Mmoja afariki, wengine wajeruhiwa ajali za Simba na Yanga

MASHABIKI wa klabu za soka za Simba na Yanga, wamepata ajali katika maeneo tofauti alfajiri ya leo na taarifa za kipolisi zimethibitisha mtu mmoja amefariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Kwa mujibu wa viongozi wa Yanga na Simba tawi la Tunduma, wanasema yalikuwa magari matatu tofauti ya mashabiki yakiwa katika misafara miwili tofauti, ambapo gari la Simba kutoka Kiwira ndilo limepata ajali kubwa hadi kumpoteza dereva eneo la Vigwaza, mkoani Pwani.

Kwa upande wa msafara wa magari ya Yanga na Simba kutoka Tunduma wao ndio wamegongana na hakuna vifo bali mashabiki wawili wa Simba ndio wameumia na gari kuharibika.

Katibu Mkuu wa Simba Tawi la Tunduma, Dany Mgavilo ameliambia Mwananchi kuwa, gari walilokuwa wakisafiria liliigonga gari la Yanga kwa nyuma na kusababisha majeraha kwa watu wawili, Elias Mbukwa na Asifa Kaminyoge.

"Sisi ajali yetu hapa Doma hatukuumia sana isipokuwa gari ndilo limeharibika tunatafuta usafiri mwingine kuendelea na safari ila ya wenzetu kutokea Kiwira ndio dereva amefariki kule Vigwaza," amesema Mgavilo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Yanga Tawi la Tunduma, Esau Rwinga amesema wako salama na hakuna aliyeumia na wanaendelea kuchukuliwa maelezo Polisi ili waendelee na safari.

"Msafara wetu tumekuja na wenzetu Simba kutoka Tunduma tulipofika Duma gari la lililokuwa limewabeba mashabiki wa Simba lilitugonga kwa nyuma na kuharibika lakini kuwajeruhi wawili ila wengine kwa ujumla tuko salama," amesema Rwinga.

Kamanda wa Polii Mkoa wa Pwani, Pius Lutumo amethibitisha kutokea kwa kifo cha shabiki mmoja na majeruhi watatu katika ajali iliyohusisha gari aina ya Toyota Coaster na lori alfariji ya leo  eneo la Vigwaza mkoani humo.

"Ni kweli kumetokea ajali iliyosababisha kifo cha mtu mmoja na majeruhi watatu," amesema Kanda Lutumo.

Mashabiki hao wa Simba na Yanga walikuwa wakitokea Mbeya kwenda Dar es Salaam kuwahi mechi za robo fainali za Ligi ya Mabingwa Afrika za timu hizo zinazopigwa leo Ijumaa na kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Simba leo kuanzia saa 3:00 usiku itaikaribisha Al Ahly ya Misri ambao ni watetezi wa taji la michuano hiyo ikiwa ni mara ya nane kwao kukutana katika michuano ya CAF tangu mwaka 1985, huku kesho itakuwa ni zamu ya Yanga kuvaana na Mamelodi Sundowns ya Afrika Kusini.

Timu hizo zote zinatarajiwa kurudiana ugenini Aprili 5 kwa Yanga kuifuata Mamelodi jijini Pretoria, Afrika Kusini na Simba kwenda Cairo Misri kumalizana na wenyeji wao ambao katika mechi zao sita nane zilizopita ikiwamo ya Kombe la Washindi mwaka 1985 kila ikishinda nyumbani, Simba ikishinda 2-1 na kulala 2-0 ugenini.

Timu hizo zilikutana katika Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi mara mbili 2018-2019 na 2020-2021 na katika mechi za ugenini Simba ilifungwa 5-0 na 1-0 mtawalia na yenyewe kushinda 1-0 kwa kila mechi kabla ya kuvaana katika michuano mipya ya African Football League, kila moja kupata sare nyumbani, Simba ikianza na 2-2 kisha kulazimishwa 1-1 ugenini na kutolewa kwa faida ya bao la ugenini.