
| Nchi yetu tajiri wa maneno, wananchi wake sura masikini | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 20:19 |
|
Neville Meena TUNANGOJA kusikia kiwango cha fedha kilichokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mwezi Januari mwaka huu, ili tupime iwapo ni halali kwa nchi yetu kulia njaa. Nasema hivi kwani Januari 17, mwaka huu TRA walitangaza kwamba Desemba mwaka jana, walifanya ‘kufuru’, pale walipoweza kukusanya kodi kwa kiwango ambacho hakijawahi kufikiwa tangu kuundwa kwake, zaidi ya miaka 15 iliyopita. Vyombo vya habari vilimnukuu Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipakodi wa TRA, Allan Kiula akisema Desemba, mamlaka hiyo ilikusanya Sh682.5 bilioni na kuvuka lengo la Sh645 bilioni lililokuwa limewekwa. Kiula alisema Novemba mwaka jana mamlaka hiyo pia ilikusanya Sh512 bilioni ambazo pia zilikuwa hazijawahi kukusanywa kabla. Naam mafanikio makubwa sana haya. Hii ingekuwa dalili njema kwa nchi yetu kwani kuvunja rekodi katika ukusanyaji wa mapato, kwa lugha rahisi kunamaanisha Serikali kuwa na uwezo wa kutekeleza mahitaji yake ya kibajeti na kuwa na ziada kwa ajili kukabilina dharura zozote zile. Lakini ajabu na kweli kwa nchi yetu tukufu Tanzania, kwani hali ni tofauti. Kukusanya zaidi hapa kwetu pengine kuna maana tofauti ambayo ni ukata zaidi na hali mbaya zaidi ya kifedha!. Nasema hivi kwani yapata miezi minne sasa tunaambiwa nchi iko katika hali mbaya kifedha. Katika siku za karibuni malipo ya mishahara kwa watumishi Serikali imekuwa yakichelewa bila kutolewa kwa ufafanuzi wowote wa sababu za ucheleweshaji huo. Mathalan, hadi jana jioni wakati naandika makala haya, wapo watumishi wa Serikali nchini ambao walikuwa hawajalipwa mishahara ya Januari. Hali hii ni tofauti na walivyozoea kwani wengi wanasema mishahara yao ilikuwa ikiwahi na kila ilipofika tarehe 26 ya kila mwezi, walitembelea benki zao na kukuta fedha zao zikiwa tayari. Ukata Serikalini pia una mchango mkubwa katika mgomo wa madaktari ambao umeifikisha nchi pabaya, kwani kiini cha mgomo huo ni kuchelewa kwa malipo ya posho kwa madaktari wanafunzi kwa miezi ya miwili. Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hadji Mponda alikiri kuwapo kwa uchelewashaji wa malipo ya posho za madaktari wanafunzi na kwamba hali hiyo ilitokana na ukata ulioikumba wizara, mwishoni mwa mwaka jana. Licha ya mifano hii na mingineyo, Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo mara kadhaa amenukuliwa akisema “fedha zipo, tena za kutosha” na kwamba wizara na idara za Serikali zifuate taratibu katika kuomba fedha husika. Lakini sasa ni dhahiri kwamba kuna ukata serikalini, kwani juzi Rais Jakaya Kikwete alikiri kuwa hali ni mbaya kifedha kiasi cha Serikali kushindwa kutekeleza baadhi ya shughuli katika idara zake mbalimbali. Rais Kikwete alitoa kauli hiyo wakati akitoa salaamu za maadhimisho ya Siku ya Sheria zilizofanyika nje ya Viwanja vya Mahakama Kuu Dar es Salaam, kauli ambayo ilitokana na kilio cha Jaji Mkuu, Mohamed Chande Othman kuwa Mahakama nchini imekuwa ikishindwa kutekeleza majukumu yake kwa mafanikio kutokana na ama kucheleweshewa pesa au kupewa chini ya mahitaji. Rais Kikwete anasema ukata Serikalini unatokana na hatua ya kulipia malimbikizo ya madeni ya nyuma, ambayo hata hivyo hakuyaweka wazi. Pamoja na kauli hii ya Rais kuna mambo mawili ya kuhoji; Kwanza siku zote Serikali ilikuwa wapi kuwaelea Watanzania kuhusu sababu za ukata ambao umekuwa mwiba mkali na kusababisha ugumu wa maisha yao? Lakini pili ni ipi mipango ya Serikali katika utekelezaji wa bajeti yake, hivi ni kweli kwamba ilipanga kulipa madeni kiasi cha kuwaumiza Watanzania kwa kunyang’anya fedha zilizostahili kugharamia huduma nyingine muhimu za jamii? Lazima tufahamu kwamba tangazo la TRA kwamba imevunja rekodi linakuwa na maana tu pale wananchi wanapoweza kupata huduma na mahitaji yao muhimu ya kila siku. Ikumbukwe kwamba yawe mabilioni au matrilioni, makusanyo ya TRA yanakuwa na maana ikiwa wananchi wanapata huduma stahili na kwa wakati. Hakuna maana ya kuhubiri maneno ya utajiri, hali tukiwa na sura za umasikini. Mwandishi ni Mhariri wa Mwananchi Jumamosi – 0787 - 675555 |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














