Dk Mwinyi awatunuku nishani Rais Samia, Maalim Seif

Muktasari:

 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewatunuku nishani viongozi 17 wakiwemo Rais Samia Suluhu Hassan na Hayati Maalim Seif Sharif Hamad ikiwa ni maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar yaliyofanyika Januari 12, 1964

Unguja. Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amewatunuku nishani viongozi 17 akiwamo Rais Samia Suluhu Hassan na Hayati Maalim Seif Sharif Hamad ambaye ametunukiwa nishani ya Mapinduzi ya viongozi wenye sifa ya kipekee.

Viongozi wengine waliotunukiwa nishani hizo ni pamoja na Dk Mohammed Gharib Bilali (Makamu wa Rais mstaafu), Shamsi Vuai Nahodha, Balozi Seif Ali Iddi (makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar), ambao wametunukiwa nishani ya Mapinduzi ya viongozi na wananchi wenye sifa maalumu.
Hafla ya kuwatunuku nishani viongozi hao imefanyika leo Alhamisi, Januari 11, 2024 katika viwanja vya Ikulu Mjini Unguja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Akisoma wasifu wa Rais Samia, Meja Martin Alfon Mabena kutoka Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) amesema, Rais Samia ni kiongozi wa kwanza mwanamke kushika nafasi ya juu ya uongozi wa nchi ambaye alishika nafasi ya Makamu wa Rais kabla ya kuwa Rais Machi 19, 2021.

Amesema ni kiongozi wa mfano aliyefanya kazi kuanzia ngazi ya chini ya mtunza kumbukumbu (masjala) na kuongoza wizara tofauti ikiwemo ya utalii, biashara na uwekezaji katika serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Pia, alikuwa Waziri katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano.


Amesema, alivyokuwa Waziri wa Utalii katika Serikali ya Mapinduzi wa Zanzibar aliweza kujenga misingi imara ya kukuza biashara ya utalii na awali uchumi wa Zanzibar ulikuwa ukitegemea zao la karafuu lakini lilishindwa kufanya vizuri.

 “Rais Samia ni kiongozi wa mfano ambaye anaendelea kudumisha Muungano wa Tanganyika na Zanzibar bila ya kutetereka,” amesema 

 

Maalim Seif 

 Hayati Maalim Seif Sharif Hamad ametunukiwa nishani ya Mapinduzi ya viongozi wenye sifa maalumu. 
Akisoma wasifu wake, Meja Mabena amesema, Maalim Seif alikuwa ni kiongozi aliyehudumu katika nafasi ya Waziri Kiongozi kuanzia Februali 1984 hadi Januari 1988, ofisi yake ndiyo ilikuwa yenye dhamana ya kusimamia shughuli zote za Serikali.

Amesema, Hayati Maalim Seif alikuwa Mwanzilishi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) na kiongozi wa kwanza aliyehudumu nafasi ya Makamu wa kwanza wa Rais baada ya SUK ya kwanza kuingia madarakani mwaka 2010 hadi mwaka 2015 akiwa CUF.

 Kisha alihudumia wadhifa huo wa Makamu wa kwanza wa Rais kwa tiketi ya Chama cha ACT Wazalendo kuanzia mwaka 2020 hadi Februari 17, 2021 umauti yalipomfika.

Amesema, Maalim Seif alikuwa ni kiongozi aliyejitolea kutumikia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, katika maisha yake alidumisha umoja, amani na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.


Wengine waliotunikiwa 

Pia, Dk Mwinyi amewatunuku nishani ya utumishi wa muda mrefu na utii kwa idara maalum za SMZ, ambao ni Mohammed Suleiman Haji, Maryam Kurwa Nassor, Seif Omar Makwega na Khadija Ahmada Rai.
Waliotunukiwa nishani ya ushujaa ni Marehemu Ramadhan Khalfan Ngozoma, Ikrab Mikidadi Hassan, Marehemu Khalid Abass Hassan na Dk Suleiman Maulid Mussa aliyemsaidia mzazi katika boti ya Kilimanjaro V.

Katika hafla hiyo viongozi mbalimbali walihudhuria wakiwemo marais wastaafu Jakaya Kikwete, Dk Amani Abeid Karume na viingozi wakuu wa Serikali za Jamhuri na ya Zanzibar.