Sababu ya mwamuzi wa Dortmund kulia uwanjani

Muktasari:

  • Wajerumani hao walifanikiwa kutinga fainali baada ya kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-0 na sasa watavaana na Real Madrid ambayo iliichapa Bayern Munich kwa jumla ya mabao 3-2.

Paris, Ufaransa, Mwamuzi wa mchezo wa nusu fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya PSG na Borrusia Dortmund, Daniele Orsato juzi alimwaga machozi uwanjani baada ya kupuliza filimbi ya kumaliza mchezo huku Dortmund ikitinga fainali.

Wajerumani hao walifanikiwa kutinga fainali baada ya kupata ushindi wa jumla ya mabao 2-0 na sasa watavaana na Real Madrid ambayo iliichapa Bayern Munich kwa jumla ya mabao 3-2.
Mashabiki walishangaa kumuona mwamuzi huyo akilia baada ya kupuliza filimbi ya mwisho na wengi walifikiri anafanya hivyo kutokana na makosa aliyofanya kwenye mchezo huo.

Orsato, ambaye alianza kuwa mwamuzi wa FIFA tangu mwaka 2010, hakuwa na mchezo mzuri baada ya kulalamikiwa kuwa aliinyima penalti PSG baada ya beki wa Dortmund  Matts Hummels kumwangusha Dembele kwenye boxi lakini badala yake akatoa mpira wa adhabu.  

Baada ya mchezo huo, mwamuzi huyo alionekana akisali, huku akifuta machozi, lakini imefahamika kuwa siyo makosa hayo yaliyokuwa yakimliza bali huu ulikuwa mchezo wake wa mwisho kuchezesha kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.

Mwamuzi huyo raia wa Italia mwenye miaka 48, hatachezesha tena michuano hiyo na mashindano yake makubwa yatakuwa yale ya Euro baadaye mwaka huu na baada ya hapo ataachana kabisa na kazi hiyo ya uamuzi.

Orsato anatajwa kuwa mmoja kati ya waamuzi bora kuwahi kutokea nchini Italia, akiwa ameshachezesha michezo mingi mikubwa, ukiwemo ule wa fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya kati ya Bayern Munich na PSG mwaka 2020.

Mwamuzi huyo ambaye amechezesha michezo mingi ya Ligi Kuu ya Italia Seria A, msimu huu na alitajwa na Shirika la Ujerumani la Historia na Takwimu (IFFSH) linalotambuliwa na Shrikisho la Soka la Kimataifa (Fifa), kuwa mwamuzi bora wa mwaka 2020.

Pia alichezesha mchezo wa ufunguzi wa Kombe la Dunia kati ya wenyeji Qatar walipovaana na Ecuador mwaka juzi, kabla hajachezesha mchezo wa nusu fainali kati ya Argentina na Croatia, ambapo alilaumiwa na kiungo wa Croatia Luca Modric kuwa alichezesha vibaya.

Manchester United wanamfahamu mwamuzi huyo ambaye alichezesha mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya PSG mwaka 2019, mchezo ambao alitoa kadi kumi, huku akimtoa kiungo wa United Paul Pogba kwa kadi nyekundu