MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Hoja Binafsi Nguvu ya Hoja:Nchi yangu Tanzania,
BOOKMARK THIS PAGE
Nguvu ya Hoja:Nchi yangu Tanzania,  Send to a friend
Saturday, 04 February 2012 20:17


itajengwa na nani?
ENZI zile za Mwalimu Julius Nyerere na falsafa yake ya Uhuru na Umoja, walikuwapo watu waliojitolea kufa kwa ajili ya nchi yao; waliojitolea kuipenda kwa moyo wa dhati; waliokuwa tayari kujitoa kulinda na kuienze kwa haki; waliokuwa tayari kutumia muda wao kufanya kazi kwa bidii na kusimamia uzalishaji;  na walikuwapo waliokuwa tayari kuitetea kwa mapenzi ya dhati na kudumisha umoja wa kitaifa.
Naukumbuka wimbo huu ambao ulitumika kuwahamasisha Watanzania kuipenda nchi yao uliotungwa na marehemu Moses Nnauye wenye maneno yanayosema:
“Tanzania, Tanzania,
nakupenda kwa moyo wote;
Nchi yangu  Tanzania,
 Jina lako ni tamu sana.
Nilalapo nakuota wewe,
Niamkapo ni heri mama wewe,
Nchi yangu Tanzania,
Nakupenda kwa moyo wote ....”
Maneno na sauti ya wimbo huu yakiimbwa kwa kutafakari kwa kina yana  msukumo na msisimko wa hali ya juu kiasi cha kumfanya mtu anayeimba na kuusikiliza kwa makini kububujikwa machozi na kupata hamasa ya hali ya juu kuitetea nchi yao kwa moyo wa dhati.  

Enzi hizo, vijana wa TANU wakiimba wimbo huo walipata morali wa hali ya juu (kama wa Moran wa Kimasai) na kutoa kiapo cha dhati kutoka katika sakafu ya mioyo yao kuitumikia na kulinda nchi yao kwa moyo wote.  

Hata vijana wa Kitanzania waliokuwa katika majeshi yetu hasa Jeshi la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania  (JWTZ) na Jeshi la Kujenga Taifa(JKT), walipata ari ya kulinda nchi yao kwa nguvu zote na kushiriki katika uzalishaji ili kuiendeleza pamoja na watu wake.
Hata wanasiasa na viongozi wa umma na taasisi nyingine walikuwa na hamasa hiyo hiyo ya kutetea maslahi ya Watanzania na nchi yao, ili pamoja na kuwa kisiwa cha amani, iwemo katika orodha ya nchi bora kiuongozi na maendeleo chini ya Kiongozi wao Mkuu Mwalimu Nyerere, ambaye alihubiri umoja na uzalendo kwa dhati kila kukicha ili kujenga nidhamu katika taifa letu changa wakati huo.
Baadaye, na hasa baada ya vita kati ya nchi yetu na  Uganda na hali ya maisha kugeuka kuwa magumbu na ulanguzi ulipozaliwa na kuwa sehemu ya maisha yetu, wimbo huo ulianza kutoweka taratibu na hatimaye kuzimika kabisa kuashiria kwamba; mapenzi ya Watanzania kwa nchi yao yalikuwa yamekwisha.  
Ni kweli wasingeweza tena kuuimba wimbo katikati ya matatizo na mateso ya umasikini.  Wasingeweza kuuimba wimbo huu wakiwa hawana matumaini.  Wasingeweza kuuimba wimbo huu wa mapenzi wakati wamebuni njia mbadala na binafsi ya kujikomboa kutoka kwenye ugumu wa maisha.  

Isingewezekana kwani kufanya hivyo ingekuwa ni usaliti na unafiki wa hali ya juu kwa nchi yao.  Hata mapenzi ndani ya wanandoa yakipungua misemo na nyimbo  hata maongezi ya mapenzi yanatoweka huku kila mtu akifanya analotaka  na hata kusalimiana na kupeana pole kwa kazi hupotea kabisa.

Isingewezekana  kuuimba wimbo huo kwa sababu hata wanasiasa na viongozi wa taasisi zote na baadhi ya waliokuwamo kwenye vyombo vya ulinzi walitumia nafasi zao kujikwamua kimaisha ili kukabiliana na hali hiyo na hata kutafuta namna ya kujiwekea akiba ya kutosha.  
Hali hiyo ilisababishwa na mabadiliko ya mfumo wa maisha  kwa Watanzania ambao ulipoteza kabisa mwelekeo na matumaini ya wananchi karibu wote wakiwamo viongozi, huku Mwalimu Nyerere akibakiwa na viongozi wachache jasiri na wenye roho ngumu.
Kadiri miaka ilivyokuwa ikisonga mbele, ndivyo uroho wa madaraka na mali ulivyoongezeka na uzalendo ulivyozidi kutoweka miongoni mwa Watanzania na hasa hamasa ya kuuimba wimbo wa mapenzi kwa nchi yao ulivyopotea kabisa.

Unafiki pia uliendelea kukua huku usanii na kubuni miradi hewa ukazaliwa mpaka ndani ya mfumo wa utawala na ndiyo kaburi la uzalendo na wimbo wa “Tanzania , Tanzania  nakupenda kwa moyo wote...”
Kwa wanaofuatilia mfumo wa maisha na siasa za Tanzania na vituko vyake, watakubaliana nami kwamba, wimbo huu ulianza tena kuimbwa mwaka 2010 wakati wa mchakato na harakati za Uchaguzi Mkuu kama njia ya kuwahamasisha Watanzania kuipenda nchi yao.

Lakini safiri hii ulianza kuimbwa kwa kutumia kanda zilizokuwa zimehifadhiwa katika maktaba za taifa letu na hasa Radio ya Taifa (TBC) ambayo zamani ilikuwa Radio Tanzania (RTD) kwa sababu ulisahaulika au kuzikwa ndani ya kaburi la ufisadi.
Marehemu akifufuka inakuwaje?  Watu wanakimbia wakidhani na mzimu au pepo lililochukua sura na mwonekano wake, hawawezi kukubali kukaa naye au kumshika mkono hata kama walikuwa wanampenda sana.  Hata kama alikuwa baba au mama, mtoto, mume au mke wake mpenzi. Ni vigumu na ni kazi ngumu zaidi.
Ulipofufuliwa wimbo huu ni wakati huo siasa za uchaguzi katika majukwaa ya kampeni zilikuwa zikihubiriwa na baadhi ya wagombe na wapambe wao kutahadharisha kulipuka vurugu, hivyo  wimbi ulifufuliwa kuwahamasisha wananchi kuipenda nchi yao na kutahadharisha au kuwatishia kuwa wasipoipenda nchi yao wataiingiza kwenye machafuko na kuharibu kabisa usalama na amani yao.
Huu ni unafiki na kujidanganya marehemu wa siku nyingi hawezi kusaidia kuleta mabadiliko wakati mioyo na dhamira ya waliokuwa hai inahubiri vingine.  Hatuwezi kuuimba wimbo huo kwa dharura kama ngao wakati matatizo yetu yanaendelea.

Hatuwezi kuimba na kutangaza mapenzi kwa Tanzania kwa midomo wakati watu na hasa viongozi wetu, wametawaliwa na ubinafsi unaosababisha hali ya maisha kwa Watanzania walio wengi kuwa maisha magumu.  

Kama viongozi na wanasiasa wanachangia  uchumi wa taifa kwa kukosa sera sahihi za kuleta maendeleo ya Taifa na kutatua matatizo sugu ya jamii, haitawezeka kuwashawishi wananchi kuipenda nchi yao kama zama za kale hata  zikiimbwa ngonjera na nyimbo zilizotumika wakati ule.  

Kwanza zimepitwa na wakati na haziendi sambamba na mazingira ya sasa ambayo hata kizazi chake kimebadilika ili kulingana na mazingira ya sasa.
Nataka kusema kizazi cha wakati wa shibe na raha kwa hali zote kinatofautiana na kizazi cha wakati njaa na ugumu wa maisha kama ilivyo katika nchi yetu sasa.

Waliozaliwa wakati wa uzalendo ni tofauti na wanaozaliwa sasa wa kifisadi na ulafi na ubabaishaji wa kisiasa . Wanazaliwa ili kukabiliana na changamoto za kifisadi na ikiwezekana, nao wawe mafisadi au kubuni njia ya kutoa ufisadi kwa ngonjera za kale ambazo hawazijui.  Kwanza hawagusi kama ilivyokuwa wakati ule.
Si rahisi kuuimba na kupata hisia za kweli katika mazingira ya kukosekana huduma muhimu za jamii, katika mazingira ya mgomo wa madaktari na vifo vya watu kwa kukosa tiba; katika mazingira ya hali ngumu ya maisha na uchumi mbaya unaoendelea kuporomoka; katika mazingira ya mfumo wa bei unaosababisha watu kupunguza mlo na bei mbaya za vyakula;

Katika mazingira magumu ya kupata elimu; katika mazingira ya wanasiasa kulipana na kugombea posho bila kujali hali halisi ya uchumi wa taifa na umasikini wa wananchi wao na katika mazingira ya rasilimali za taifa kuporwa na viongozi wao kwa kushirikiana na makabaila wa nje wanaokuja chini ya mwamvuli wa uwekezaji!
Ni ajabu kwamba, kiongozi wa Serikali anakubali kusaini mradi wa kuhujumu rasilimali  na uchumi wa taifa kwa kupewa fedha na wawekezaji au wazabuni halafu utajiri huo unaenda nje,  huku yeye akiishi kama yuko paradiso pamoja na familia yake na kuwapuuza Watanzania wengine.  

Halafu wanasiasa wanahamasisha  Wimbo wa ’’Tanzania nakupenda kwa moyo’’  kwa masilahi yao. Ndiyo, wao wana haki kusema nakupenda kwa moyo wote kwa sababu imewapa ulaji kwa upendeleo badala ya Watanzania wote!
Mimi naihurumia nchi yangu na naililia kwa sababu inakoelekea siko tulikotamani kufika. Vijana wetu wanaangamia kwa dawa za kulevya magonjwa hatari ya Ukimwi na TB kwa sababu baadhi ya viongozi wetu wameamua kukiangamiza kizazi hiki.
Nafikiri kwa uchungu kwamba, kama vijana wetu wanakuwa wavuta bangi, tutakapoondoka sisi, tutaicha Tanzania ya kizazi cha ina gani? Yaani cha wavuta bangi na wala dawa za kulevya zinazosambazwa na watu wazima tena wenye akili timamu, wakiwamo wanasiasa na maofisa wetu wa umma!

Piga picha vurugu zinazotokea vyuoni. Je, tumewahi kuangalia upande wa pili wa shilingi tukajua tuna vijana wa aina gani humo vyuoni.  Kama vyuo vinakuwa na asilimia kubwa ya wavuta bangi na wala dawa za kulevya unategemea nini? Wakimaliza shule hao ndiyo watakuwa viongozi wa nchi yetu wakiwamo wanasiasa na mawaziri. Je, kuna taifa endelevu...?  
Ebu fikiria waziri mvuta bangi, atakuwaje huyo? Maana yake akiingia ofisini lazima avute bangi. Atafanya kazi nzuri huyo nchi yetu imeharibika. Ebu fikiria daktari bingwa mvuta bangi atakuwaje huyo na huduma yake itakuwaje.  Ebu fikiria walimu, mhariri mvuta bangi na wengineo...
Daniel Mwaijega ni Mhariri wa Gazeti la Mwananchi Jumapili
O713 704 898/ 0688 182 088

Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner