Kaka afunguka ishu ya ndoa yake

Muktasari:

  • Ndoa ya Kaka na Caroline ilikuwa gumzo kwa kipindi kirefu kutokana na mapenzi ya wawili hao tangu staa huyo hajaanza kuzichezea timu kubwa Ulaya.

Staa wa zamani wa timu ya Taifa ya Brazil, Ricardo Kaka amefunguka sababu ya kuachana na mke wake Caroline Celico, na kusema alifanya kila kitu kuhakikisha anailinda ndoa hiyo, lakini ikashindikana.

Ndoa ya Kaka na Caroline ilikuwa gumzo kwa kipindi kirefu kutokana na mapenzi ya wawili hao tangu staa huyo hajaanza kuzichezea timu kubwa Ulaya.

Akiwa mchezaji mkubwa wa AC Milan mwaka 2005, Kaka alifunga ndoa na mpenzi wake huyo, lakini miaka kumi baadaye waliachana kwa siri kubwa.

Inaelezwa kuwa wawili hawa walianza kuwa wapenzi tangu wakiwa wadogo na iliaminika kuwa Kaka angemuacha mwanamke huyo endapo angepata fedha, lakini baadaye ilikuwa tofauti.

Hivi karibuni Caroline alisema kuwa aliachana na Kaka miaka kumi iliyopita kwa kuwa mwanasoka huyo alikuwa anampenda kupita kiasi, jambo ambalo kwake aliliona siyo sawa.

Hata hivyo, Kaka juzi kwa mara ya kwanza alizungumzia ishu hiyo akisema alitumia nguvu kubwa kuilinda ndoa yake lakini ilishindikana na bado anaamini Wakristo hawaoani ili kupeana talaka.

Kaka anasema ni zaidi ya miaka kumi sasa hayupo na mke wake pamoja na kwamba walijaaliwa watoto wawili, mmoja wa kiume na mwingine wa kike.

"Mwaka 2015, nilifunga ndoa na mke wangu, lakini baadaye aliniambia hataki tena kukaa kwenye ndoa, nilishtuka sana.

"Maneno yake yalikuwa machache, nataka kurudi Brazil, nataka kuishi kule na sitaki tena jambo linaloitwa ndoa tena.

"Nilitumia nguvu kubwa kuhakikisha kuwa nailinda ndoa yangu kwa kuwa Wakristo hatuwezi kufunga ndoa na kuachana, naamini nilikuwa na juhudi kubwa kuzuia talaka," alisema Kaka kwa uchungu.

Hivi karibuni Caroline alisema: "Kaka hakuwahi kunisaliti hata siku moja, alinipa mapenzi bora na kunipa familia, lakini nilikuwa sina furaha kuna kitu kilikuwa kinakosekana kwenye maisha yangu.

 "Tatizo ni kwamba alikuwa mtu muhimu sana kwangu hilo tu ndiyo tatizo hakuna jambo lingine."

Baada ya kuachana Kaka alianza harakati za kutafuta talaka, lakini anasema amekutana na ugumu.

 "Nilikaa mwenyewe mwaka mmoja na nilikijaribu kuona kama naweza kuishi kwenye mazingira hayo, nilikuwa nikijaribu kuimaliza hali hiyo nikizungumza na wachungaji kwa kuwa Biblia inasema huwezi kutoa talaka na mimi ni shahidi kwa hilo," alisema.

Hata hivyo, anasema mwaka 2017, alianza uhusiano na mpenzi wake wa sasa mrembo Carolina Dias na wanatarajia kuvishana pete baadaye mwaka huu, wakiwa tayari na mtoto mmoja mwenye mwaka mmoja.

Kaka mwenye miaka 41 ambaye amewahi kutwaa tuzo ya mchezaji bora wa dunia alifanikiwa kuzichezea timu kubwa duniani, Sao Paulo, AC Milan, Real Madrid na Orlando City kabla hajastaafu mwaka 2017.

Amefanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, pia Kombe la Dunia akiwa na Brazil aliyoichezea michezo 92.