Fahamu kuhusu utaratibu wa madai na fidia ya bima

Mpendwa msomaji wa ukurasa rasmi wa Kamishna wa Bima, karibu katika muendelezo wa makala hizi ambapo leo Kamishna anazungumzia kuhusu utaratibu na hatua stahiki za kudai fidia ya bima.

Tunafahamu pia Tanzania ime­timiza miaka 60 ya Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar hivyo pia Kamishana anatumia ukurasa huu kuzungumzia maswala machache yanayohusu bima na Muungano. Tafadhali fuatilia.


Sheria inavyoakisi kuwa TIRA ni taasisi ya Muungano

Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania ni Taasisi ya Muungano iliyoanzishwa kupitia kifungu cha 5 cha Sheria ya Bima sura ya 394, na kwa mujibu wa kifungu cha 6 cha Sheria hiyo inatekeleza majukumu yake chini ya usimamizi wa Wizara ya Fedha ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kifungu cha 2 cha Sheria ya Bima kinabainisha kuwa Sheria hii itatumika pande zote za Muungano.

Mamlaka inaongozwa na Kamishna wa Bima akisaidiwa na Naibu Kamish­na wa Bima walioteuliwa na Rais wa Jamhuri ya Mungano kwa Mamlaka aliyopewa kupitia vifungu vya 7 na 8 vya Sheria ya Bima. Ili kuakisi tas­wira ya Muungano, sheria hii kupitia kifungu cha 8(2) inaeleza kwamba, ikiwa Kamishna wa Bima atateuliwa kutoka upande mmoja wa Muungano, basi Naibu Kamishna atatoka upande mwingine wa Muungano. Mfano kwa sasa, Kamishna anatokea Tanzania Bara na Naibu Kamishna wa Bima anatokea Tanzania Visiwani.

Makao Makuu yapo Dodoma. Aidha, katika kurahisisha majukumu ya kiutendaji kwa pande zote mbili za Muungano TIRA ina ofisi Zanzibar na kwa sasa ina Ofisi nyingine mbili za Kanda huko Zanzibar, yaani Unguja na Penda.

Kwa Tanzania Bara, halikadhalika pia Mamlaka ina ofisi yake ndogo jijini Dar es Salaam na pia ina ofi­si za kanda 8 zilizopo katika mikoa mbalimbali ikiwemo kanda mpya ya Tanganyika iliyopo mkoani Katavi.

Katika kudumisha dhima ya Muun­gano TIRA inafanya kazi kwa karibu na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Makatibu Wakuu wa Wiz­ara mbalimbali lakini pia Makati­bu Wakuu wa Wizara wa Tanzania Bara. Tunapoadhimisha Miaka 60 ya Muungano TIRA inajivunia mchango wake katika sekta ya bima kwa mfano katika kampuni za bima 36 ilizosajili kampuni Mbili zipo Zanzibar, katika Wakala 1096 Wakala 80 wapo Zanzi­bar, katika Wataalamu 116 wa ushau­ri wa bima wataalamu Wanne wapo Zanzibar na Katika Benki Wakala 30, Zanzibar wapo Sita. Watoa huduma wote hao wanafanya biashara ya bima kwa pande mbili za muunga­no bila mipaka. Wateja wa bima pia hawafungwi kupata huduma kutoka sehemu yeyote ya Muungano.

Tukirudi kwenye mada inayohusu utaratibu na hatua za kudai ya bima ni vyema kwanza kufahamu yafua­tayo;

Majukumu ya TIRA yameanish­wa kwenye kifungu cha 6, na yale ya Kamishna yameainishwa kwenye kifungu cha 11 cha Sheria ya Bima. Mamlaka ina jukumu kuu la kumlin­da mteja wa bima. Katika kutekeleza majukumu hayo, TIRA inahakikisha kwamba wateja wa bima wanapa­ta fidia stahiki na kwa wakati huku ikizuia au kuondoa migogoro kwa kutoa miongozo na elimu kwa wadau wote katika sekta ya bima. Miongo­zo hiyo Pamoja na mambo mengine imeweka utaratibu wa kushughulikia madai.


I. Ushughulikiaji wa madai katika bima

Mamlaka imetoa Muongozo wa kushughulikia Madai ya bima una­opatikana kwenye tovuti ya Mamla­ka. Hata hivyo Ili kuelewa utaratibu wa madai ya Bima, ni vyema kujua maana ya baadhi ya Misamiati inayo­tumika.


i. Madai ya bima

Haya ni maandishi ya mdai dhidi ya Kampuni ya Bima kudai urejesho au fidia kutokana na hasara/maumi­vu/uharibifu uliosababishwa na kuto­kea kwa janga lililokingwa na bima


ii. Fidia ya bima

Huu ni urejesho wa gharama/ hasara kutokana na janga lililokingwa kibima/katiwa bima


iii. Malalamiko

Ni hali ya kutoridhika kuhusu hudu­ma au bidhaa inayotolewa na watoa huduma. Inaweza kuhusisha, lakini inapaswa kutofautishwa na madai na haijumuishi maombi ya taarifa (mfano-kucheleweshwa, kutojibu au kutolipwa ndani ya muda wa kisheria wa siku arobaini na tano, kutokupewa mkataba wa bima, kufuta bima pasi­po sababu, kutopakiwa bima katika mfumo TIRAMIS.


a. Misingi ya fidia ya kibima

Ili fidia ya bima iweze kutekeleze­ka kuna misingi na sheria ambazo zinatakiwa kufuatwa. Sheria hizo ni; sheria (ya Bima ya Vyombo vya Moto Sura ya 169 [R.E. 2002], na Sheria ya Bima, Sura 394, sheria ya Mikataba, Sura.345 R.E 2019, Misingi ya Makosa ya Madhara / Sheria ya Sheria ya Vifungu Mbalimbali vya Ajali mbaya (Fattal Accident Mis­cellenous Provisions Act, Cap 310), Sheria ya Ukomo wa Muda (Law of Limitations Act, Cap 89, mkataba wa Bima (kutegemeana na aina/Daraja ya Bima) na miongozo ya kiutendaji kwa soko (miongozo ya fidia za bima kwa majeruhi na vifo na miongozo ya kushughulikia madai ya bima.


b. Aina kuu za fidia ya bima

Kuna aina kuu mbili za fidia ya bima ambazo ni; fidia ya jumla (kipa­to kilichopotea/kitakachopotea, maumivu na mahangaiko, ukosefu wa utegemezi).

Aina nyingine ni fidia maalum yan­ayothibitika kwa nyaraka- matumizi/ hasara kutokana na janga lililoking­wa kibima kama vile usafiri, matiba­bu, gharama za matengenezo, kuvuta gari na gharama za mazishi, vifaa tiba.


c. Aina kuu za madai ya fidia

Madai ya mkata bima kwa uharibi­fu wa mali yake (own property dam­age, madai ya mtu wa tatu kwa uharibifu wa mali (third Party Property damage Claim), madai ya mtu wa tatu majeruhi (third-party bodily injury claim) na madai ya mtu wa tatu kwa kifo (third-party death claim).


d. Utaratibu na hatua stahiki za kudai fidia ya bima

Utaratibu na hatua za kudai fidia hutegemea aina ya madai. Utarat­ibu na hatua stahiki ni pamoja na; kutoa taarifa ya kutokea kwa tukio kwa wakati (Kwa polisi na kwa Kam­puni), kupata taarifa za kipolisi juu ya tukio husiika, kukusanya uthibitisho wa gharama au hasara mfano; matibabu risiti, usafiri, vifaa tiba, matengenezo, kuvuta gari, n.k, kuandaa taarifa za kibima (risiti ya malipo, mkataba au kava Note), kuandaa taarifa za umiliki wa Chom­bo/kifaa-mfano kadi ya gari, kuan­daa nyaraka za Utambulisho-Leseni, Kuandaa madai- (unadai nini/kia­si gani-kwa barua na kuwasilisha madai kwa kampuni ya bima.


e. Haki na wajibu wa mdai

Wajibu wa mdai ni pamoja na; kudai fidia, kuandaa madai (hatua zote), kuwasilisha madai, kufuatilia madai na kuwa mkweli katika kudai fidia (udanganyifu unaweza kusababisha kukataliwa kwa dai na kuchukuliwa hatua za kisheria.

Haki ni pamoja; kupe­wa orodha ya nyaraka zinazohita­jika katika madai, kupokelewa kwa dai na kupewa taarifa ya kupokelewa dai lake, kulipwa fidia stahiki kwa mujibu wa sheria, kanuni, mkataba na miongozo na kushughulikiwa au kupata ufumbuzi wa malalamiko kwa wakati.


f. Utaratibu wa malalamiko

Katika utaratibu wa kuwasilisha malalamiko vitu vikubwa vinavyozin­gatiwa ni pamoja na; sifa za lalamiko, aina/sababu za lalamiko, nani anawe­za kuleta lalamiko/sifa za mlalami­ka, njia za kuwasilisha lalamiko na mchakato na utaratibu wa kushughu­likia lalamiko.


g. Sifa za lalalamiko

Malalamiko dhidi ya huduma au bidhaa za mtoa huduma za bima ali­yesajiliwa, malalamiko kuhusiana na tukio lililotokea si zaidi ya mia­ka mitatu iliyopita na malalamiko mengine yoyote yatakayoonekana kuwa ya kweli kama mamlaka itaka­vyoamua.


h. Aina/sababu za kulalamika/ lalamiko

k u c h e l e ­wa kutatua malalamiko, kutozin­gatia Kifungu cha 131(1) cha Sheria ya Bima, kufuta mkataba wa Bima, kutorejeshewa malipo ya ada ya bima, ucheleweshaji wa Uchunguzi au tathmini ya madai, matumizi ya lugha chafu kwa wateja, kutolipa kamisheni na ada, kukiuka vigezo na masharti ya mkataba wa bima, watoa huduma wa bima waliosajiliwa kuto­kutoa majibu kwa wateja na jambo lingine lolote linalohusiana na viten­do vya watoa huduma za bima.


i. Nani anaweza kuleta lala­miko

Anayeweza kuleta lalamiko ni pamoja na; mkatabima, mtu wa tatu, watoa huduma za bima waliosajiliwa, mwakilishi wa kisheria kwa niaba ya mwenye bima au mnufaika, msimam­izi wa mirathi, mnufaika wa mkataba wa bima, Watoa huduma za bima na mtu mwingine yeyote aliyeidhin­ishwa.


j. Njia za kuwasilisha lalamiko

Malalamiko yanaweza kupokele­wa kwa maandishi au kwa mdomo ikiwa ni pamoja na; barua ili­yoandikwa kwa Kamishna wa bima, barua pepe kwa [email protected] au anwani nyingine yoyote ya barua pepe iliyoainishwa ya mamlaka, mfumo wa malalamiko una­opatikana kwenye tovuti ya mamlaka (www.tira.go.tz), kwa kujaza fomu ya malalamiko na njia nyingine yoyote kama itakavyoagizwa na Mamlaka.