Ipswich yarudi EPL baada ya miaka 22

Muktasari:

  • Timu mbili zinazoongoza msimamo wa Ligi ya Championship England mwishoni mwa msimu zinapanda Ligi Kuu ya England (EPL) moja kwa moja.

Kiu ya miaka ya 22 ya Ipswich Town kushiriki Ligi Kuu ya England imeisha rasmi leo baada ya timu hiyo kupanda daraja kufuatia ushindi wa mabao 2-0 iliopata nyumbani mbele ya Hudderfield Town.

Mabao ya Wesley Burns na Omar Hutchinson yalitosha kuifanya Ipswich Town imalize katika nafasi ya pili ya Ligi ya Championship na kuungana na Leicester City ambayo yenyewe ilianza kutangulia kupanda.

Ipswich imefikisha pointi 96 ambazo ni moja pungufu ya zile za Leicester City ambayo mbali na kutinga EPL, imetwaa na ubingwa wa Championship msimu huu.

Na kwa Ipswich Town, ushindi huo unawafuta jasho walilovuja kwa miaka 22 mfululizo la kusaka tiketi ya kushiriki Ligi Kuu England.

Ipswich Town ilishuka daraja mwaka 2002 na baada ya hapo imepambana pasi na kukata tamaa katika kuisaka nchi ya ahadi.

Kupanda leo hapana shaka kunafuta kumbukumbu mbaya ya kichapo cha mabao 5-0 ambacho walikipata kutoka kwa Liverpool, siku ambayo walishuka daraja, Mei 11, 2002.

Wakati Ipswich wakiungana na Leicester City kwenda EPL, timu za Leeds United, Southampton, West Bromwich na Norwich City zitacheza mechi za Mchaki kusaka nafasi moja iliyobakia ya kucheza Ligi Kuu ya England msimu ujao.