Othman: Mageuzi ya kiutendaji yanaanza na mabadiliko ya nafsi

Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Zanzibar, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Othman Masoud akizungumza na viongozi wapya wa Chama hicho Mkoa wa Kaskazini Pemba

Muktasari:

  • Makamu Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Zanzibar, Othman Masoud OthmAmewataka kuzingatia misingi ya uadilifu, haki, kuvumiliana, umoja na ushirikiano mbele ya wananchi wote.

Pemba. Wakati chama cha ACT-Wazalendo kikijipambanua kuwa taasisi ya inayosimamia harakati za kuleta mageuzi ya kisiasa hatimaye kushika dola, Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Zanzibar, Othman Masoud amesema ni lazima kila kiongozi kuanza na mabadiliko ya nafsi yake na kutenda haki.

Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo Septemba 16, 2023 katika mkutano maalumu wa viongozi wapya wa chama hicho, kutoka Mikoa ya Wete na Micheweni kichama, Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Amewataka kuzingatia misingi ya uadilifu, haki, kuvumiliana, umoja na ushirikiano mbele ya wananchi wote.

“Mageuzi ya kweli yanayojali maisha ya wananchi, hayatofikiwa kwa kuendelea kuighiliba sehemu hiyo muhimu ya jamii, kwa seti ya jezi za mpira,” amesema.

Amesema, kushindwa kuelewa kwa viongozi na watu waliopewa nafasi mbalimbali, kwamba mamlaka ni dhamana, ndiko kunakoendelea kufanya hali duni na kudhoofika kwa hali ya maisha ndani ya Zanzibar na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ujumla.

Akifafanua hilo, Othman alisema: “Ieleweke kwamba haya siyo ya kisiasa bali ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya watu ndani ya nchi hii yanakoelekea hayaleti matumaini kutokana na ukosefu wa kujipanga, kushindwa kuzingatia haki na uadilifu huku kukikosekana kujali dhamana na maadili ya uongozi,”

Othmani amesema kazi ya kuwapata viongozi hao wapya hivyo ili kuepuka kurudi nyuma katika kuendeleza siasa ni vyema kwa wote waliojitokeza kugombea waamini juu ya hali ya matokeo katika ushindani wowote, chini ya kaulimbiu isemayo, “tuchague mmoja tubaki wamoja”.

Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Salim Bimani, amewakubusha viongozi wapya kutambua kwamba misingi ya chama hicho siyo kupata nafasi za ubunge, uwakilishi wala udiwani, bali muhimu ni kuzingatia umoja na utumishi wa haki, kwa Wazanzibari wote.

Katibu wa Chaguzi wa ACT-Wazalendo, Muhene Said Rashid amesema kazi ya kuwapata viongozi wa ngazi zote wa chama hicho, kuanzia matawi yote 678 na majimbo 50 ya Unguja na Pemba imefikia asilimia 93.8.

Katika chaguzi hizo pia tayari kura za maoni za kumpata mgombea atakayepeprusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mdogo wa uwakilishi wa Mtambwe ambapo jina lake litapelekwa halmashauri kuu ya chama hicho ili kumpitisha rasmi.

Uchaguzi wa jimbo hilo unatarajiwa kufanyika Oktoba 28, kutokana na kifo cha aliyekuwa mwakilishi wa jimbo hilo, Habib Ali Mohamed kilichotokea mapema mwaka huu.