Dube aigomea Simba

Muktasari:

  • Baada ya kutangaza kujiondoa kwenye kikosi cha Azam FC, Dube mawakili wamefafanua kuwa mchezaji huyo ana nafasi kuamua anapotaka kwenda na sio kulazimishwa.

Dar es Salaam. Wakati ikiripotiwa kuwa Simba sio kipaumbele cha kwanza nchini kwa mshambuliaji Prince Dube wa Azam FC baada ya kupeleka rasmi ofa ya kumhitaji, mawakili wamefafanua kuwa mchezaji huyo ana nafasi kubwa ya kuamua wapi pa kwenda bila kulazimishwa na timu yake.

 Maoni hayo ya mawakili yametolewa muda mfupi baada ya klabu hiyo kuthibitisha kuwa Simba na Al Hilal ya Sudan ndizo klabu pekee ambazo zimeonyesha kumhitaji Dube huku chanzo cha karibu na mchezaji huyo kikifichua kuwa kipaumbele cha kwanza kwa Dube hapa nchini ni Yanga.

"Azam inathibitisha kwamba imepokea ofa kutoka vilabu viwili tofauti vikimhitaji mchezaji wetu, Prince Dube, raia wa Zimbabwe. Ofa hizo zimetoka katika vilabu vya Simba ya Tanzania na Al Hilal ya Sudan.

"Uongozi unazifanyia tathmini ofa hizo ili kuona ipi inafaa. Aidha, Azam FC inavikaribisha vilabu vingine kuleta ofa zao kwani milango bado iko wazi," ilifafanua taarifa ya Azam FC.

Juzi, mtu wa karibu na Dube aliiambia Mwananchi Digital kuwa Simba sio kipaumbele cha kwanza kwa upande wa klabu za hapa Tanzania.

"Dube hitaji lake kwa hapa nchini ni Yanga na anaamini itapeleka ofa mezani ya kuhitaji huduma yake na kinyume na hapo amepanga kujiunga na timu ambayo iko nje ya Tanzania. Kwa Simba wanahitajika kumshawishi sana ili abadilishe mawazo na kujiunga nayo vinginevyo sio jambo rahisi," kilisema chanzo hicho.

Wakizungumza suala hilo kwa  nyakati tofauti, mawakili Alhaji Majogoro na Iddy Monday, walisema kuwa pamoja na Azam kukaribisha ofa mezani, mwenye uamuzi wa mwisho wa wapi akacheze ni Dube mwenyewe kwa vile hawezi kupelekwa timu ambayo haridhii kuichezea.

Walisema kuwa iwapo Simba, Al Hilal au klabu nyingine ambayo itakubaliwa na Azam kumchukua Dube, itatakiwa kufanya mazungumzo binafsi na mchezaji huyo na ikiwa itashindwa kufikia muafaka maana yake hatoweza kujiunga nayo hata kama iliafikiana na klabu inayomuuza.

"Mchezaji hawezi kulazimishwa kwenda sehemu asiyoitaka. Kinachoweza kufanyika ni mchezaji kutimiza mahitaji ya mwajiri wake ili yeye awe huru kwenda anapotaka," alisema Wakili Majogoro.

Wakili Monday alisema,"Ukishasaini mkataba unakuwa mali ya klabu husika. Wao watasikiliza ofa kubwa ila mchezaji ana haki ya maslahi yake kama watashindwana maslahi binafsi na timu husika anaweza kukataa kwenda akachagua pengine.

"Lazima kuwe na balansi baina ya klabu inayomiliki mchezaji kupata inachotaka kwa kuzingatia thamani ya mchezaji na mchezaji mwenyewe kupata maslahi anayotaka timu anayokwenda kulingana na thamani yake."

Kanuni ya 59 (2) ya Ligi Kuu Tanzania Bara, inalazimisha klabu kufanya makubaliano binafsi na mchezaji kabla ya kumsajili hata kama klabu inayommiliki mchezaji husika imeridhia kumuuza.

"Klabu inayotaka kumsajili mchezaji aliyesajiliwa au aliye na mkataba uliobakisha muda zaidi ya miezi sita (6) na klabu nyingine, italazimika kuafikiana na klabu yake kuhusu uhamisho wake kabla ya kukubaliana na kumsajili mchezaji huyo. Klabu inawajibika kuheshimu masharti ya msingi ya mkataba wa mchezaji wa klabu nyingine," inafafanua kanuni hiyo.Kuonekana msimu ujao

Kama Dube atachukuliwa na timu ya hapa nchini, maana yake atalazimika kusubiri hadi msimu ulimalizike ili aweze kujiunga nayo lakini kinyume na hapo hatoweza kwani hakidhi vigezo vya kikanuni kutumika kwa msimu huu kwa vile tayari ameshaitumikia Azam FC,

"Mchezaji wa kulipwa ambaye mkataba wake umekwisha kabla ya kipindi cha usajili anaweza kusajiliwa nje ya kipindi cha usajili, TFF itahitaji kujiridhisha juu ya kuaminika kwa hali nzima ya kumalizika huko kwa mkataba na maombi mapya ya usajili yanayokusudiwa, hali hii haitamhusu

mchezaji ambaye mkataba wake umesitishwa au umevunjwa," inafafanua kanuni ya 66(2).