Ligi ya Mabingwa ya kibabe Ulaya 

Muktasari:

  • Awali ilionekana kama Bayern ndiyo ina nafasi ya kutinga fainali na  kutokea ile ya mwaka 2013, iliyokutanisha Bayern na Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Wembley. 

Madrid, Hispania, Mabao mawili ya dakika za majeruhi yaliyofungwa na Mato Joselu yalitosha kwa Real Madrid kupindua meza na kuichapa Bayern Munich mabao 2-1 na kutinga kibabe fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.

Awali ilionekana kama Bayern ndiyo ina nafasi ya kutinga fainali na  kutokea ile ya mwaka 2013, iliyokutanisha Bayern na Borussia Dortmund kwenye Uwanja wa Wembley. 

Na hapo ingekuwa uwanja ni uleule na wababe ni walewale. Lakini, Bayern imeshindwa kulinda bao lake lililofungwa na Alphonso Davies dakika ya 68 baada ya kuruhusu nyavu zao kuguswa mara mbili dakika 89 na 91 na straika Joselu na hivyo kupata tiketi ya kwenda kuchuana na Dortmund kwenye fainali itakayopigwa Wembley, Juni Mosi.

Chama hilo la Los Blancos limetinga fainali kwa jumla ya mabao 4-3 baada ya sare ya 2-2 Uwanja Allianz Arena, Jumanne iliyopita.

Na sasa ni kipute cha Dortmund na Real Madrid. Kipigo hicho kwa Bayern kinafanya timu hiyo ya Thomas Tuchel kumaliza msimu huu mikono mitupu, bila taji lolote ikiwa ni msimu wa kwanza kwa straika Harry Kane katika kikosi hicho cha Allianz Arena.

Awali ilikuwa inatajwa kuwa Kane anakwenda Bayern ili kufanikiwa kutwaa kombe lake la kwanza, lakini mambo yameonekana kuwa magumu kwake na hivyo ni rasmi sasa anakwenda kumaliza msimu bila kombe lolote, ikiwa ni mara ya kwanza kwa Bayern kwa miaka ya hivi karibuni.

Ushindi huo umeibua ndoto za Los Blancos kuongeza taji la 15 la Ligi ya Mabingwa Ulaya huku ikiwa imebeba taji la La Liga msimu huu na hivyo inakwenda kwenye fainali ikiwa inataka kuhakikisha inatwaa ubingwa huo.

Dortmund yenyewe imetinga fainali baada ya kuisukuma nje Paris Saint-Germain kwa jumla ya mabao 2-0.

Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu itafanyika uwanjani Wembley, Juni Mosi na inaonekana kuwa timu zote zinakwenda kwenye Uwanja huo zikiwa tayari zimeshawahi kucheza hapo fainali.

Carlo Ancelotti

Kocha wa Real Madrid, Carlo Ancelotti ameendelea kuweka rekodi zake kwenye michuano hiyo baada ya kuwa kocha wa kwanza kufanikiwa kufika fainali ya michuano hiyo mikubwa barani Ulaya mara sita, kitu ambacho hakuna mwingine amewahi kufanya hivyo.

Alifika fainali msimu wa 2002/04, 2004/05, 2006/07, 2013/2014,2021/2022 na 2023/2024 katika misimu hii, kocha huyo ameweka rekodi ya kutwaa ubingwa huo mara nne akiwa anapewa nafasi kubwa ya kuchukua ubingwa msimu huu. 
Dondoo za Madrid ya kibingwa

Real Madrid kwa sasa imefanikiwa kutinga fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya 18 ikiwa ni mara saba zaidi ya timu nyingine yoyote.

Kitendo cha Bayern Munich kupoteza kimewafanya wapoteze mchezo wa 11 wa Michuano ya UEFA dhidi ya Real Madrid, ikiwa ndiyo timu iliyopoteza zaidi dhidi yao.

Mchezo wa huu ulikuwa wa sita msimu huu Real Madrid, wanaanza kuruhusu bao lakini mwisho wanaibuka na ushindi jambo ambalo limewafanya kuweka rekodi ya michuano hiyo kuanzia msimu wa 2016-17, ilipofanya yenyewe na mwisho ikitwaa ubingwa.

Staa wa Real Madrid Joselu, aliyefunga mabao ya nusu fainali msimu huu ameshafunga mabao matano kwenye michuano hiyo, manne amefunga dhidi ya timu za Ujerumani, mawili dhidi ya Union Berlin na Bayern Munich, anakuwa mchezaji wa tatu kufunga mabao mawili kwenye mchezo wa nusu fainali akitokea kwenye benchi tangu Georginio Wijnaldum alipofanya hivyo Mei 2019 (Liverpool vs Barcelona) na Rodrygo Mei 2022 (Real Madrid vs Manchester City).

Toni Kroos amefikisha michezo 150 ya Ligi ya Mabingwa amekuwa mchezaji wa saba kufikisha idadi hiyo.

Kinda wa Real Madrid Jude Bellingham juzi alicheza mchezo wake wa 31 kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya akiwa na umri wa miaka 21.


Vigogo wa fainali

Fainali itapigwa Juni 1 kwenye Uwanja wa Wembley, Dortmund inashika nafasi ya nane kwa ubora wa Uefa, ikiwa ilitwaa ubingwa msimu wa 1996/97, kocha wao ni Edin Terzić ambaye alianzia maisha yake ya ukocha kwenye akademi ya Dortmund mwaka 2010 akiwa hana rekodi kubwa.

Timu hii inamtegemea zaidi mkongwe Julian Brandt, mwenye miaka 27 akiwa amecheza kwenye timu hiyo kwa miaka minne.
Unajua? 

Dortmund inafika fainali kwa mara ya kwanza tangu msimu wa 2012/13, wakati vijana wa kocha Jürgen Klopp walipochapwa 2-1 na Bayern Munich kwenye Uwanja wa Wembley.

Real Madrid, inashika nafasi ya tatu kwa ubora wa Uefa, ikiwa imetwaa ubingwa huo mara 14, kocha wao Carlo Ancelotti ameweka rekodi ya kuchukua ubingwa mara nne, lakini pia ameipa Madrid ubingwa wa La Liga na kuwa kocha wa kwanza kutwaa kombe la ubingwa kwenye nchi za Italia, England, Ufaransa, Ujerumani na Hispania.

Mashabiki wanasubiri kuona kama kinda Jude Bellingham anaweza kutwaa ubingwa akiwa kwenye Uwanja wa nyumbani kwao Wembley, lakini wanasubiri kuona kiungo Luka Modric akitangaza kustaafu baada ya mchezo huu.