Simba fasta kuiwahi Yanga

Muktasari:

  • Simba ilitua Zanzibar Jumanne na kufanya mazoezi ya kwanza siku hiyo hiyo na jana ilifanya tena mazoezi ya pili kisha leo kufanya awamu ya tatu lakini Mwanaspoti limepenyezewa huenda baada ya hapo ikavuka maji na kurejea Dar tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mechi Jumamosi.

SIMBA ipo visiwani Zanzibar ilikoweka kambi maalumu kwa ajili ya mechi ya 'Kariakoo Derby' dhidi ya Yanga itakayopigwa Jumamosi Aprili 20 uwanja wa Benjamin Mkapa, lakini Wekundu wa Msimbazi hao tayari wameanza safari ya kuwawahi Wananchi ambao watakuwa wenyeji wa mechi hiyo.

Simba ilitua Zanzibar Jumanne na kufanya mazoezi ya kwanza siku hiyo hiyo na jana ilifanya tena mazoezi ya pili kisha leo kufanya awamu ya tatu lakini Mwanaspoti limepenyezewa huenda baada ya hapo ikavuka maji na kurejea Dar tayari kwa maandalizi ya mwisho kabla ya mechi Jumamosi.

Chanzo cha kuaminika kutoka kambini Simba, kimeliambia Mwanaspoti, timu hiyo itarejea Dar es Salaam leo Alhamisi kimya kimya kwa ajili ya maandalizi ya mwisho.

"Tunatarajia kurudi Dar leo, hatujathibitisha ni muda gani lakini iko hivyo. Kuna baadhi ya taratibu inabidi tuzifanye tukiwa hapo," kilieleza chanzo chetu.

Ofisa Habari wa Simba Ahmed Ally amesema taarifa kamili itatoka kwenye mitandao rasmi ya klabu hiyo.

"Tutatoa taarifa rasmi lini tunarejea kupitia mitandao yetu," amesema Ahmed.

Hata hivyo, kulingana na taratibu za Bodi ya Ligi, mkakocha na manahodha wa timu zote mbili wanatakiwa kuzungumzia maandalizi kamili ya mchezo siku moja kabla ya mechi, pia timu ngeni, itafanya mazoezi ya mwisho kwenye uwanja ambao mechi itapigwa na muda sawa na ule wa mchezo jambo ambalo kwa mechi hii Simba ndio inapaswa kufanya hivyo Ijumaa.