Serikali Mtandao na mageuzi makubwa ya sekta ya Tehama nchini

Muktasari:

Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) duniani yameifanya dunia kwa sasa kutekeleza sehemu ya shughuli zake kidijitali na suala hili limebebwa kama ajenda ya dunia katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia.

By Rainer Budodi

Maendeleo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) duniani yameifanya dunia kwa sasa kutekeleza sehemu ya shughuli zake kidijitali na suala hili limebebwa kama ajenda ya dunia katika nyanja zote za kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni na kiteknolojia.

Kutokana na kasi hiyo ya maendeleo, Serikali ya Tanzania iliamua kuweka mfumo wake madhubuti wa kusimamia matumizi ya teknolojia hiyo kwa taasisi za umma. Mwaka 2012 Serikali ilianzisha Wakala ya Serikali Mtandao ili kusimamia jitihada za Serikali Mtandao nchini.

Dhana hii ya Serikali Mtandao au Serikali Kidijitali kwa muktadha huu ni pale taasisi za umma zinapotumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kurahisisha utendaji kazi, kuongeza tija, ufanisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa umma.

Aidha, Serikali kidijitali ni zaidi ya matumizi ya Tehama au mifumo ya kielektroni kwa kuwa inahusisha mageuzi ya kiutendaji na ni nyenzo wezeshi katika kuboresha utendaji kazi na utoaji wa huduma kwa umma.

Hivyo, matumizi ya Tehama hususani utengenezaji wa  Mifumo na usakinishaji wa miundombinu inayoendana na mahitaji yetu na kuendeshwa na wataalam wa ndani ya nchi inasaidia kuboresha utendaji kazi na matokeo yake ni huduma kupatikana kwa urahisi, haraka, kwa gharama nafuu, wakati wowote na mahali popote.

Akieleza katika hatuba yake ya Miaka 60 ya Uhuru, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb), alitanabaisha kuwa hapo awali utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao kwa taasisi za umma ulikuwa wa namna tofauti na hakukuwa na sheria, kanuni, taratibu, viwango na miongozo inayoziongoza kwa ufasaha.

Mhe. Mchengerwa anasema kuwa, mwaka 2019 Serikali ilianzisha Mamlaka ya Serikali Mtandao (e-GA) kwa lengo kudhibiti utekelezaji wa jitihada za serikali mtandao kwa taasisi za umma, hivyo anaelekeza taasisi za umma zote nchini kutotengeneza mifumo au kusakinisha miundombinu ya Tehama bila kuwasiliana au kuihusisha Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa ushauri na msaada wa kiufundi.

Vilevile, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Mohamed Mchengerwa (Mb) anaongeza kuwa Serikali ya Tanzania inakwenda kuwa Serikali ya kidijitali, hivyo sharti  isimamiwe kwa ufasaha ili kuwa na jitihada za pamoja na endelevu.

“Ninaziagiza taasisi zote za umma kuhakikisha kuwa zinaihusisha e-GA wakati wa kuanzisha miradi, kutengeneza mifumo na kusakinisha miundombinu ya Tehama Serikalini. Hii itaisadia e-GA kujiridhisha kuwa Sheria, kanuni, taratibu, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao vinazingatiwa” alisema Mhe. Mchengerwa.

Akielezea historia ya kuundwa kwa taasisi ya kuratibu utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. Dkt. Laurean Ndumbaro alitanabaisha kuwa, Mwezi Aprili 2012, Serikali ilianzisha Wakala ya Serikali Mtandao kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 Sura ya 245 ya mwaka 1997 iliyokuwa na jukumu la kuratibu na kusimamia utekelezaji wa Serikali Mtandao kwa taasisi za umma lakini baada ya takribani miaka saba (7) ya utendaji kazi, Serikali ilibaini kuwa kuna umuhimu wa kuiongezea Wakala hiyo uwezo wa kisheria wa kudhibiti utekelezaji holela wa jitihada za serikali mtandao.

Hivyo, mwaka 2019 kupitia Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019, Serikali ikaanzisha Mamlaka ya Serikali ya Mtandao (e-GA) yenye nguvu ya kisheria ya kudhibiti utekelezaji wa serikali mtandao kwa taasisi za umma na kuipa jukumu la kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza uzingatiaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao katika taasisi za umma.

Aidha, Mhe. Dkt. Ndumbaro akatanabaisha zaidi kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao iliyoanzishwa, ilirithi na kuendeleza shughuli za iliyokuwa Wakala ya Serikali Mtandao kwa lengo la kurahisisha utendaji kazi Serikalini, kuongeza tija na ufanisi, kuboresha upatikanaji wa taarifa na utoaji wa huduma kwa umma.

Ameongeza kuwa sekta ya Tehama Serikalini haiwezi kujiendesha bila kuzingatia sheria taratibu, kanuni, miongozo na viwango, Serikali ya Tanzania imeweka mfumo wake madhubuti wa kudhibiti matumizi ya teknolojia hiyo kwa taasisi za umma ili kutoa huduma kwa wananchi wakati wowote, kwa urahisi na kwa gharama nafuu.

Naye, Mkurugenzi Mkuu wa eGA Mha. Benedict Benny Ndomba anasema kuanzishwa kwa Mamlaka ya Serikali Mtandao mwaka 2019 kunaendeleza afua za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na kuchukua sehemu ya mipango yake kwa sababu majukumu ya taasisi hizi yanafanana ingawa yanatofautiana katika mamlaka ya utendaji.

Aidha, Mha. Ndomba anaongeza kuwa taasisi za umma na wananchi kwa jumla watambue kuwa Mamlaka imejizatiti kutoa huduma bora za Tehama kama ilivyoelekezwa kwenye Sheria. Kwa mantiki hiyo, anatoa wito kwa wadau wote wa Tehama wa ndani na nje ya Serikali kuhakikisha kunakuwa na jitihada za pamoja katika kuendeleza Serikali Mtandao nchini ili kuleta tija inayotarajiwa kwa manufaa ya umma.

“Ili Serikali Kidijitali itokee na mwananchi aone anapata huduma za serikali kidijitali, inatakiwa kila taasisi inayohusika kutoa huduma kwa umma iwe inatumia Tehama katika utoaji wa huduma zake. Pia, mifumo ya taasisi za umma sharti iwe na uwezo wa kuwasiliana na kubadilishana taarifa ili kuondoa usumbufu kwa wananchi”. Anasema Mha. Ndomba.

Mha. Ndomba anaendelea kusema kuwa, tangu kuanzishwa kwa e-GA falsafa yake imekuwa ni kujenga uwezo wa wataalam wa ndani ya nchi katika kutekeleza jitihada za Serikali Mtandao, Hivyo imekuwa ikitumia wataalamu wa ndani ya nchi katika usanifu, ujenzi na uendeshaji wa mifumo na  miundombinu ya Tehama kwa kiasi kikibwa na  wakandarasi pale inapobidi.

Mha. Benedict Benny Ndomba anaendelea kusema kuwa, Mamlaka ya Serikali Mtandao kwa kushirikiana na taasisi za umma imebuni, kusanifu na kutengeneza mifumo mbalimbali katika kipindi cha utendaji kazi wake.

Baadhi ya mifumo hiyo ni: Mfumo wa Ajira (Recruitment Portal) unaosaidia kuharakisha mchakato wa ajira Serikalini na waombaji kuomba ajira kimtandao, Mfumo wa Kielektroni Ukusanyaji Mapato Serikalini (Government e-Payment Gateway - GePG) unaowawezesha wananchi kulipia kodi na tozo mbalimbali za Serikali, Mfumo wa Ofisi Mtandao (Government e-Office System), Tovuti Kuu ya Serikali (Government Portal), Mfumo wa Ukataji Tiketi kwa njia Mtandao TRC na Kampuni ya Huduma za Meli za Taifa (MSCL)  na Mfumo wa huduma kwa simu za Mkononi - Government Mobile Services unaowezesha taasisi za umma kutoa huduma kwa njia ya simu za mkononi kupitia namba maalum ya  *152*00# (USSD) na 15200 kwa ujumbe mfupi wa maandishi.

Mifumo mingine ni mfumo wa Barua Pepe Serikalini (Government Mailing System - GMS), Mfumo Shirikishi wa Kusimamia Shughuli na Rasilimali za Taasisi (Enterprise Resource Management Suite - ERMS), Tovuti ya Huduma za Tehama Serikalini - (Government ICT Service Portal - GISP), Mfumo wa Usimamizi wa Mafunzo na Semina (Training and Seminars Management System - TSMS), Mfumo wa Watumishi wa Umma kuomba vibali vya kusafiri nje ya nchi (e-Vibali), Mfumo wa Huduma kwa Wateja (Helpdesk System) na Tovuti za Taasisi mbalimbali za Serikali.

Aidha, Mamlaka imefanya uendelezaji na usimamizi wa miundombinu shirikishi ya Tehama inayowezesha mifumo ya Taasisi za Umma kufanya kazi na kuwafikia wananchi.

Kwa upande wake, Meneja wa Huduma za Sheria wa Mamlaka ya Serikali Mtandao, Kamishna Msaidizi wa Jeshi la Polisi na ACP. Raphael Rutaihwa ameufafanua kuwa e-GA inaratibu na kudhibiti jitihada za Serikali Mtandao kwa kutengeneza kanuni, taratibu, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao (e-Government Standards and Guideline), kufanya ukaguzi wa viwango, ubora na usalama wa mifumo pamoja na kuthibitisha miradi ya Tehama.

“Tunatoa mafunzo na kufanya vipindi vya kuelimisha umma kwa njia ya Radio, Televisheni, Mitandao ya kijamii, warsha na makongamano kwa taasisi za umma ili kuziongezea uwezo wa kutekeleza jitihada za serikali mtandao” Amebainisha ACP. Rutaihwa.

Sambamba na hilo, amesema kuwa taasisi za umma zimeanzishwa kwa malengo tofauti, lakini Tehama ni nyenzo inayoziwezesha taasisi hizo kufanya kazi kwa urahisi na kutoa huduma kwa wananchi kwa gharama nafuu, hivyo ni jukumu la msingi la e-GA kutoa ushauri wa kitaalamu na msaada wa kiufundi ili kupata thamani halisi ya uwekezaji wa Tehama serikalini.

Aidha, ACP. Rutaihwa amesema kuwapo kwa Sheria, kanuni, taratibu, viwango na miongozo ya serikali mtandao kunaifanya sasa serikali kuwa na mifumo inayowasiliana na yenye uwezo wa kubadilishana taarifa. Ametoa mfano wa namna ya kupata pasi za kusafiria kuwa kwa sasa inaombwa na kutolewa kidijitali kwa mifumo kuwasiliana.

“Ninaziomba taasisi za umma kuzingatia  sheria, kanuni, taratibu, viwango na miongozo ya Serikali Mtandao katika kusanifu miundombinu ya serikali kwa maana ya majengo, barabara na reli lazima iwe na utayari wa kuweka mifumo na miundombinu ya Tehama ili kuepuka ubomoaji ili kuunganisha mifumo ya Tehama”. ACP. Rutaihwa

Naye, Meneja Usimamizi wa Viwango vya Serikali Mtandao Bi. Sultana Seif anasema Serikali kupitia Mamlaka ya Serikali Mtandao, imeandaa viwango na miongozo mbalimbali inayotoa maelekezo na ufafanuzi wa taratibu zinazotakiwa kuzingatiwa ili kuwa na matumizi sahihi na salama ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika hatua za kupanga, kubuni, kupata, kununua, kusimamia na kuendesha mifumo mbalimbali ya Tehama Serikalini.