Polisi yatoa tahadhari kipindi sikukuu ya Eid el Fitri

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Abubakar Khamis Ally akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Madema leoJumatatu Aprili 8, 2024

Muktasari:


  • Wakazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wa Sikukuu ya Eid el Fitri ili kuepuka vitendo vya uvunjifu wa amani.

Unguja. Wakazi wa Mkoa wa Mjini Magharibi,wametakiwa kuchukua tahadhari wakati wa Sikukuu wa Eid el Fitri inayotarajiwa kuwa kati ya Aprili 10 au 11, huku wakionywa siku hiyo siiwe sababu ya kufanya vitendo vya uvunjifu wa Amani.

 Tahadhari hiyo imetolewa leo Jumatatu Aprili 8, 2024 na Kaimu Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Abubakar Khamis Ally alipozungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Madema.

Amesema wapo baadhi ya watu hutumia siku za sikukuu kama chanzo cha kujipatia kipato kwa njia isiyo halali, hivyo akasema jeshi hilo limejipanga kuwachukulia hatua kwa watakaojihusisha na vitendo hivyo.

"Jeshi la Mkoa wa Mjini linatoa onyo kwa yeyote atakayejaribu kujihusisha na vitendo vya uvunjifu wa amani na kujipatia kipato kwa njia isiyo halali, tutamkamata na kumchukulia hatua, ili iwe fundisho kwake na wengine wenye tabia hizo," amesema Kaimu Abubakar.

Hata hivyo, amesema jeshi hilo litaimarisha doria na msako, ili kudhibiti madereva wazembe na wasiotii sheria za usalama barabarani.

Pia, amekemea tabia ya baadhi ya  vijana kuendesha vyombo kwa mwendo kasi na kupiga misere (drifting) barabarani, hasa katika barabara za Michenzani, Fumba, Uwanja wa Ndege, Fuoni, Amani na Mwera kuacha tabia hiyo, kwani ni hatari kwa usalama wao.

Kaimu Kamanda huyo amewaomba wananchi wanaotoka majumbani kwenda viwanja vya sikukuu, kuhakikisha hawaondoki wote, ili kuimarisha usalama wa nyumba zao.

"Pia wananchi wanapaswa waepuke kuchelewa kurudi nyumbani kwa sababu baadhi yao wanatumia fursa hiyo kuvunja nyumba na kuiba, hivyo watu lazima kuwa makini kipindi hiki cha sikukuu," amesema Kaimu Kamanda Abubakar.

Kwa upande wake, Yusra Nabil, mkazi wa Michenzani amesema kipindi cha sikukuu kawaida matukio ya uvunjifu wa amani yanatokea kwa wingi, hivyo wananchi wanapaswa kuchukua tahadhari mapema.