Ratiba ya Ligi Kuu ilivyokuwa shubiri kwa ‘vibonde’

Kocha wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah 'Baresi'

Dar es Salaam. Timu nne zinazoshika mkia kwenye msimamo wa ligi zinakabiliwa na mechi za mtego za kumalizia msimu ambazo zinalazimisha kila moja kuchanga vyema karata zake ili iweze kukwepa janga la kushuka daraja vinginevyo mambo yanaweza kuwa magumu kwao mwishoni mwa msimu.

Uwepo wa mechi ngumu dhidi ya timu zilizo juu ya msimamo wa ligi ambazo zipo kwenye vita ya kuwania ubingwa na hata kumaliza katika nafasi ya pili, michezo ya ugenini pamoja na mwenendo usioridhisha wa Mtibwa Sugar inayoshika mkia, Tabora United iliyo nafasi ya 15, Mashujaa ambayo ni ya 14 na Geita Gold iliyopo nafasi ya 13 zinazipa timu hizo kila moja kazi kubwa ya kufanya katika michezo iliyosalia ili iweze kujinusuru.

Mtihani mkubwa upo kwa Mtibwa Sugar ambayo licha ya kutokuwa na mwenendo mzuri, inakabiliwa na mechi nne ngumu kati ya sita ilizobakiza huku ikizidiwa kwa pointi sita na timu iliyo juu yake kwenye msimamo wa ligi.

Mechi hizo nne, ni mbili za nyumbani dhidi ya Yanga na Azam FC ambazo sio tu zinaongoza msimamo wa ligi lakini pia zimekuwa na kiwango bora na mwendelezo wa kufanya vizuri.

Mechi nyingine mbili ngumu ni za ugenini dhidi ya Mashujaa na Ihefu na hilo linachagizwa na rekodi isiyovutia msimu ya Mtibwa Sugar ugenini ambapo katika mechi 13 ilizocheza ugenini kwenye ligi msimu huu imekusanya pointi sita tu kati ya 17 ilizonazo, ikishinda mechi moja, kutoka sare tatu na kufungwa michezo tisa huku ikifunga mabao tisa tu yenyewe kuruhusu mabao 22.

Mbali na michezo dhidi ya Azam na Yanga, Mtibwa Sugar pia itakuwa nyumbani katika mechi dhidi ya Namungo na Tabora United.

Tabora United ambayo ipo nafasi ya 15, nayo ina mtihani mgumu kwani imebakiza mechi mbili tu nyumbani ambazo ni dhidi ya Mahujaa na Ihefu ambazo zote zipo katika mapambano ya kuwania kubaki.

Hapana shaka presha kubwa ni mechi nne za ugenini ambazo mbili kati ya hizo ni dhidi ya Yanga inayoongoza msimamo wa ligi na Simba inayoshika nafasi ya tatu, ingawa nyingine mbili ni dhidi ya Mtibwa Sugar na Namungo.

Matokeo ya ugenini yamekuwa sio mazuri kwa Tabora United msimu huu ambapo hawajapa ushindi hata mara moja katika mechi 11 walizocheza hadi sasa, wakitoka sare tano na kupoteza sita huku wakifunga mabao matano na wenyewe wameruhusu mabao 15.

Mashujaa inayocheza na Yanga leo, inaweza kuwa ndio yenye ratiba iliyo na nafuu kidogo kulinganisha na nyingine tatu zilizopo kwenye kundi la timu nne zinazoshika mkia.

Timu hiyo ya mkoani Kigoma baada ya kucheza na Yanga leo, itakuwa na mechi mbili tu ugenini dhidi ya Tanzania Prisons na Tabora United huku michezo mitatu ya nyumbani ikiwa ni dhidi ya Mtibwa Sugar, KMC na Dodoma Jiji FC.

Kwa upande wa Geita Gold, yenyewe baada ya kupoteza jana dhidi ya JKT Tanzania kwa mabao 2-0, sasa imebakiza mechi mbili tu nyumbani ambayo ni moja dhidi ya Azam FC na nyingine ni dhidi ya Coastal Union.

Geita ambayo mechi za ugenini msimu huu imeshinda mbili kati ya 11, mechi ambazo haitokuwa mwenyeji ni dhidi ya Namungo Simba na Singida Fountain Gate.

Kocha wa Mtibwa Sugar, Zuberi Katwila alisema wanaamini lolote linaweza kutokea licha ya ugumu wa mechi zilizo mbele yao.

"Unajua kwanza unatakiwa upate pointi. Ukishapata pointi katika hesabu hizi zinazopigika ndio unajua ufanyaje. Tunatakiwa kuwa wavumilivu katika kiipindi hiki ili tuweze kupata matokeo mazuri tuweze kuwa katika nafasi nzuri," alisema Katwila.

Nahodha wa Tabora United, Said Mbatty alisema wachezaji wa timu hiyo wanapaswa kuamka ili kuinusuru isifanye vibaya zaidi.

"Muda hautusubirii na mechi zinazidi kupungua hivyo sisi wachezaji tusipokaza buti na kupata matokeo mazuri tutajiweka katika hatari ya kushuka daraja. Ratiba ni ngumu lakini hatuna namna inabidi tucheze kwa ajili yetu, kwa ajili ya timu na watu wa Tabora," alisema Mbatty.

Kocha wa Mashujaa FC, Mohamed Abdallah 'Baresi' alisema watahakikisha wanafanya vizuri hasa mechi za nyumbani.

"Mechi za ugenini huwa sio rahisi kupata matokeo mazuri kuliko za nyumbani. Ni kweli sisi tuna faida ya kuwa na mechi nyingi nyumbani ambayo tunapaswa kuhakikisha tunashinda ili kupata pointi tisa ambazo zitatuweka katika nafasi nzuri. Lakini pia hata hizo za ugenini tunatakuwa kupata ushindi," alisema Baresi.