Mtibwa yashinda mechi ya tano msimu huu

Muktasari:

  • Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili kutafuta nafasi ya kubaki kwenye ligi kuu msimu ujao, ambapo kabla ya mchezo wa leo Mtibwa Sugar ilikuwa nafasi ya 16 kwenye msimamo baada ya mechi 25 na alama 17, ikiwa imeshinda tano, sare tano na kupoteza 16, huku Tabora United ikiwa nafasi ya 15 na alama 23 katika michezo 25 waliyocheza.

Timu  ya Mtibwa Sugar bado inaitaka ligi kuu, ndivyo unavyoweza kusema baada ya leo Mei 9,2024  kufanikiwa kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Tabora United katika mchezo wa Ligi Kuu Bara uliopigwa kwenye Uwanja wa Manungu uliopo Turiani mkoani Mkoani Morogoro, ukiwa ni ushindi wake wa tano msimu huu.

Mchezo huo ulikuwa muhimu kwa timu zote mbili kutafuta nafasi ya kubaki kwenye ligi kuu msimu ujao, ambapo kabla ya mchezo wa leo Mtibwa Sugar ilikuwa nafasi ya 16 kwenye msimamo baada ya mechi 25 na alama 17, ikiwa imeshinda tano, sare tano na kupoteza 16, huku Tabora United ikiwa nafasi ya 15 na alama 23 katika michezo 25 waliyocheza.

Mashujaa wa Mtibwa Sugar kwenye mchezo huo walikuwa Jimyson Mwanuke  aliyefunga bao la kwanza dakika ya 15 ya kipindi cha kwanza baada ya kupokea pasi kutoka kwa mshambuliaji Charles Ilanfya huku bao la pili likifungwa na Charles Ilanfya dakika ya 56 baada ya kupewa pasi na Seif Karihe ambapo alifunga kwa kichwa huku lile la tatu likifungwa na Nickson Mosha dakika ya 79 ya mchezo huo.

Kivutio kikubwa katika mchezo huo alikuwa kiungo mshambuliaji wa Tabora United Najim Mussa ambaye alionekana kuwa maeneo muhimu katika mchezo huo huku kivutio kingine kikiwa ni timu hizo kuwahi kuingia uwanjani baada ya mapumziko ya kipindi cha kwanza kabla ya waamuzi kurejea jambo ambalo ni nadra kutokea.

Mtibwa Sugar ilishinda kwenye uwanja wao wa nyumbani Machi 9, ambapo waliifunga Tanzania Prisons mabao 2-1, na baada ya hapo imecheza michezo dhidi ya Geita ikatoka 2-2, ikafungwa 2-0 na KMC, ikafungwa 2-1 na  JKT Tanzania, na kupoteza dhidi ya Simba 2-0, sawa na Azam.

Licha ya Mtibwa Sugar kupata ushindi huo imeendelea kusalia mkiani mwa ligi hiyo ikiwa imekusanya pointi 20 baada ya michezo 26 huku ikiwa imefungwa  mabao 43 na kufungwa 26.
Kocha wa Tabora United, Masoud Djuma amesema wachezaji wake hawakucheza kwenye kiwango bora ndiyo maana timu yake imepoteza mchezo huo ambapo ameahidi kurejea kufanya vizuri mechi nne zilizosalia 

"Hatukuwa kwenye ubora wetu ndiyo maana tumepoteza mchezo huu, wapinzani wetu Mtibwa walikuwa bora kuliko sisi, tulimiliki eneo la kiungo lakini hata zile nafasi chache tulizotengeneza hatukuzitumia hivyo tunaenda kujipanga ili mechi zilizobaki tufanye vizuri na timu imalize ligi kwenye nafasi salama"

Kocha wa Mtibwa Zuberi Katwila amewapongeza wachezaji wake kwa kujituma ambapo  amesema ushindi huo unawapa kujiamini kuelekea mechi za ligi zilizobaki huku akisisitiza kuwa timu yake bado inahitaji kucheza Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.

"Nawapongeza wachezaji kwa kujituma na kupata matokeo, huu mchezo ulikuwa muhimu kwetu sote maana hatupo kwenye nafasi nzuri kwenye msimamo wa ligi, lakini tumeshinda, ushindi huu unatupa kujiamini ili tuweze kushinda michezo iliyobaki, hatujakata tamaa, lolote linaweza kutokea na kwa mechi nne zilizobaki tutacheza kufa na kupona ili ligi ikimalizika tuone tutakuwa wapi maana malengo yetu bado ni kucheza ligi kuu  msimu ujao," alisema Katwila.