
| Mwashangaa:Ndoga gani hizo kama si uchuro au utapia akili? | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 20:16 |
|
Na Papaa Mawani NAJE? Acha tu nishangae hadi na akina Che Mala, Che Urdu, Che Beni na Che Pepe huko Nyengedi, Nanjota, Nanganga na Nkalapa waungane nami kuukemea huu ufisadi mamboleo. Ote! Binadamu kwa utashi wenu mmeamua kuuvaa uhayawani kwa kuingiza mzaha katika ndoa? Mmeamua kuuvaa ushupavu wa kunguni? Naapa sipati picha! Harika! Mmechagua kunguni awe mfano wenu wa kuigwa? Huenda kuna hoja ya msingi. Au ni kuvutiwa na ushupavu wa mdudu huyu? Nasikia anao uthubutu na upekuzi kuzidi viumbe wengine. Mnashangaa nini kana kwamba mlitegemea nimtaje tembo, faru, simba, mamba au nyati? Hatuongelei ukubwa wa umbo au uzito wa mnyama, bali tumejikita kwenye ushupavu. Kama ni ushupavu tu, kunguni kawazidi hao wote. Hicho ndicho kitu kinachompa heshima mjini. Ukiona vitanda au magodoro yanaanikwa juani, elewa tu kuwa keshakatisha kunguni. Si ushupavu huo? Hawa huingia popote, pawe Oystebay, Capri Point, Mikocheni, Njiro Hill, Masaki, Eastleigh, Shanty Town, Ununio au Manzese. Naapa wadudu hawa huenda bila kuwekewa zuio. Kunguni hawahitaji kupatiwa kadi za mwaliko popote watakapo kwenda, kuwe White House kwa Obama, Vatican kwa Papa Benedicto, au Pentagon kwa anko. Ndo “Free Pass” waliyozaliwa nayo. Turejee kwenye hoja ya msingi zaidi kuwa zama hizi kuna wanadamu shupavu mithili ya kunguni. Elewa kuwa kunguni hajali umevaa shati la rangi nyeupe au suti ya bei gani. Kunguni ni moto mara moja. Hachagui upo na akina nani au wamebeba wadhifa gani. Hana cha protokali kwenye sherehe au dhifa ya aina yoyote. Hawekewi ratiba na wala msijaribu. Hukatisha tu hata uwepo meza kuu au “Officers’ Mess”, ikiwa imesheheni wenye nafasi zao. Hawajui kama upo na mkweo au na baba yake. Tukio gani limtishalo kunguni nawaomba mnieleze. Kunguni bila soni hujipachika popote atakapo bila kujali utaadhirika vipi. Huyu hana cha geti la kumkwaza atakapo kupunga hewa au kuota jua. Huyu mdudu wala hajali utakuwa na mazungumzo na nani. Ni binadamu wachache tu wenye ushupavu huu. Wanaosikika sana ni hao wanaume wanaothubutu kuwaoa wanawake walowazidi umri. Hiki ni kipaji nadra sana. Hawajali wanafikiriwaje au hatma yao na hao ajuza wao ni ipi. Wala si hoja kama “Rest in Peace - RIP” za hao wenzi wao zinasomeka bayana kwenye resepsheni. Si ishu kusikia kuwa waliooana nao hawatakuwa na uwezo wa kupata watoto. Nalo hilo haliwasumbui. Wao wanachotambua ni kuwa farasi mzee ndiye mwenye uzoefu wa mizigo. Aidha, huamini kuwa ng’ombe haelemewi na nunduye. Tena hushikilia kuwa mchagua jembe si mkulima. Msidhani kuwa wanatafuta kutengeneza historia. Hapo ndo wamefika. Litawasumbua sana ninyi kwa pilipili msizozila. Mara mtawaza kuwa amempendea nini huyo “mzee”, kumbe yeye kamwona ndiye “lulu”. Mpo hapo? Sasa huu utaachaje kuwa ushujaa kwa mwanamume mwenye sifa zote anayeamua kumwoa mwanamke wa jika la mama yake mzazi? Kama kadhania huu ni ushupavu, basi anaelekea kwenye uchizi. Labda ushupavu unakojitokezea zaidi kwenye namna ya kuanzisha hoja hiyo ya kuoana. Anaanza na “shikamoo mama, shikamoo binti, shikamoo mtoto au shikamoo bibi”? Hapa kunahitaji ujasiri wa ziada. Ni mtu shupavu sana kwani uwezekano wa mtu huyu kutengwa na jamii kwa huu unyaa. Uwezekano huo ni mkubwa sana unapoamua kuishi maisha ya kinyama. Bisheni tu mkipenda. Eleweni tu sehemu nyingi duniani hususan huko kwao akina Mangi ukithubutu kumwoa aliyekuzidi umri, utakuwa mwisho wako wa kwenda hija za Krismasi ulizozoea. Kwanza afadhali usifike huko milimani kwani utawapelekea kichefuchefu na kuwakwaza nduguzo. Dada zako watamwita mkeo wifi, dada mkubwa, shangazi au wifi mzee? Marafiki wa kukutembelea watapungua sana kwa kuwa hayupo atakayetaka kumtambua huyo mama mzee wako kama shemeji. Kwani huelewi huko ni kuwakwaza? Kama umedhani ulichofanya ni fasheni, basi itabakia kuwa yako mwenyewe na mkeo. Kama ulikuwa ni msukumo wa ushirikina, basi mganga wako atakuwa kawini. Lakini, acha turejee na kwenye sera zetu za mahusiano ya kijinsia. Mtu wangu! Wapo ami ya wanaume wanaowaoa mabinti wenye umri wa binti zao wa mwisho. Hizi ni tabia zinazoashiria utapia akili. Huko ni kuwakwaza wanao wa kiume. Sasa tueleze hawa watamtambua huyo kadogoo wako kama nani? Ni shemeji, mama mdogo, anti au “hoyaa” mwenzao? Pia, utawakwaza wenzako utakaokutana nao. Wanaweza kukukosea heshima kwa kumtambua kimakosa kama bintio au hausigeli kumbe ni “something” yako. Acheni hizo wanakwetu! Kwanza ni uchuro wa kumwaga kuonekana ukichumbia ukubwani. Na wewe binti ni wazi huna adabu! Kwani amri zote za Mungu na mila zenu zinazokataza hayo hukuziona? Wewe binti mdogo wa umri wa mdogo wetu wa mwisho wataka nini? Au kisa unataka mshirikiane na huyu mstaafu kutafuna pensheni yake Hatimaye ukatambulike kwenye kifo chake kama mke wa marehemu? Lakini na wewe binti si tofauti na kunguni. Ulianzaanzaje kuujenga huo mradi? Ulimtambua kama baba, babu, bosi au mshikaji? Na huyo babu salamu zilitoka katika uwiano gani? Kwanza ukienda na huyo mkeo kliniki, manesi hawakawii kukukemea kuwa wanaoruhusiwa kwenye maeneo ya leba ni waume za wahusika na wala siyo baba wazazi. Si ni kutafuta kuadhirika? Mkienda kwenye sherehe, si ajabu baunsa akamzuia mkeo getini akidai watoto hawaruhusiwi. Sura hazidanganyi ni yupi wa marahaba na ni yupi wa shikamoo. Hata kwenye operesheni ya huyo dogo wako, utapambana na madaktari. Utakataliwa kusaini; ukitumwa ukamwite mumewe, kwani baba mkwe hawaruhusiwi kuwa na mamlaka hayo. Huko nyumbani nako utawakwaza dada zako. Watamtambua kama wifi, wifi kadogoo au anti? Kwanza ukweni ukifika majirani hawakawii kukudhania wewe ndo baba mkwe wa binti yao. Usikosee ukaibuka na wivu wa kumsindikiza mkeo saluni. Watakuona ni mnoko fulani au jibaba lenye wivu na bintiye, hadi linamsindikiza saluni. Kwa nini utafute kutungiwa nyimbo? |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














