MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Hoja Binafsi Mwana wa gavana anapotenda kosa nani aadhibiwe?
BOOKMARK THIS PAGE
Mwana wa gavana anapotenda kosa nani aadhibiwe?  Send to a friend
Saturday, 04 February 2012 20:11



Maggid Mjengwa,

Ndugu zangu
KUNA  kisa cha mwana wa gavana katika Misri ya Kale.  Mwana  yule alitembea akijivunia cheo cha baba yake. Akajawa kiburi kufikia siku mmoja kumdhalilisha mwalimu wa shule mtaani . Alifanya hivyo huku watu wazima na watoto  wakiangalia.  

Mwalimu Yule wa shule alidhalilishwa. Ndio, mwana yule alimchapa bakora ya matakoni mwalimu yule, tena hadharani. Mwalimu alifedheheshwa sana, maana hata kosa lake hakulijua.  Mwalimu  akafunga safari ndefu kwenda kuarifu jambo lile kwa mfalme wa nchi . Huko akapokelewa. Akaeleza yaliyomsibu.

Mfalme akaamuru mwana yule wa gavana aletwe haraka kujibu shauri akimbatana na baba yake, yaani gavana. Baada ya kusikiliza shauri lile, mtawala yule akajiridhisha, kuwa mwana yule wa gavana alifanya kosa. Akamwamuru mwalimu yule achukue bakora na kumchapa mwana yule wa gavana bakora mbili.  Bakora za matakoni.

Mwalimu aliinua bakora kisha akaanza; moja, ikaja ya pili. Akatamka; “ Mfalme wangu, nimemaliza”. Mfalme akatamka; “Bado, chukua tena bakora mchape gavana bakora tatu za matakoni”.

“ Ewe Mfalme wangu, gavana hajanitendea kosa lolote, ni mwanawe”. Alitamka mwalimu yule. Mfalme akamwambia; “ Nimekwambia mchape gavana bakora tatu kwa kuwa bila ya yeye mwanawe asingetenda kosa hilo!”  Tendo hili linatuachia kazi ya kutafsiri. Hakika, kuna tunachojifunza katika hilo.

Kuna wakati Mwalimu Nyerere kupitia kitabu chake aliandika; “  Ndugu Rashid Kawawa alikuwa Waziri Mkuu wangu kwa muda mrefu . Hakuwa amefanya kosa lolote; lakini nilitaka kumbadili na kuteua Waziri Mkuu mwingine.

Nilimwita nikamwambia hivyo. Tukakaa pamoja, mimi na yeye, tukashauriana na kukubaliana juu ya ni nani  anafaa kushika nafasi yake.  Nikamteua hayati Edward Moringe Sokoine.  Najua , kuwa watu wa aina ya Rashid Kawawa ni adimu sana duniani, hawazaliwi kila siku. ’’

Mwalimu aliendelea kusema; “  Lakini,  hata hivyo, ni jambo la kushangaza kidogo, kwamba Viongozi wetu , hata bado hatujafa, wanaona kuwa ni kosa  kuwakumbusha kuwa  vyeo walivyo navyo ni dhamana. Wanadhani, kuwa Uwaziri ni Usultani; ukisha kuwa sultani utakufa sultani!

Nadhani wanakosea. Nchi hii iliwahi kung’oa masultani wa kila aina. Tukianza kuvumilia masultani wa kuchaguliwa tutapanda mbegu ya masultani wa kuzaliwa.” ( Mwalimu Nyerere; Uongozi Wetu na Hatima Ya Tanzania, uk, 45)
Mwalimu hakupata kufanya kazi ya utabiri, lakini, mengi ya aliyoyasema na kuandika unaweza kuyaona yakitokea kila siku ipitayo.

Ndio maana binafsi sichoki kusoma maandiko ya Mwalimu, ni shule kubwa.  Maana , leo tunaona  baadhi ya tuliowapa dhamana za uongozi wanavyopenda sana ‘ Ubwana Mkubwa’ kuliko kujiona kuwa ni watumishi wa umma.  Wanapenda ‘ Usultani’, na kuna walio chini yao wenye kuwanyanyasa  Wana wa Nchi kwa vile tu wao wenye kunyanyasa ni ‘ wateule’.

Na hakika, ni jambo  baya na la hatari pale kiongozi anapokimbiwa na wakati. Maana kuna tofauti ya kupitwa na wakati na kukimbiwa na wakati. Ni heri anayepitwa na wakati, maana anaweza kuukimbilia. Aliyekimbiwa na wakati  hawezi kuufikia tena hata kama atajaribu kuruka angani.Na Mwalimu  alipata kusema; “ Nchi yetu  bado changa.

Tusione haya kuendeleza taratibu ambazo zinaonekana kuwa  zinafaa, na wala kubadili zile ambazo japokuwa huko nyuma zimetufaa, lakini sasa zimepitwa na wakati.

Mwalimu alikuwa mtu huru. Ni hulka yake ya kusema anachoamini, bila unafiki wala hofu ndio iliyomfanya ajisikie kuwa mtu huru.  Kuna viongozi wengi wa nchi hii waliojifunza kuishi na kutenda kama Mwalimu ingawa ni kazi ngumu sana kuwa kama Mwalimu.

Ikumbukwe, kuwa katika dunia hii kuna wanaokufa, kufukiwa na kusahauliwa.  Lakini kuna wanaoishi milele hata baada ya kufa. Si binadamu wengi wenye nafasi ya kuingia kwenye kundi la wenye kuishi milele hata baada ya kufa. Hata matajiri wenye mali nyingi, kwa fedha zao hawawezi kununua nafasi hii ya kuwamo kwenye kundi la wenye kuishi milele hata baada ya mauti kuwafika.
 
Kutokana na matendo yao, jinsi walivyoishi na hususan kuwatetea
wanyonge wa nchi hii, katika nchi hii kuna mifano ya viongozi wanaoishi
na wataendelea kuishi hata baada ya mauti kuwafika. Mwalimu Nyerere, Edward Sokoine  na Rashid Kawawa ni baadhi ya mifano ya wanaoishi hata baada ya kufa.

Tuwaonee wivu na tuige mifano ya tabia na matendo yao. Na zaidi mapenzi yao kwa nchi yao waliyozaliwa. Uzalendo wao.
 
Ni dhahiri, kuwa muda wetu wa kuishi humu duniani ni mfupi sana.
Tofauti na wanyama, binadamu katika maisha yetu ya duniani, tuna
kawaida ya kufikiria hiba ya kuacha nyuma yetu, kwa familia zetu
na kwa jamii tunayoishi. Fikiri mtoto uliyemzaa akikuuliza; “ Mama/
Baba, ukiondoka hapa duniani ungependa tukukumbuke kwa lipi?
 
Hilo ni swali gumu kwa yeyote anayeulizwa. Majibu ya swali hili
yanatupa visheni/uona mbali wa anayejibu. Swali hili linahusu haiba ya
 
mtu anayoiacha nyuma yake. Haiba ambayo angependa akumbukwe
kwa kuhusishwa nayo, ni urithi, wazungu wanaiita ‘Legacy’.

0754 678 252, 0788 111 765, 0712 956131  
This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it ,
http://mjengwa.blogspot.com

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner