilishinda 2-0 nyumbani baada ya sare ya 1-1 huko Ujerumani. Je, safari hii itakuwaje.

Kylian Mbappe anatazamiwa kufanya kitu kikubwa kwenye mchezo huo ili kuifikisha PSG fainali kwenye msimu ambao unatazamwa kama wa mwisho wa fowadi huyo wa kimataifa wa Ufaransa kucheza Parc des Prince akiwa anaongoza kwenye chati ya ufungaji baada ya kufunga mabao manane.