MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Hoja Binafsi MOYO UNADUNDA;Viongozi wa dini, mwanamke sio jiwe lisilo na hisia
BOOKMARK THIS PAGE
MOYO UNADUNDA;Viongozi wa dini, mwanamke sio jiwe lisilo na hisia  Send to a friend
Saturday, 04 February 2012 20:15



Na Assumpta Nalitolela

NIMEKUWA nikisikiliza sana mahubiri ya viongozi wa dini za kikristo kuhusu uchumba, maisha ya ndoa, wajibu wa wanandoa na haki zao na maisha ya wanafamilia kwa ujumla.  

Nimekuwa nikifuatilia mahubiri hayo kwenye luninga na wakati mwingine kwenda moja kwa moja kwenye mikutano yao. Mahubiri mengine ambayo leo ningependa niyazungumzie, licha ya kwenda kinyume na juhudi za Serikali za kuboresha afya ya Watanzania hasa watoto na kupambana na unyanyasaji wa binadamu wengine hasa wanawake lakini pia yanatoa sura tofauti ya Mungu wa upendo ambaye tumekuwa tukisikiliza habari zake tangu tukiwa watoto.

Mahubiri hayo yamezibariki ndoa kuwa kampuni za biashara zenye kuzalisha faida ambayo moja anakuwa mwekezaji na mwingine anakuwa mfanyakazi.

Baya zaidi mahubiri hayo yanamchukulia mwanamke kama jiwe lisilo na hisia, na kwamba ndiye peke yake mwenye wajibu wa kurekebisha matatizo ya ndoa.

Kwa mtazamo wangu naona mahubiri hayo yanaifanya dini kutokuwa na mchango wa maana katika kuimarisha ndoa na mahusiano ya kifamilia kitu ambacho ni hatari sana hasa ikizingatiwa ndoa hutoa walimu, madaktari, viongozi wa dini, mafundi, wanandoa wengine nk, hivyo kwa namna yoyote ile masuala ya ndoa yanapaswa kuchukuliwa kwa tahadhari.

Kwa wale mnaosikiliza mahubiri kwa njia ya luninga, naamini mmeshawahi kumsikia Mchungaji anayeshabikia mayai kula baba badala ya mtoto kama mila inasema hivyo, kwa sababu walioweka mila hizo walikuwa na nia ya kuweka alama zitakazoonesha heshima kwa kiongozi wa nyumba.

Piga picha ya kiongozi wa nyumba aliyenawiri halafu mtoto wake ana utapiamlo kwa sababu tu anataka kuonesha yeye ndiyo kiongozi wa nyumba. Kwangu mimi huko ni kwenda kinyume na juhudi za Serikali za kuboresha afya za watoto ambao ndio nguvu kazi ya taifa miaka ijayo.  

Lakini pia namshangaa mchungaji huyo kwa sababu ukiangalia maisha ya sasa kwa mtu maskini angalau anaweza kufuga kuku wa kienyeji kwa kule kijijini ambako elimu ya afya bora inahitajika sana; mchungaji anategemea maskini kama huyo mwenye kuamini mafundisho yake, watoto wake watatoa wapi protini kwa ajili ya makuzi yao?

Sitashangaa mchungaji kama huyu akitoa ushauri kwamba baba akifika watu wote wanyong’onyee na kujificha kuonesha kuwa mtu mkubwa sana ameingia ndani ya nyumba kwa sababu alionesha kukerwa na hata neno la mfumo dume, akiamini kwamba maisha yale ya ubinafsi wa wanaume ndiyo maisha yaliyoumbwa na Mungu.

Mungu ametoa amri ya wanawake kuwaheshimu waume zao sio kuwaogopa na kuheshimiwa huko hakupo kwenye mayai wala firigisi kama yeye anavyotaka watu waelewe. Kuheshimiwa huko kunaendeana na upendo.

Nyumba ambayo wanaona heri baba alazwe hospitali kuliko kuwako nyumbani hata kama wanampelekea mayai yake huko huko hospitali utasema baba huyu anaheshimiwa?
 
Wachungaji ninaowazungumzia leo wanawachukulia wanawake kama mawe fulani yasiyo na hisia, yanayoweza kuachwa mahali yakapigwa na jua na mvua yasipate madhara lakini bado yakaendelea kutumika na viumbe hai kwa kazi moja au nyingine.

Mwanaume anahama nyumbani kwake kwa mwezi mzima na katika hili kiongozi wa kiroho anaishia kumwambia mwanamke peke yake “Usimkasirikie mwanaume huyo kwani ukifanya hivyo atarudi tena alikotoka”. Neno “atarudi alikotoka” likitiliwa mkazo.

Kiongozi wa dini anapaswa kujua kwamba mwanamke huyo kama binadamu amepata maumivu hivyo anahitaji faraja na matumaini toka kwa Mungu ya namna gani maumivu yake yatapozwa sio kutishiwa kwamba huyo mwanaume atarudi alikotoka.

Mchungaji mwenyewe akikasirishwa anakasirika kweli lakini kwa kufuata maagizo ya Mungu, baadaye anasamehe na kuendelea mbele, anamtegemeaje mtu mwingine aoneshe tabasamu pale alipoumizwa? Halafu kama suala ni kutaka kuijenga hiyo ndoa mchungaji anafikiri kuondoka kwa huyo mwanaume kunamuathiri mwanamke tu?

Mchungaji anasahau kuna UKIMWI unaomsubiri mwanaume huyo, kuna hatari ya shetani kufanya mageuzi katika nyumba hiyo na kuleta mtawala mwingine wa nyumba ambaye anaweza akawa yeye mwenyewe mchungaji.

Kuepusha hilo mchungaji anapaswa kuelekeza juhudi zake kwa wote mwanaume na mwanamke akimng’ang’ania mwanaume kubadilisha mwenendo wake badala ya kumwongezea machungu mwanamke kwa vitisho vya “ataondoka tena”.

Katika kundi hilo la wachungaji wapo wanaihubiri ndoa kama kampuni ambayo mwanaume ni mwekezaji na mwanamke ni mfanyakazi anayesubiri kulipwa mshahara wake mwisho wa mwezi.

Kama tunavyojua mfanyakazi hatoi hela yake kuipa kampuni labda kama analipa deni alilokopeshwa na kampuni. Ndivyo wachungaji hawa wanavyotaka ndoa ionekana kwa mwanamke kutotoa kabisa fedha yake kusaidia uendeshaji wa familia.

Cha ajabu mwanamke huyo huyo anahimizwa kutoa sadaka na fungu la kumi kanisani kama maandiko yanavyotaka. Wachungaji wanapaswa kuwaacha wanandoa kupanga matumizi ya fedha zote zinazopatikana toka kwa wote wawili kwa ajili ya ustawi wa familia yao.

Kumshawishi moja kutochangia kwenye pato la nyumba ni kutaka kurudisha nyuma maendeleo ya nyumba zinazotegemea michango ya wote wawili. Hivi wapi panapoelekeza kwamba mwanamke kutoa fedha kwa ajili ya shughuli za kifamilia ni chukizo mbele ya Mungu?

Kama wewe ni msichana na bado hujaolewa, halafu ukawasikiliza wachungaji hawa utafikiria ndoa ni zigo moja kubwa la mahangaiko ambalo Mungu amelitengeneza kumwadhibu mwanamke.

Ni kweli tunasoma katika Biblia kwamba Adam na Eva walipomkosea Mungu, pamoja na adhabu nyingine Mungu alimwambia Eva, mumeo atakutawala. Sasa kama viongozi hawa wa dini wanaona kutawala ni sawa na kunyanyasa, basi hawana haja ya kuwakemea watawala wa nchi pale wanapofanya vitendo vinavyonekana kuwa ni unyanyasaji kwa wananchi wao.

Wakati umefika kwa wachungaji na viongozi wengine wa dini kubadilisha mwelekeo wa macho yao wanapohubiri toka upande wanakokaa wanawake kwenda kule wanakokaa wanaume na kuwapa maagizo sahihi ya majukumu yao katika ndoa, badala ya kuwaelekea wanawake tu kana kwamba wao ndio pekee wenye jukumu la kujenga  ndoa imara.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner