MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Johari Malezi:Familia ni zaidi ya baba, mama na watoto
BOOKMARK THIS PAGE
Malezi:Familia ni zaidi ya baba, mama na watoto  Send to a friend
Saturday, 04 February 2012 20:32


FAMILIA hutafsiriwa kuwa ni baba, mama na watoto, ingawa katika uhalisia wake ni mahali ambapo watoto wanajifunza kuishi na wenzao kwa upendo, amani na furaha.

Ni mahali pa kurithishana imani, ambapo watoto wanatambua wito na utu wao, kwa njia ya mifano bora ya wanafamilia na ambapo wanaweza kujifunza mambo mengi ambayo watayaweka katika uhalisia wa maisha yao.

Wazazi wanatakiwa kuwa na matendo yaliyo mfano bora wa kuigwa na watoto wao, kwa kuwa ndiyo waanzilishi wa safari ndefu ya maisha yao, tangu wanapoingia duniani kupitia mikononi mwao.

Familia yenye misingi bora kiimani, ni kiini cha maisha bora ya kijamii hivyo kila mzazi na mlezi anao wajibu wa kuhakikisha familia aliyomo inakuwa juu ya msingi wa aina hiyo.

Hayo yanatakiwa kuzingatiwa zaidi na wazazi wa sasa ili kuliokoa taifa na majanga yanayolikabili, likiwemo la myumbo wa uchumi; Kwa njia hiyo tabia za ubinafsi zinazosababisha rasilimali za jamii kuhujumiwa, zitakoma.

Kila familia ikifanikiwa kujenga mazingira bora ya kiimani ndani ya mioyo ya watoto wake na kuotesha mbegu ya upendo, kutii amri za Mungu na kuzishika; Itakuwa njia muhimu na kuu ya kukabiliana na mmomonyoko wa misingi ya kimaadili na utu wema ambao jamii ya Kitanzania inashuhudia kila kukicha ukishika kasi.

Wazazi ni washiriki wa uumbaji kimwili na kiroho. Hii inamaanisha kuwa, mtoto anapoingia ndani ya familia akiwa katika umri wa mwanzo kabisa, anakuwa sawa na karatasi nyeupe pee, (matendo na maneno yake katika maisha yake ya baadaye) ni kilichoandikwa katika maisha yake ya awali, bila shaka na wazazi au walezi walio ndani ya familia aliyomo.

Hakuna ubishi kuwa mazingira yanayozunguka mtoto awapo nje ya familia yake, yana nafasi ya kumuumba kitabia tofauti na alivyoumbwa na familia yake lakini ikiwa tabia yake imeumbwa juu ya msingi imara, siyo rahisi ukaharibiwa.

Ndiyo maana inashauriwa, mtoto asifunzwe kwa ukali na vitisho bali kwa upole, upendo na kujengewa uelewa ambao hata akiwa nje ya walezi wake, ataweza kusimamia alichofunzwa ndani ya familia kwa kuwa anaelewa kwanini anatakiwa kufanya alivyoelekezwa.

Hivyo wazazi na walezi wasikatishwe tamaa na mazingira mabaya kimaadili yanayowazunguka, kwa maana huwezi kujitenga na ulimwengu ulimo. La msingi ni kutekeleza jukumu lako kwa nafasi na wakati wako, kwa lengo la kuwajengea watoto uwezo wa kuwa watu bora na wema kwa nafsi zao wenyewe na jamii kwa ujumla.
Hata hivyo, jitihada hizo zinatakiwa kutekelezwa na wazazi huku wakitambua kuwa kila kitu hutakiwa kufanywa kwa kiasi, tofauti na hivyo mambo huenda mrama.

Hapa nazungumzia baadhi ya wazazi ambao hutoa nafasi kubwa kwa mtoto kiasi cha kudhulumu haki ya mzazi mwezake. Jambo hili si sawa kabisa.

Ikumbukwe, bila mke au mume mtoto asingepatikana hivyo ni jukumu la kila mzazi kutambua na kuzingatia mipaka ya haki ya mtoto ndani ya familia, ili malezi bora yasiathiri uhusiano wa wanafamilia.

Jambo hilo lisipozingatiwa, kuna uwezekano wa umoja wa kifamilia kupoteza mwelekeo  hata kufikia kiwango cha kuathiri malezi ya mtoto husika, jambo ambalo linaweza kuharibu kazi nzuri iliyokusudiwa.

Hivyo ifahamike kuwa kazi ya kulea mtoto kwa kiwango bora katika familia si ndogo na rahisi kama inavyoweza kudhaniwa, bali inaweza kuwa hivyo ikiwa hekima, busara na umoja wa kifamilia ukizingatiwa na kila mwanafamilia.

Imeandaliwa na Editha Majura, TSJ
0716 263949

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner