Rais Mwinyi ahimiza amani, kuendeleza mema ya mwezi wa Ramadhan

Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi akizungumza kwenye Baraza la Idd lililofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar leo Aprili 10, 2024.

Muktasari:

 Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi ameshiriki Baraza la Idd huku akiwasihi waislamu na wananchi kuendeleza matendo mema

Unguja. Licha ya mwezi mtukufu wa Ramadhan kumalizika, Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi amewataka waislamu na wananchi wote kwa jumla kuendeleza matendo mema yaliyofanywa kipindi cha mwezi huo.

Dk Mwinyi amesema mbali na kujiweka na makatazo ya Mungu, walijitahidi kuswali, kusoma Quran na taasisi zilitoa sadaka kwa wenye uhitaji hivyo lazima mambo hayo yaendelezwe.

Dk Mwinyi ametoa kauli hiyo wakati wa Baraza la Idd lililofanyika Makao Makuu ya Polisi Zanzibar leo Jumatano Aprili 10, 2024 baada ya kumaliza swala ya Idd El-Fitri.

“Katika mwezi mtukufu wa Ramadhan tulijitahidi sana kufanya mambo ya kheri na kujiweka mbali na makatazo ya mola wetu. Mambo haya yaliongeza mapenzi, kuhurumiana, umoja, mshikamano na amani katika nchi yetu.

“Hakika hali tuliyokuwa nayo ya maisha yetu katika mwezi mtukufu wa Ramadhan, ilituongezea uchamungu. Hivyo, namna bora ya kubainisha kufuzu kwetu katika mafunzo tuliyoyapata ni kuyaendeleza mafunzo hayo katika maisha yetu ya kila siku,” amesema Dk Mwinyi.

Amewataka waendelee kufanya mambo ya kheri na kuyaacha mambo yote maovu kwa kuwa Mwenyezi Mungu ameusifia umma katika aya mbalimbali za Quran kuwa ni umma bora wenye kuamrishana mambo mema na kukatazana mabaya.

Amewashukuru wafanyabiashara walioitikia wito wa Serikali wa kutopandisha bei ya bidhaa ili kuwezesha watu wote kumudu kununua bidhaa hasa zile zilizokuwa zikitumika zaidi katika mwezi wa Ramadhan.

“Ni dhahiri kuwa, hali hii iliwapa furaha watu wote hususan wenye uwezo mdogo,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema kuwapo na amani na utulivu nchini kuna umuhimu mkubwa kwa kuwawezesha wananchi kutekeleza ibada zao kwa uhuru na usalama pamoja na kufanya shughuli za maendeleo.

Kwa kuzingatia kuwa kipindi cha sikukuu huwa na harakati nyingi zikiwamo za viwanja vya sikukuu na matumizi makubwa ya usafiri wa barabara, ameliagiza Jeshi la Polisi kuhakikisha linaimarisha usalama wakati wote.

Pia, Dk Mwinyi amewashukuru waumini wa dini nyingine kwa ushirikiano mkubwa walioutoa kwa waislamu katika kipindi chote cha Ramadhan na kutaka ushirikiano huo uendelelee kudumishwa.

“Kwa hakika, hatua hiyo ya ushirikiano ni muhimu na kielelezo cha ustahamilivu na ustaarabu ambao nchi yetu inauendeleza tokea zamani kwa wananchi wetu wenye imani tafauti za dini,” amesema Dk Mwinyi.

“Hali hii inapaswa kuendelezwa kwa kuwa ina mchango mkubwa wa kuifanya nchi yetu kuendelea kudumu katika amani, utulivu na umoja,” amesema

Awali, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Katiba sheria, Utumishi na Utawla Bora, Haroun Suleiman amesema ipo haja kuendeleza utaratibu wa baraza la Idd ambao umekuwapo kwa viongozi waliotangulia.