Kambole azuia usajili Yanga

Muktasari:

  • Mashirikisho hayo yamefikia uamuzi huo baada ya aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo Lazarus Kambole kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.

Shirikisho la Soka la Kimataifa FIFA na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeifungia klabu ya Yanga kusajili wachezaji wa kimataifa na wa ndani.

Mashirikisho hayo yamefikia uamuzi huo baada ya aliyekuwa mchezaji wa timu hiyo Lazarus Kambole kushinda kesi ya madai dhidi ya klabu hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na TFF imesema Kambole aliishitaki Yanga kwa madai ya malimbikizo ya mshahara na fidia ya kuvunjiwa mkataba, ambapo timu hiyo ilipewa siku 45 kulipa pesa hizo na ilishindwa.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa kushindwa kutekeleza hukumu ndani ya muda husika ndio sababu ya timu hiyo kufungiwa kusajili usajili wa ndani na wa nje.

Pia, Aprili 14, 2024, TFF ilitoa taarifa ya kufungiwa usajili klabu hiyo baada ya kukiuka Annexe ya 3 ya kanuni ya uhamisho wa wachezaji RSTP ya FIFA pamoja na kutokuingiza uthibitisho wa malipo ya uhamisho wa mchezaji (ambaye hakutajwa jina) katika usajili (TMS) licha ya kukumbushwa kufanya hivyo.

Hata hivyo, FIFA iliitaka Yanga kutekeleza matakwa ya kikanuni na kuwasilisha taarifa kwa sekretarieti ya Kamati ya Nidhamu ya FIFA ambapo suala hilo lilifikishwa kwa ajili ya hatua zaidi.

Yanga ilimtambulisha Kambole raia wa Zambia Juni 16, 2022 akitokea Kaizer Chiefs ambapo Septemba,2022 iliachana na mchezaji huyo na kumpeleka kwa mkopo kwenye timu ya Wakiso Giant ya Uganda.

Kambole hakucheza mechi yeyote ya kimashindano akiwa ndani ya Yanga kwani alipata majeruhi katika mechi za kirafiki wakati timu hiyo ikijiandaa na msimu mpya wa 2022/2023.