
| Hoyce Temu: Itungwe sheria kuwaadhibu warembo wanaokiuka maadili | Send to a friend |
| Sunday, 29 January 2012 09:14 |
![]() Na Florence Majani TANGU mashindano ya urembo yapewe baraka mwaka 1994, baada ya kupigwa marufuku miaka ya ‘60 wamekuwapo warembo mbalimbali ambaye kila mmoja, amekuwa na haiba yake na mitazamo mbalimbali katika fani hiyo. Kwa sasa tunahesabu warembo takriban 17 tangu kuanza kwa mashindano hayo. Miongoni mwao ni Hoyce Temu, aliyetwaa taji hilo mwaka 1999. Lakini Hoyce, amekuwa ni mwanamke anayefanya jitihada lukuki za kuhamasisha ukuaji elimu na masuala ya kiuchumi na zaidi, kuwanyanyua wanawake wengine katika sekta mbalimbali. Baada ya kumaliza muda wake kama Mrembo wa Tanzania, hakuketi chini, bali alijiendeleza kielimu, kuanzia ngazi ya shahada na sasa ana shahada ya pili (masters) Hoyce anasema, tofauti kubwa iliyopo kati ya Hoyce wa zamani na wa sasa ni muono. Anasema,sasa hivi ana upeo mpana kwa sababu amepitia changamoto mbalimbali za maisha na pia ana elimu. “Elimu imenisadia kupanua mtazamo wangu, lakini pia, nimepitia mambo mbalimbali katika maisha kwa hiyo nayafahamu na nimejifunza nini maana ya maisha,” anasema. Anasema, anakumbuka maisha yake ya nyuma, kuwa alizaliwa katika familia masikini, ya kula mlo mmoja, shule ya kijijini ya kuandika chini, na kwenda peku, na hilo limemsaidia kuwa ‘mpiganaji’. “Lakini historia hiyo imefutwa kwa sababu nina elimu, ambayo imeniwezesha kuikomboa familia yangu kutoka kwenye umaskini,” anasema. Hoyce ambaye kwa sasa ni Ofisa Uhusiano wa Shirika la Umoja wa Mataifa(UN), anasema wanawake bado wana kazi kubwa kuyafikia maendeleo. “ Maendeleo ya mtu ni mtu mwenyewe. Wanawake wawe na malengo, tuachane na kasumba, tuyakimbie majungu na tukikaa, tuzungumze maendeleo,” anashauri. Anasema, wanawake wasitumie nafasi zao vibaya, kama mwanamke amepewa dhamana yeyote ile, ahakikishe anaifanya kazi yake vyema ili iwe mfano wa kuigwa katika jamii. Hoyce anasema, mwanamke ni mtu mwenye uwezo mkubwa, anafanya kazi nyingi kwa wakati mmoja, kwa mfano malezi, na utafutaji wa kipato hivyo anawashauri kutobaki nyuma. Hoyce hakusita kuzungumzia jinsi tasnia ya urembo ilivyo hapa nchini na kusema baadhi ya warembo wamekuwa wakifanya matendo yanayoidhalilisha tasnia hiyo. “Sitafunga mdomo, nitakemea warembo wanaofanya matendo mabaya katika jamii na kwenda kinyume na maadili ya Mtanzania,” anasema. Anasema, yeye kama mrembo na kama mama mwenye mtoto wa kike anayeitwa Ruby, hafurahishwi na jinsi baadhi ya warembo wanaosikika kwa habari za kugombea wanaume au kulewa kupita kiasi au kuvaa mavazi yasiyo na heshima. “Kama kweli hizi habari tunazozisikia kuhusu warembo wetu ni kweli, kwa kweli zinanisikitisha sana, na ninazikemea kwa nguvu zote, zinaidhalilisha tasnia ya urembo na wanawake kwa ujumla,” anasema. Anasema imefika mahali ile maana ya mashindano ya urembo inatoweka kwani inaonekana kama tasnia ya kihuni kutokana na mienendo ya baadhi ya warembo hao. “Ingepatikana sheria ambayo itawaadhibu warembo wanaokiuka maadili na kuidhalilisha tasnia hii, labda wangepunguza,” anasema Hoyce. Hoyce aliona kuwa ipo haja ya kuwepo Kamati ya Warembo wote waliopita na wa sasa ili wakutane, wakanyane, wazungumze maendeleo na waangalie wanakosea wapi ili warekebishe. “Maana ya urembo imetoweka, unajua ‘Miss Tanzania’ ni kuiwakilisha Tanzania nzima, sasa warembo wa siku hizi wanabadilisha maana halisi ya mashindano haya,” anasema. Mama huyu wa mtoto mmoja, anasema, ana mipango mingi ya kimaendeleo. Hivi sasa anaandika kitabu kitakachozungumzia dondoo za urembo wa asili,usiohitaji gharama. “Nataka watu wafahamu dhana ya urembo, si vipodozi vya gharama bali hata utembeaji, mavazi, vitu vya asili vinavyoweza kukupa ngozi nzuri, kama parachichi na limao, mavazi na mengineyo,” anasema. Lakini pia, Hoyce anawataka wanawake walio serikalini hasa wabunge, kutumia nafasi zao kuwatetea wanawake walio nje. Anawaomba wawakanye wanawake wanaokwenda kinyume, wasijitoe kuwasaidia wanawake wasiojiweza tu bali wakemee mmomonyoko wa maadili. “Tumekuwa tukililia nafasi mbalimbali za upendeleo, tunataka usawa, lakini kwanza tuwe na mienendo mizuri, tusijidhalilishe,” anasema. Anatoa ushauri kwa wanawake kutosubiri kuwezeshwa, bali waweke jitihada kwani wanaweza. Anasema, badala ya kuendekeza majungu, masengenyo, tutazamane kwa ujumla wetu, tusaidiane kwani maendeleo yapo mikononi mwetu. Hoyce alizaliwa mwaka 1978 mkoani Kilimanjaro. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Uhuru iliyopo mkoani Arusha kuanzia mwaka 1985, kisha elimu ya sekondari katika Shule ya Sekondari Arusha mwaka 1992 hadi 1996. Elimu ya kidato cha tano na sita, aliipata mwaka 1998 katika shule ya Zanaki jijini Dar es salaam. Alibahatika pia kupata Shahada ya Mawasiliano ya Umma katika chuo cha Arizona State University –USA mwaka 2005. Hoyce ambaye ni wa saba kuzaliwa kati familia ya watoto nane, alitunukiwa Stashahada ya Uzamili katika Menejimenti ya Mahusiano ya Kimataifa, mapema mwaka huu. |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani















