Raya ashinda tuzo, Arsenal ikiichapa Chelsea 5-0

Muktasari:

  • David Raya yupo kwa mkopo Arsenal akitokea Brentford kukiwa na kipengele kwenye mkataba huo cha kununuliwa moja kwa moja

Dar es Salaam. Kipa wa Arsenal, David Raya ameshinda tuzo ya kipa bora wa msimu katika Ligi Kuu England (EPL) baada ya kuiongoza Arsenal kuibuka na ushindi wa mabao 5-0 dhidi ya Chelsea jana.

Kitendo cha mechi hiyo kumalizika bila nyavu za Arsenal kutikisika kimemfanya Raya afikishe mechi ya 14 bila kuruhusu bao (clean sheet), idadi ambayo haiwezi kuvukwa na kipa mwingine yeyote msimu huu.

Kwa mujibu wa kanuni za EPL, kipa ambaye amacheza idadi kubwa ya mechi bila kuruhusu bao, ndiye huwa mshindi wa tuzo ya kipa bora.

Na ikitokea makipa zaidi ya mmoja wamelingana kwa kucheza idadi kubwa ya mechi bila nyavu zao kutikiswa, kila mmoja hupata tuzo hiyo.

Haikuwa siku nzuri kwa Raya peke yake bali pia Ben White, Kai Havertz na Leandro Trossard ambao walifunga mabao hayo muhimu yaliyoifanya Arsenal ifikishe pointi 77 na kuendelea kuongoza msimamo wa ligi hiyo.

Trossard alifungulia sherehe ya mabao ya Arsenal kwa kuifungia bao la kuongoza dakika ya nne ya mchezo akimaliza pasi ya Declan Rice, bao ambalo lilidumu hadi muda wa mapumziko.

Kipindi cha pili ndio kilikuwa kigumu zaidi kwa Chelsea ambapo ilijikuta ikiruhusu mabao manne ambayo yalifungwa na nyota wao wa zamani, Kai Havertz na beki wa zamani wa Brighton, Ben White.