Mechi ya nafasi muhimu Ligi Kuu Bara

Muktasari:

  • Azam iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57, ikipoteza leo, maana yake itaitangulia Simba kwa pointi moja huku wapinzani wao hao wakibakia na faida ya mchezo mmoja mkononi ambao utawapa faida ya kusogea juu yao ikiwa watashinda.

Timu yoyote itakayopoteza mchezo baina ya Azam na Simba leo kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 12:15 itajiweka katika mazingira magumu ya kumaliza katika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara lakini itafuta rasmi ndoto za ubingwa.

Azam iliyo katika nafasi ya pili ikiwa na pointi 57, ikipoteza leo, maana yake itaitangulia Simba kwa pointi moja huku wapinzani wao hao wakibakia na faida ya mchezo mmoja mkononi ambao utawapa faida ya kusogea juu yao ikiwa watashinda.

Ni kama ilivyo kwa Simba ambayo ikipoteza itabakia na pointi zake 53 ambazo zitakuwa saba pungufu ya Azam ambayo itahitajika kupata ushindi katika mechi tatu kati ya nne zitakazofuata ili ijihakikishie nafasi ya pili ambayo itaifanya ishiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.

Ikiwa Simba itapoteza, itaondoka rasmi kwenye mbio za ubingwa na ikiwa hivyo kwa upande wa Azam itakuwa ni kama imerahisisha mbio za ubingwa kwa Yanga inayoongoza msimamo wa ligi hiyo.

Azam ambayo ni mwenyeji katika mechi ya leo, inaingia ikiwa inamtegemea zaidi kiungo mshambuliaji wake Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye ameshafumania nyavu mara 15 kwenye Ligi Kuu msimu huu.

Simba inaingia ikiwa inamtegemea mshambuliaji wake Freddy Koublan ambaye licha ya kuanza kwa kusuasua baada ya kujiunga na timu hiyo katika dirisha dogo la usajili, ameshapachika mabao matano kwenye ligi kuu hadi sasa.

Wakati Azam ikiingia ikiwa imetoka kushinda mechi nne kati ya tano zilizopita za ligi huku ikitoka sare moja, Simba yenyewe katika mechi tano zilizopita za ligi, imepata ushindi mara mbili, sare mbili na kupoteza moja.

Kumbukumbu za mechi tano zilizopita za Ligi Kuu baina yao, zinaonyesha kuwa shilingi imesimama kwani kila timu imeibuka na ushindi mara moja na zimetoka sare katika michezo mitatu.

Hamu ya wengi katika mechi ya leo ni kuona kama Azam FC inaweza kupata matokeo mazuri bila ya uwepo wa Prince Dube ambaye ameifunga Simba katika mechi tatu mfululizo zilizopita za Ligi Kuu.

Simba inategemea zaidi safu yake ya kiungo ambayo leo itamkosa Clatous Chama kuzalisha mabao yake huku Azam FC yenyewe hapana shaka itaendelea kuweka matumaini kwa mawinga wake katika kuzalisha na kufunga mabao.

Kaimu kocha mkuu wa Simba, Juma Mgunda amesema kuwa Azam ni timu bora na ndio maana ipo nafasi ya pili kwenye msimamo lakini wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi.

“Itakuwa mechi nzuri, Azam ni timu bora lakini tumejipanga kucheza na timu bora na tupo tayari kupambana ili kupata ushindi.

“Maandalizi ya mchezo yamekamilika, wachezaji wapo kwenye hali nzuri tayari kupambana na lengo letu ni kupata pointi tatu,” amesema Mgunda.

Kocha wa Azam FC, Bruno Ferry alisema kuwa anaamini mechi itakuwa ngumu na wamejipanga kuhakikisha wanapata ushindi ingawa ameomba waamuzi kuzitafsiri vyema sheria 17 za mchezo wa mpira wa miguu.

"Tunajua itakuwa mechi ngumu kwetu. Tupo tayari kucheza hii mechi na tunatumaini vyema. Wasiwasi mkubwa ni kuhusu refa. Sipendi sana kuzungumzia waamuzi. Kipindi hiki kuna uamuzi tata hivyo kesho (leo) hatupendi kuwepo na uamuzi tata.

"Tunahitaji mechi ichezeshwe kwa haki na timu bora icheze vizuri na ipate ushindi. Nadhani nimehitajika kusema hilo kwa vile wanatakiwa kufahamu kwamba tunaenda mwisho mwa msimu kila pointi moja ni muhimu," alisema Ferry.

Kwenye Uwanja wa Manungu Complex, Morogoro, Mtibwa Sugar inayoshika mkia kwenye msimamo wa ligi itaikaribisha Tabora United ambayo ipo katika nafasi ya 15 katika mechi itakayochezwa kuanzia saa 10 kamili jioni.

Ihefu ambayo ipo nafasi ya 11 kwenye msimamo wa ligi yenyewe itakabiliana na JKT Tanzania katika Uwanja wa Liti, Singida kuanzia saa 10.

Mechi nyingine leo itakuwa ni kwenye Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa ambapo Namungo FC itaikaribisha Dodoma Jiji kuanzia saa 2.30 usiku