Mali za Sh15 bilioni za watuhumiwa dawa za kulevya kutaifishwa Z’bar

Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Burhani Zuberi akitoa tamko la kutaifishwa mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya leo Unguja. Picha na Jesse Mikofu

Muktasari:

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka hiyo kufanya operesheni maalumu Janauri mwaka huu na kufanikiwa kukamata zaidi ya kilo 100 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, hashi na bangi

Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCE), imetangaza kutaifisha mali za watuhumiwa wa dawa za kulevya zenye thamani ya Sh15.3 bilioni kuwa mali ya Serikali.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya mamlaka hiyo kufanya operesheni maalumu Janauri mwaka huu na kufanikiwa kukamata zaidi ya kilo 100 za dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, hashi na bangi.

Akizungumza kuhusu kutaifishwa kwa mali hizo ofisini kwake leo Jumatatu  Aprili 22, 2024 , Kamishna Mkuu Burhani Zuberi Nassoro amesema dawa hizo ziliingizwa nchini na wafanyabiashara wakubwa wa dawa za kulevya.

 Kamishna Nassoro amewataja watuhumiwa hao kuwa ni Salehe Khamis Basleman na Gawar Bachi Fakir wote wakazi wa Chukwani, Wilaya ya Magharibi B Mkoa wa Mjini Magharibi.

Watuhumiwa hao wamebainika kufanya biashara haramu ya dawa za kulevya Zanzibar, Tanzania Bara, Afrika, Asia, Ulaya na Marekani.

Hata hivyo iwapo kuna mtu hajaridhika na tamko hilo anaweza kwenda mahakamani ndani ya siku 30 kuanzia leo.

“Kupitia biashara hiyo wamejipatia kiasi kikubwa cha fedha wanazozitumia kwa njia ya utakatishaji wa fedha haramu kwa kununua magari ya kifahari, nyumba viwanja na kuanzisha biashara hewa,” amedai Kamishna Nassoro.

Amesema anataifisha mali hizo kwa uwezo aliopewa chini ya kifungu cha 73 (1) cha Sheria namba 8 ya 2021 ya Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibarna baada ya kuzingatiwa matakwa ya kifungu cha 71 cha sheria hiyo.

Kamishna Nassoro  amedai kuwa,  kabla ya kufikia hatua hiyo mamlaka kupitia matangazo mbalimbali kwenye gazeti la Serikali na maeneo ya watuhumiwa, waliitwa ili waonyeshe vyanzo vya mapato au mali namna zilizotumika kuzipata lakini hawakuripoti ndani ya siku 30 zilizowekwa kwa mujibu wa sheria.

Amezitaja mali hizo ni magari sita yenye thamani ya Sh399 milioni, vyombo vya usafiri vya majini vya Sh29.9 milioni na viwanja vya makazi na biasara vinane vyenye thamani ya Sh6.8 bilioni.

Zingine ni nyumba za kifahari tatu zenye thamani ya Sh6.3 bilioni na nyumba za makazi na biashara nane zenye za Sh1.7 bilioni huku mali zote zikiwa maeneo tofauti ya mikoa ya Unguja.

Amesema kiasi hicho cha fedha ni kikubwa kinachoweza kuendesha takriban wizara mbili katika Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ).

“Tunazungumza haya ili wananchi wa Zanzibar waelewe kuwa kuna watu wamejilimbikizia utajiri uliopatikana kwa njia haramu ya kuuza dawa za kulevya na kuumiza vijana wetu.”

Baadhi ya wakazi wa mjini Unguja licha kupongeza hatua zinazochukuliwa na mamlaka hiyo, wametaka kuwakamata wanaohusika ili kudhibiti mtandao.

“Kama watu hawa hawajakamatwa, wanaweza kuendeleza biashara hizo kwa mbinu nyingine maana ninachokiamini hawawezi kuwa pekee yao kuna watu wanashirikiana nao,” amedai Ayoub Hamad.

 “Tunajua waraibu wa dawa za kulevya wanavyohangaika mitaani kuiba, kunyang’anya au kufanya kazi za ajabu ili waweze kupata fedha za kununua dawa za kulevya, kwahiyo mbinu zinatakiwa kuongezwa.”