
| Malezi:Kusali pamoja huimarisha uhusiano kifamilia | Send to a friend |
| Sunday, 29 January 2012 08:51 |
|
Tofauti na zamani ambapo ilikuwa nadra kukuta watu wa familia moja wakijengeana chuki, siku hizi imekuwa kama desturi ya Watanzania wanaotoka familia moja kuchukiana hata kufikia kuharibiana maisha. Hali hiyo ndani ya familia inachochewa na watu kuendekeza fitna, uchonganishi, wivu, uongo. Tabia hizo zinasababishwa na familia nyingi kujengwa bila misingi ya kiroho, ambayo ni chimbuko la maadili mema. Kuna mbinu nyingi ambazo viongozi wa familia zilizotangulia, walizitumia kujenga misingi bora ya kiimani, katika familia zao. Misingi hiyo iliotesha mbegu za upendo na kuchochea ari ya kuwa na uhusiano mzuri wa kindugu na Kimungu. Moja ya mbinu hizo ilikuwa kufanya maombi (sala) pamoja. Familia inapotenga muda maalumu kwa ajili ya kujumuika nyumbani na kusali pamoja, hujijengea mazingira mazuri ya kimahusiano baina yao. Hatua hiyo hutoa fursa kwa wanafamilia kushirikishana masuala binafsi mbalimbali, wanayokabiliana nayo katika maisha ya kila siku, kwa lengo la kuyafanya kuwa miongoni mwa mambo muhimu ya kuyaombea kifamilia. Kushirikishana mambo na kuomba pamoja kwa ajili ya hayo huimarisha kiungo cha umoja kati ya wanafamilia, kwani kiimani maombi husalia na kudumu tu iwapo ni katika mazingira ya kiroho na moyo safi. Kukosa kuomba pamoja si tu kwamba huwatenga mbali na Mungu, bali hali ya umoja wa kindugu na hata upendo miongoni mwa wanafamilia hufifia kadri siku ziendeleavyo na hata kufikia hatua ya ndugu wa familia moja kufanyiana matendo yasiyofaa. Miongoni mwa matendo ambayo katika hali halisi, Watanzania tumekuwa tukiyashuhudia ni pamoja na ndugu wa familia moja kufanyiana hujuma katika nyanja mbalimbali, mathalan kuharibiana kazi, uhusiano wa kimapenzi na kuchafuliana majina. Chuki hizo zimeendelea kuenea na kuota mizizi miongoni mwa Watanzania wengi, ambapo sasa jamii inashuhudia ndugu wakitoana roho, kwa siri au hadharani. Mfano mzuri ni wa tukio lililojiri hivi karibuni, Kibaha mkoani Pwani ambapo ndugu wawili waliuawa na ndugu yao, aliyekuwa askari kisha naye kujiua kwa risasi. Madhara ya kukwepa gharama za kujenga misingi bora na imara ya kuwezesha familia kuwa na uhusiano mzuri, ni makubwa kuliko inavyoweza kufikiriwa. Mbali na kusababishiana hasara, majonzi, magonjwa na hata kuuana, inaleta umaskini kwa mtu mmoja mmoja na jamii kwa ujumla. Ili kufanikisha mpango mmoja wapo wa kujenga umoja wenye msingi wa upendo ndani ya mioyo ya wanafamilia ni kutumia uwezo wote kuweka na kudumisha maisha ya maombi katika familia. Hilo litafanikiwa endapo viongozi wa familia watakuwa na utashi wa kujiweka safi kiroho kwa wenzao na kwa Mungu, ili maombi yao yalete mafanikio kiroho na kimwili. Kufanikisha mpango wa kuchagua muda mwafaka wa kuomba pamoja ni hatua isiyokuwa rahisi, kutokana na ukweli kwamba binadamu hutofautiana katika nyanja mbalimbali kimaumbile, kifikra, kimazingira na namna ya kufanya maamuzi. Pamoja na yote hayo, ni lazima viongozi wa familia waafikiane wakati mwafaka kwa familia yao kuomba pamoja. Kila mmoja kwa nafasi yake, atoe kipaumbele kwa wakati huo walioafikiana uwe wa kufanya maombi pamoja. Hilo likifanikiwa katika kila familia, kwa kuzingatia misingi na maadili ya imani yake, hakika kazi ya kutoa malezi bora kwa familia itarahisishwa, hivyo taifa kuwa na jamii yenye maadili mema. Imeandaliwa na Editha Majura, TSJ 0716 263949 |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














