Bei ya ndizi yapaa Zanzibar

Mkazi wa Zanzibar, Nafunda Faki akitazama ndizi aina ya Mkono wa Tembo katika Soko la Mwanakwerekwe, Mjini Unguja. Mkungu wa ndizi hiyo unauzwa kati ya Sh60,000 hadi Sh80,000. Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

 Licha ya kuwapo ndizi za aina tofauti kutoka Tanzania Bara, wengi bado wanatumia walizozoea

Unguja. Licha ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kuondoa zuio la uingiaji wa ndizi kutoka Tanzania Bara bei ya zao hilo bado ipo juu visiwani hapa.

Mwananchi Digital leo Machi 25, 2024 imeshuhudia minada ya ndizi katika masoko tofauti kukukiwa hakuna tofauti kati ya awali na sasa licha ya Serikali kufungua milango ya kuingia bidhaa hiyo.

Zuio la ndizi, miche na majani ya migomba kutoka Tanzania Bara liliwekwa na SMZ mwaka 2007 kwa madai ya kushambuliwa na maradhi.

Machi 14, 2024 baada ya miaka 17 Serikali kupitia Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji na Maliasili, Shamata Shaame alitangaza kuondolewa kwa zuio hilo, akisisitiza uwepo wa tahadhari.

Hata hivyo, katika mnada kwenye Soko la Jumbi, Wilaya ya Kati Unguja, ndizi aina ya Mtwike mkungu unauzwa kati ya Sh40,000 hadi Sh50,000 kulingana na ukubwa wake.

Aina hii ya ndizi kabla ya kuanza mfungo wa mwezi Mtukufu wa Ramadhan na kuondolewa zuio la Serikali iliuzwa kati ya Sh25,000 na Sh30,000.

Katika Soko la Kibandamaiti, ndizi aina ya Mkono wa Tembo inayotumika zaidi wakati wa mfungo wa Ramadhan inauzwa kati ya Sh60,000 na Sh80,000.

Ndizi moja ya aina hiyo inauzwa Sh3,000 hadi Sh4,000, tofauti na awali ilipouzwa kati ya Sh1,500 na Sh2,000.

Baadhi ya wanunuzi wa bidhaa hiyo wamesema licha ya bei kuwa juu, wanalazimika kununua kutokana na mahitaji yaliyopo.

Ali Kheri, mfanyabiashara eneo la Mpendae, Unguja amesema hana sababu itakayomzuia kununua ndizi kutokana na mahitaji ya bidhaa hiyo wakati huu wa mfungo.

"Pamoja na Serikali kuruhusu uingiaji wa ndizi kutoka Tanzania Bara lakini bei haishikiki, inawezekana  zinazoletwa si ambazo watu wanazihitaji na pengine hawajazizoea kabisa," amesema Kheri.

Amesema chana moja inauzwa kati ya Sh5,000 na Sh6,000 kwa bei ya jumla na wao wanauza hadi Sh8,000.

Mize Silima, mfanyabiashara mkazi wa Tomondo, Unguja amesema kuna haja ya jamii kujengewa uelewa juu ya matumizi ya ndizi kutoka Tanzania Bara.

Amesema alichokiona  huenda watu hawazijui na hawajazizoea ndiyo maana bei ya bidhaa hiyo haishuki licha ya kuwapo kwa wingi.

"Nina wasiwasi maana ndizi za Mzuzu na Bukoba sasa zinapitishwa hadi mitaani lakini watu wanaonunua ni wachache, sote tunakuja kuzongana huku sokoni," amesema.

Nassor Salim, mkulima na mfanyabiashara kutoka Kisiwa cha Pemba, amesema ongezeko la bei kunatokana na kuongezeka kwa mahitaji kipindi cha Ramadhan.

Amesema wakulima wengi wanaitazama sikukuu ya Eid, hivyo wamekuwa wakiuza bidhaa hizo kwa malengo maalumu.

"Kila mmoja anatazama mwanaye atavaa nguo gani mpya sikukuu, anajua fika kila ndizi moja anaweza kutoa nguo moja ya mtoto wake na ndiyo sababu bei huanza kubadilika kwa mkulima kabla ya kuja sokoni," amesema.

Hata hivyo, amesema kuna haja ya uwepo wa mkakati maalumu utakaowasaidia wakulima kuona kilimo cha ndizi ni muhimu na chenye kuhitajika ili kuondoa mazoea ya watu kulima kama sehemu tu ya bustani za nyumbani.