Tanzania na Japan: Balozi wa Japan aangazia urafiki na ushirikiano wa muda mrefu

Kutoka kushoto, Balozi Yasushi Misawa, Balozi wa Japan nchini Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa kwenye sherehe ya kidiplomasia ya Sherry ya mwaka huu.

Siku ya kitaifa ya Japan na Mfalme wa Japan

Wajapani husherehekea siku ya kuzaliwa ya mfalme aliyeko madarakani kama siku ya kitaifa. Mfalme wa sasa wa 126, Mtukufu Mfalme Naruhito, alizaliwa mwaka 1960, na anatimiza miaka 64 leo, tarehe 23 mwezi Februari.

Wakati tukisherehekea siku ya kuzaliwa ya Mfalme, hebu tufanye tafakuri ya urafiki kati ya Japan na Tanzania ambao umeendelea kuimarika kwa miongo kadhaa, pamoja na mustakabali wetu.


Japan na Tanzania

Kuna umbali wa takribani kilometa 12,000 kati ya Tanzania na Japan. Hata hivyo, nchi hizi zimeunganishwa na bahari ya IndoPacific. Kuna kumbukumbu za Mwafrika aliyefika Japan kutoka pwani ya mashariki mwa Afrika kupitia India, na kufanya kazi kama “Samurai” yaani msaidizi wa Mpiganaji aliyekaribia kuiunganisha Japan katika karne ya 16.

Hata hivyo, mawasiliano kati ya Tanzania na Japan yaliimarika wakati Tanganyika ilipopata uhuru mwaka 1961. Japan ilianzisha uhusiano wa kidiplomasia na Tanganyika mara baada ya kupata uhuru wake. Tangu mwaka 1962, Serikali ya Japan imetekeleza programu za maendeleo katika maeneo mbalimbali.

Pamoja na ujenzi wa daraja la Selander miaka ya 1980, barabara kuu nyingi za Dar es Salaam na miundombinu imejengwa kwa msaada wa Japan.

Miaka ya hivi karibuni, JICA imetoa msaada katika ujenzi wa barabara ya juu ya kwanza Tanzania, barabara ya juu ya Mfugale iliyoko njiapanda ya Tazara, Barabara mpya ya Bagamoyo na daraja la Gerezani.

JICA pia imetoa msaada katika ujenzi wa mkondo wa umeme wa Iringa-Shinyanga, mradi wa kuunganisha umeme kati ya Kenya na Tanzania, na programu za kujenga uwezo za TANESCO, pamoja na miradi mingine mingi.

Hali kadhalika, kampuni za Sumitomo na Toshiba Plant zilishirikiana na TANESCO kujenga kituo cha kuzalisha umeme cha Kinyerezi II, kituo cha kuzalisha umeme wa gesi chenye uwezo wa kuzalisha megawati 240, misaada ambayo inachangia kuimarisha usambazaji wa umeme.

Eneo jingine ambalo JICA imejihusisha nalo kimahususi ni kilimo, hasa kilimo cha mpunga. Tangu wakati wa mradi wa maendeleo ya kilimo Kilimanjaro (Kilimanjaro Agricultural Development Center Project) miaka ya 1970, JICA imeendelea kutoa msaada katika kilimo cha mpunga Tanzania kupitia miradi mbalimbali nchi nzima.

JICA pia inatoa misaada kwenye miradi mingine kama vile kukuza uwezo wa kiutawala katika serikali za mitaa, kuongeza uzalishaji katika biashara ndogo na za kati, kuwaunga mkono wanamichezo na wajasiriamali wa kike, na kuwasaidia wanafunzi wenye umri mdogo kuanzisha biashara zao binafsi.

Leo, tunafurahi kuona Tanzania inachangia katika usalama wa chakula barani Afrika kama muuzaji wa mchele nje ya nchi na uchumi wake ukiendelea kuelekea uchumi wa kipato cha kati.

Hata hivyo, ukuaji wa maendeleo wa Tanzania ni mkubwa, na ikiwa vijana wa Tanzania wana utashi wa dhati na wakaendelea kufanya kazi bila kuchoka, tunaweza kutarajia mustakabali mzuri zaidi. Japan itaendelea kushirikiana na Tanzania na inakusudia kuwa bega kwa bega na Tanzania katika maendeleo.


Urafiki wa Tanzania na Japan na ushirikiano katika ngazi ya kimataifa

Ingawa Japan na Tanzania zimeendelea kuwa na uhusiano mzuri, migogoro mikubwa inaendelea kutokea ulimwenguni.

Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, vitendo vya ugaidi, na mgogoro wa kibinadamu katika ukanda wa gaza ni mifano michache. Barani Asia, kuna hali ya wasiwasi kuhusu mpango wa Korea Kaskazini wa kutengene¬za silaha za nyuklia, majaribio ya makombora na vitendo vingine vya kinyama vinavyokinzana na maazi¬mio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Katika ukanda wa Mashariki na Kusini mwa bahari ya China, tunashuhudia mifano ya majaribio ya kutaka kubadili utaratibu uliozoeleka kwa kutumia nguvu na vitisho.

Wakati jamii ya kimataifa inakabil¬iana na changamoto za kiusalama, Japan inaamini kwamba kuanzisha utaratibu huru na wazi unaozingatia utawala wa sheria ni hatua muhimu sana katika kuleta amani na mafani¬kio katika ukanda husika na maeneo mengine.

Kwa kuzingatia mlengo huu, Waziri Mkuu wa zamani Shinzo Abe alizindua maono yake ya “Indo-Pacific huru na wazi” kwenye mkutano wa sita wa kimataifa wa Tokyo unaohusu Maendeleo ya Afrika (TICAD6) ulio¬fanyika nchini Kenya mwaka 2016.

Kupitia mkutano huo, Japan inalenga kutoa taarifa kwa mataifa mengine kuhusiana na sheria za kimataifa za bahari, kutangaza uta-ratibu wa kutengeneza sheria za uchumi huru na wa haki, kuungani-sha nchi kupitia misaada ya maende leo, kusaidia kukuza biashara na uwekezaji, kuimarisha utawala, na kuhakikisha usalama majini, mambo ambayo yatachangia katika kuimari¬sha amani na maendeleo ya kiuchumi katika ukanda wa Indo-Pacific, ikiwa ni Pamoja na Afrika.

Kuelekea mkutano wa tisa wa kima¬taifa wa Tokyo juu ya Maendeleo ya Afrika (TICAD9) na Maonyesho ya Kimataifa ya Osaka-Kansai ya 2025

Mwaka kesho, mkutano wa tisa wa kimataifa wa Tokyo juu ya Maende¬leo ya Afrika (TICAD9) utafanyika Yokohama, Japan. Nikiwa Balozi wa Japan nchini Tanzania, natumaini kwamba Afrika pamoja na Tanzania, na Japan zinaweza kubadilishana mawazo na kuimarisha ushirikiano kuelekea mkutano huo.

Maonyesho ya Osaka-Kansai ya 2025 pia yatafanyika mwaka kesho. Ushiriki wa kwanza wa Tanzania katika maonyesho ulikuwa mwaka 1970 katika maonyesho ya Osaka.

Tukio hili liliibua shauku yangu katika masuala ya mataifa ya kigeni kwa mara ya kwanza nikiwa na umri wa miaka 7. Miaka 55 imepita tangu kipindi hicho. Kama Balozi wa Japan nchini Tanzania kutokea Kansai, nafurahi kwamba Tanzania itashiriki tena kwenye maonyesho ya Osaka.


Karibu Osaka kwa mara nyingine tena!

Nchini Japan, mwaka 2024 unaitwa “Reiwa 6’’. Hii ni kwa sababu ni mwaka wa sita tangu Mfalme wa sasa aingie madarakani. “Reiwa” maana yake ni “maelewano mazuri”, na neno hili linatokana na shairi la zamani sana la kijapani, la karne ya nane.

Ni matumaini yangu kwamba Japan na Tanzania zitaimarisha ushirikiano wetu, kuelekea TICAD9 na maonyesho ya kimataifa ya 2025, yanayotangaza “maelewano mazuri” si tu katika eneo la Indo-Pacific bali ulimwenguni kote.


Kutoka kushoto, Balozi Yasushi Misawa, Balozi wa Japan nchini Tanzania, na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwa kwenye sherehe ya kidiplomasia ya Sherry ya mwaka huu.