Msala wa kwanza wa Mgunda Ligi Kuu

Siku moja baada ya kuachana na kocha wake Abdelhak Benchikha Simba inarudi uwanja  kwenye uwanja mgumu ugenini itakapokutana na wabishi Namungo ya Lindi.

Simba baada ya kuondokewa na Benchikha aliyerusha taulo kwa sababu za kifamilia akiachana na timu hiyo, leo kikosi chao kitakuwa chini ya kocha wa Juma Mgunda ambaye atasaidiana na Seleman Matola.

Matola wala sio mgeni kwa Namungo kwanza alikuwa hapohapo akimasaidia Benchikha lakini pia anaijua Namungo ambayo msimu huu akiwa kama kocha wa muda kabla ya ujio wa kocha huyo Mualgeria alilazimishwa sare ya bao 1-1 nyumbani akisawazisha kuinusuru timu hiyo isilale nyumbani.

Presha kubwa kwa wekundu hao ni kwamba inaweza kuwakosa wachezaji wake baadhi ambao ni majeruhi ambao ni staa wao Clatous Chama mwenye mabao saba kwenye ligi ambaye alipata majeraha kwenye mashindano ya Kombe la Muungano.

Mbali na Chama pia Simba inaweza kuwakosa mabeki Shomari Kapombe, Henock Inonga, kiungo Sadio Kanoute ambao nao wanapambana na majeraha mbalimbali.

Hata hivyo, Wekundu hao bado wana kikosi imara mbele ya Namungo ambapo ikiwa bila ya wachezaji hao ilibabe Kombe la Muungano ikiichapa Azam FC kwa bao 1-0.

Simba itaingia kwenye mchezo huo ikisaka ushindi wa 15 msimu huu, lakini hata kama itashinda na kufikisha pointi 49 bado haitaweza kutoka nafasi ya tatu ingawa itakuwa imebakiza mechi mbili za viporo ikiendelea kuwafukuza Azam FC iliyo nafasi ya pili na pointi 54 na Yanga iliyopo kileleni na alama 62.

Namungo itatakiwa kuwa makini na mshambuliaji Fredy Koublan ambaye ameanza kuonyesha makali yake akiwa tayari na mabao manne kwenye ligi tangu asajiliwe kwenye kipindi cha dirisha dogo.

Huu ni mtihani wa Simba ikiwa ugenini dhidi ya Namungo kwani haijawahi kuondoka na ushindi na leo itatakiwa kufanya kazi kubwa kuhakikisha inapata pointi tatu muhimu.

Akizungumzia mchezo huo Matola alisema wanafahamu kwamba itakuwa mechi ngumu lakini kikosi chake kimejipanga kuhakikisha kinapata ushindi mbele ya wenyeji wao.

"Hii ni mechi ngumu tumeshasahau kuhusu Kombe la Mapinduzi, tunakwenda kukutana na Namungo ambayo mchezo wa mwisho kati yetu ilituzia kushinda na kugawana pointi, tuna imani kwamba vijana wako sawa kutupa ushindi kwenye mchezo huu ,"alisema Matola.

Namungo ikiwa chini ya Kocha Mkongomani Mwinyi Zahera, bado inajitafuta kusaka muendelezo mzuri wa ushindi baada ya kushinda mechi yao ya mwisho dhidi ya Coastal Union kwa bao 1-0.

Huo ulikuwa ushindi wa pili kwa Zahera ambaye akiwa na kikosi hicho kwenye mechi zake tano za mwisho ameshinda mbili na kupoteza tatu.

Changamoto kubwa ambayo Namungo inapambana nayo ni safu yake ya ushambuliaji kukosa makali ambapo imefunga mabao mawili pekee kwenye mechi zake tano zilizopita ambapo Zahera amekiri kwamba mambo magumu kwa washambulaiji wake ambao kinara wa ufungaji ni Pius Buswita mwenye mabao manne.

"Tunakwenda kukutana na Simba tunawaheshimu timu kubwa kama hii kuna wakati inaweza kupata matokeo kutokana na wachezaji bora ilionao, tumejipanga kuendeleza ushindi wetu tukiwa nyumbani," alisema Zahera.

"Ni kweli safu yetu ya ushambuliaji bado haijafanya vizuri lakini tumeendelea kuwaongezea mbinu wachezaji wetu na tunaamini watakuwa na mabadiliko kwenye mchezo huu.”