Waarabu sasa wamwania  Mourinho

Kwa mujibu wa ripoti kutoka The Sun, kocha wa zamani wa AS Roma na Manchester United Jose Mourinho yupo katika mazungumzo na baadhi ya timu za Saudi Arabia kwa ajili ya kurudi kazini baada ya kuwa nje kwa  muda tangu afungashiwe virago na Roma Januari mwaka huu.

Kocha huyu ambaye amewahi pia kuzifundisha Chelsea, Tottenham, Real Madrid na FC Porto aliwahi kuhusishwa na Chelsea kwa ajili ya kuchukua mikoba ya Maurico Pochettino lakini dili likafeli kwa kile kilichoelezwa kwamba alikataa.

Kwa mujibu wa mwandishi wa habari  Ben Jacobs, Al-Qadsiah ya Saudi Arabia imeshaanza kuzungumza na Jorge Mendez ambaye ni wakala wa Mourinho ili kumpata kocha huyo kwa msimu ujao.

Timu hiyo ambayo ipo katika nafasi nzuri ya kupanda Ligi Kuu kutoka Ligi Daraja la kwanza ambako ipo kwa sasa imepanga kufanya mageuzi makubwa dhidi ya timu nne zinazomiliikiwa na Public Investment Fund (PIF) ambazo ni  Al-Ittihad, Al-Ahli, Al-Nassr and Al-Hilal.

Al-Qadsiah, kwa sasa maskani yake ipo Mji wa  Al Khobar na inamalikiwa na kampuni ya mafuta ya  petroli  Aramco.

Kwa mujibu wa taarifa Mourinho atawasili jijini Al Khobar mwezi huu kwa ajili ya kufanya mazungumzo zaidi kabla ya kuajiriwa.
Awali Mourinho alikataa pesa kibao kwa kazi ya kuifundisha  Al-Shabab na inadaiwa aliwaambia kwamba anataka kufundisha timu ambayo itakuwa inampa motisha sio pesa pekee.

Kocha huyu mwenye umri wa miaka 65, hivi karibuni amekuwa akionekana kwenye mashindano mbalimbali ya magari na pikipiki akiwa anatumia muda wake kwa ajili ya kupumzika kabla ya kurejea uwanjani.