Mo Dewji atuliza hali ya hewa Simba

Mwekezaji wa asilimia 49 za hisa za Simba, Mfanyabiashara Mohamed Dewji amewahakikishia  mashabiki, wapenzi na wanachama wa klabu hiyo kuwa mambo mazuri yanakuja baada ya jana kufanya kikao na uongozi,benchi la ufundi na baadhi ya wachezaji wa timu hiyo.

Dewji ambaye kwa muda mrefu amekuwa kimya amesema kuwa anaamini kikao hicho kitakuwa na matunda chanya kwa timu hivyo Wanasimba hawapaswi kuikatia tamaa timu.

"Nimefanya kikao na viongozi wa Simba SC kujua changamoto zipo wapi na namna ya kuzitatua.

"Kikao kimeenda vizuri. WanaSimba tusife moyo, tuendele kushirikiana," ameandika Dewji kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii.

Kauli hiyo ya Dewji imekuja siku tano kabla ya Simba kuvaa na Yanga katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara utakaochezwa Jumamosi katika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuanzia saa 11 jioni.