Inonga ageuka kocha Simba  ikivuna pointi 3

Licha ya uwepo wa Juma Mgunda na msaidizi wake, Seleman Matola beki Mkongomani wa Simba, Henock Inonga ambaye alikuwa kati ya wachezaji wa akiba aligeuka kocha katika mchezo wa Ligi Kuu Bara ambao timu hiyo iliibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Tabora United.

Bao la Sadio Kanoute katika dakika ya 19 la tatu kwake msimu huu na Edwin Balua katika dakika 77,  yalitosha kuipa Simba ushindi huo muhimu kwenye Uwanja wa Azam Complex.

Katika kipindi cha kwanza mara kadhaa Inonga ambaye anahusishwa na FAR Rabat ya Morocco, alikuwa akifanya mawasiliano na Che Malone pamoja na Kennedy Juma ambao walikuwa wakiunda ukuta wa timu hiyo.

Inonga ambaye kwa wakati huo alikuwa ameketi alionekana kuwakumbusha majukumu yao mabeki hao baada ya kufanya kosa kubwa katika dakika ya 24 ambapo Kennedy alishindwa kuokoa mpira ambao pia ulimpita Che Malone.

Hata  hivyo, nyota wa Tabora United, Kalumba Banza alishindwa kutumia nafasi hiyo kwa mpira wake kuchezwa na Ayoub Lakred ambaye ameendelea kuonyesha kiwango bora akiwa na timu hiyo.

Hali ilionekana kuwa tofauti kwa Inonga katika kipindi cha pili, Mkongomani huyo alisimama kwa dakika zote huku safari hiyo akihamia upande wa washambuliaji ambao walikuwa wakicheza karibu naye.

Inonga alikuwa akionekana kutupa mikono huku na kule kama vile ambavyo makocha wamekuwa wakieleza muda mwingine kwa ishara na hata pale ambapo mwamuzi wa kati hakuonekana kufanya sawasawa alionyesha wazi kutokubaliana naye.

Tukio la namna hiyo limekuwa likifanywa na wachezaji kadhaa wenye wito wa ukocha na muda mwingine wenye shauku ya kutaka kuona timu inapata matokeo ya ushindi.

Katika uwanja huu huu wa Azam Complex, eneo hilo hilo ambalo alisimama Inonga ndipo Stephane Aziz Ki naye alikuwa akihamasisha wenzake baada ya kutolewa ili kufanya kweli Machi 14 katika mchezo wa ligi dhidi ya Geita Gold.

Ushindi ambao Simba imeupata umeifanya timu hiyo kufikisha pointi 54, imeendelea kusalia nafasi ya tatu nyuma ya Azam wenye pointi 57 huku wakiwa nyuma kwa mchezo mmoja. Azam iliibuka mapema na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Mtibwa.


Vikosi

Simba; Ayoub Lakred, Israel Mwenda, Mohammed Hussein 'Tshabalala', Che Malone, Kennedy Juma, Fabrice Ngoma, Edwin Balua, Sadio Kanoute, Freddy Michael, Mzamiru Yassin na Ladack Chasambi.

Tabora United;  Noble John, Shafih Maulid, Abdallah  Salum, Andy Bikoko, Pemba Kingu, Daud Rashid, Daniel Lukandamila, Najim Mussa, Eric Okutu, Kalumba Banza na Impiri Mbombo.