‘Ya Wizi’ mbinu inayotumika kulinda ndizi Zanzibar

Miongoni mwa ndizi zilizoandikwa (Ya wizi) ikiwa shambani kwa lengo la kukingwa na wizi ambao umeshamiri katika kipindi hiki cha mfungo wa Ramadhan.Picha na Muhammed Khamis

Muktasari:

  • Wananchi watakiwa kutoa taarifa wahalifu washughulikiwe kisheria.

Unguja. Kutokana na kukithiri wizi wa mazao katika kipindi cha mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan, baadhi ya wananchi Zanzibar wamebuni mbinu ya kukabiliana na hali hiyo.

Wizi huo umekithiri kwa bidhaa zinazotumika kwa futari ambazo ni pamoja na ndizi na mihogo.

Baadhi ya wakulima wameandika neno ‘Ya Wizi’ kwenye mikungu ya ndizi  wakisema kufanya hivyo kunaweza kupunguza uhalifu huo.

Ali Abdalla, mkazi wa Maungani, Unguja amesema tangu aanze kufanya hivyo kuna unafuu amepata wa mazao yake kutoibwa.

"Nafikiri wezi huiba na kwenda kuuza, haya maandishi yamekuwa yakiwarudisha nyuma, na inaonekana wanunuzi huzikataa wanapoona maandishi haya," amesema.

Mayasa Juma Ameir, anayeishi Fuoni, amesema katika kipindi cha Ramadhan ameshaibwa mikungu mitano ya ndizi shambani kwake.

Amesema wezi huenda usiku kukata ndizi bila kujali nguvu zilizotumiwa na wakulima katika kilimo.

"Ndizi zangu nne (mikungu) niliweka kwa ajili ya kuziuza nina hakika zilivyokuwa kubwa ningepata fedha za kuongezea kununua nguo za wanangu sikukuu ya Eid lakini wapi wameniacha na kilio," amesema.

Naibu sheha wa Shehia ya Kisauni, Unguja, Haji Juma amesema wanaofanya hivyo wanapaswa kuchukuliwa hatua.

Amewataka wananchi kutoa taarifa katika vyombo husika pale wanapobaini makundi ya vijana wanaojihusisha na matendo maovu yakiwamo ya wizi.