Azam Pay imeleta mapinduzi katika huduma za malipo za kidijitali

Teknolojia ya huduma za kifedha kwa njia ya kielektroniki imesaidia kwa kiasi kikubwa kuendesha uchumi katika kufanikisha maendeleo kwa ujumla.

Hii ni kwa sababu matumizi ya huduma za kifedha kupitia teknolojia mbalimbali yameongezeka ambapo imeonekana eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara ndilo limekuwa kinara wa kubuni na kutumia huduma hizi.

Tanzania ikiwa moja ya nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara imekuwa moja ya nchi zilizopokea kwa mikono miwili teknolojia hii ya huduma za kifedha ambapo kampuni mbalimbali zimekuwa zikibuni njia rahisi ili kurahisisha malipo.

Moja ya kampuni ambazo zinatumia vyema teknolojia katika kurahisisha ufanyaji wa huduma za kifedha ni Azam Pay.

Kampuni hiyo hutoa mifumo na njia mbalimbali ambazo huwezesha urahisi na salama kwa watu binafsi na wafanyabiashara kufanya huduma za malipo kwa njia ya kieleketroniki.

Malengo ya Azam Pay ni kuwezesha Tanzania kufikia huduma za kifedha za kidijitali ambazo zina bei nafuu na salama zinazochochea ukuaji endelevu wa uchumi.

Meneja Mauzo wa Azam Pay Kitengo cha Malipo, Shadrack Kamenya anasema kampuni hiyo imekuwa ikitoa mifumo na masuluhisho ambayo huwasaidia wafanyabiashara wakubwa, wa kati na wadogo kufanya na kupokea malipo kwa njia za kidijitali zenye unafuu na salama.

“Mteja wa Azam Pay ni mtu ama kampuni yoyote yenye mahitaji ya njia za malipo za kidijitali. Mfano kampuni inahitaji wateja kulipia huduma fulani kwa njia ya mtandao, sisi tunayo teknolojia ya kuwezesha kutekeleza jukumu hilo kwa kuwa kiungo kati ya kampuni, watoa huduma za kifedha na wateja,” anasema   Kamenya.

Anasema Azam Pay inatumia teknolojia kufanya malipo kwa njia kuu tatu ambazo ni simu, kadi na benki. “Malipo kwa njia ya simu kupitia mtandao yanawezesha wateja kununua huduma ama bidhaa kupitia programu tumishi za simu (Apps) ambayo kitaalamu njia hii inaitwa “Online checkout payment”.”

Anasema katika njia hii pia mteja anaweza kufanya malipo ya bili mbalimbali ikiwemo za Serikali kama vile umeme, vifurushi vya visimbuzi nk ambayo malipo haya yanafanyika kwenye ukurasa wa huduma za kifedha wa mtandao husika wa simu.

Anasema Azam Pay inatoa huduma za mfumo wa malipo kwa njia ya kadi (Visa na MasterCard) ambapo mteja anaweza kufanya manunuzi ya huduma na bidhaa kwa kutumia kadi.

“Kupitia huduma hii Azam Pay inaunganisha jukwaa la malipo la kampuni pamoja na huduma ama bidhaa inazotoa kisha mteja anaweza kutumia kadi yake kufanya malipo mahali popote na wakati wowote,” anasema Kamenya.

Anasema huduma ya tatu ni malipo kwa njia ya benki ambapo wana mfumo unaowezesha wateja kuunganisha akaunti zao za benki moja ka moja na programu mbalimbali (Apps) za malipo.

“Teknolojia hii imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza kiwango cha watu kutembea na fedha taslimu pamoja na kurahisisha upatikanaji wa bidhaa na huduma,” anasema Kamenya.

Kamenya anasema tangu walipoanza kutoa huduma zao, kamapuni hiyo imejitanabaisha kama mtoaji wa programu bora za malipo kwa njia ya kidijitali (Application Programing Interface, API) ambazo zinasaidia kuunganisha biashara na huduma za kifedha ili wafanyabiashara waweze kufanya na kupokea malipo kwa urahisi na usalama.

Anasema wateja wa Azam Pay wamegawanyika katika makundi matatu ambayo ni; wateja wakubwa wenye ujuzi na miundombinu ya teknolojia ambao hupewa mifumo hii na kuindesha wenyewe.

Kundi la pili ni wateja wa kati ambao wao wana ufahamu kidogo wa teknolojia lakini hawana utaalamu wa ubobevu wa kuendesha mifumo hii. “Wateja hawa tunawasaidia kwa kuwapa teknolojia zilizorahisishwa ili kuweza kukidhi mahitjai yao.” anasema Kamenya.

Kundi la mwisho ni wateja wadogo ambao hawana ujuzi wowote hukusu teknolojia ambao wenyewe wametengenezewa kurasa za malipo (payment page) ambayo mfanyabiashara anaweza kuingia na kutengeneza ukurasa wake ambao utamsaidia kutengeneza “link” ya malipo ambayo wateja wataitumia kwa ajili ya kufanya malipo ya bidhaa ama huduma kupitia simu ya mkononi.

Kuhusu usalama wa mifumo ya Azam Pay Kamenya anasema ni kipaumbele chao cha kwanza kwani wapo chini ya kanuni na sheria za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) ambayo inahitaji kila kampuni inayotoa huduma hizo kuwa na mifumo imara inayowezesha kulinda taarifa za wateja wake.

“Azam Pay tuna leseni ya BoT na kama unavyofahamu sheria na kanani za benki kuu zinasisitiza sana kulinda na kutunza taarifa za siri za wateja hivyo tuna mifumo imara ya kusimamia usalama wa taarifa hiz,” anasema Kamenya.