Metacha, Sopu watemwa Stars

Muktasari:

  • Wachezaji wanne wa Taifa Stars ikiwa ni miongoni mwa 31 walioitwa kambini wametemwa katika orodha ya watakaokwenda kuipeperusha bendera ya timu hiyo nchini Ivory Coast katika Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon).

Dar es Salaam. Kipa Metacha Mnata na mshambuliaji Abdul Selemani 'Sopu' ni miongoni mwa wachezaji wanne wa Taifa Stars ambao hawajajumuishwa katika kikosi cha timu hiyo kitakachoshiriki Fainali za Mataifa ya Afrika (Afcon) mwaka huu huko Ivory Coast.

Kwa mujibu wa orodha ya vikosi vya timu zote 24 zitakazoshiriki fainali hizo iliyotolewa leo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF), Sopu anayechezea Azam na Metacha wa Yanga, hawamo katika majina ya wachezaji 27 walioorodheshwa katika kikosi cha mwisho cha Taifa Stars.

Mbali na Sopu na Metacha, wengine wawili ni Khleffin Hamdoun na Twariq Yusuf.

Wanne hao walikuwa miongoni mwa wachezaji 31 wa Taifa Stars ambao wapo kambini kujiandaa na fainali hizo lakini kwa mujibu wa kanuni za mashindano ya Afcon, idadi ya wachezaji wanaohitajika kikosini ni 27.

Kikosi cha wachezaji 27 wa Taifa Stars kitakachoshiriki AFCON mwaka huu kina makipa Aishi Manula, Beno Kakolanya na Kwesi Kawawa  wakati mabeki ni Ibrahim Bacca, Dickson Job, Mohamed Hussein, Abdulmalick Zacharia, Bakari Mwamnyeto, Novatus Miroshi, Miano Danilo, Haji Mnoga, Abdi Banda na Lusajo Mwaikenda.

Viungo ni Himid Mao, Mudathir Yahya, Mzamiru Yassin, Ben Starkie, Morice Abraham, Sospeter Bajana, Feisal Salum, Taryyn Allarakhia wakati washambuliaji ni Mohamed Sagaf, Cyprian Kachwele, Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Charles M'mombwa na Kibu Denis.