
| Kuna siri gani katika posho za wabunge wetu? | Send to a friend |
| Saturday, 04 February 2012 20:20 |
|
Na Julius Samwel Magodi MARA nyingi Serikali inapoanza kujisahau na kuanza kufanya mambo yasiyofaa kwa wananchi wake, huwa inaona kama kitendo hicho ni jambo la kawaida ambalo haliwezi kuwa na madhara kwake. Dalili kuwa Serikali imeanza kujisahau ni Wanasiasa au watawala wake kutumia mabavu kufanya maamuzi hata kama wananchi hawayataki, kwa mwavuli kuwa wanafanya maamuzi hayo kwa manufaa ya umma. Ipo mifano mingi ya watawala waliofanya mambo mabaya kwa wananchi wao kwa kisingizio kuwa wanataka kugeuza nchi zao kuwa za asali na maziwa. Hata Dikiteta Adolf Hitler wa Ujerumani, alipoamua kuanzisha Vita ya Dunia na kuwaua Wayahudi, alitumia ushawishi wake kuwa hatua hiyo ilikuwa na lengo la kuwanufaisha wananchi wa nchi yake. Kinachofanywa sasa na Bunge na Serikali kutaka kupandisha posho za wabunge kwa kisingizio cha kupanda kwa gharama za maisha kwa wabunge, ni kilio kilichoficha sura ya ukatili kwa wananchi wanyonge wa Tanzania. Suala hili la kusikitisha la kupanda kwa posho za wabunge, limegeuka kuwa kama sinema hadi lilipofikia sasa: Kwanza lilianza kwa gazeti la Mwananchi kuchapisha taarifa za kupanda kwa posho za wabunge kutoka sh 70,000 kwa siku hadi Sh 200,000. Lakini Katibu wa Bunge, Dk Thomas Kashililah alikanusha vikali kuwa hakuna kitu kama hicho. Kama hiyo, ilikuwa mwanzo wa picha tu, Spika Anne Makinda akaibuka akampinga Katibu wake akisema kuwa kweli posho za wabunge zimepanda. Baada ya hapo wananchi, wanasiasa, wanaharakati, wasomi na viongozi wa dini, wakasimama kidete kupinga posho hizo. Hoja ya msingi ikiwa; maisha magumu ni kwa wabunge tu, mbona hata wananchi na watumishi wengine wa serikali wanaishi katika nchi hii na sio sayari nyingine kwa nini nao wasiongezewe? Ikaonekana uamuzi huo umechukuliwa kwa maslahi ya wabunge tu na kwamba fedha zote ambazo mbunge anapata kwa mwezi kiasi cha zaidi ya Sh milioni saba, ni kikubwa ambacho hakiwezi kulalamikiwa hata kidogo. Serikali na wabunge wakaziba pamba masikioni, hawakusikia lolote wakaendelea na uamuzi wao, wiki hii kabla ya Bunge kuanza, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda na Spika Makinda wakatangaza rasmi kuwa posho hizo sasa zimepata baraka ya Rais Jakaya Kikwete na kwamba sasa mbunge atalipwa Sh 330,000 kwa siku. Lakini cha ajabu siku iliyofuata Kurugenzi ya Mwasiliano Ikulu, ikatoa ufafanuzi wa taarifa hiyo ikieleza kuwa Rais hajabariki posho hizo isipokuwa, amekubali haja ya kuangalia upya posho kwa wabunge, lakini amewataka wabunge kutumia hekima na busara katika kulitafakari suala hili. Pia Rais Kikwete amewataka wabunge kutumia mkutano unaoendelea wa Bunge, kulizungumza upya suala hilo. Kwa hakika, ukiangalia kwa makini mfululizo wa matukio ya suala hili la posho unaweza kungundua kuwa kuna kitu ambacho kimejificha ndani yake. Suala hili bado limegubikwa na maswali kadhaa ambayo tunajiuliza. Je, Spika Makinda na Waziri Mkuu Pinda kweli wangethubutu kulidanya Bunge kuwa Rais ametoa baraka zake kama hawakuwa na uhakika na hilo? Kama walidaganya basi, kuna haja Bunge na Rais Kikwete kuwachukulia hatua za kuwaondoa. Ni jambo la ajabu sana kiongozi wa shughuli za Serikali bungeni, Waziri Mkuu na Mkuu wa mhilimi wa dola yaani Bunge, kusimama kumsingizia Rais. Ni wazi kosa hilo ni kubwa ambalo tumeshuhudia viongozi wa nchi nyingi wakiwaondoa wasaidizi wao wanapofikia hatua hiyo, achilia mbali shinikizo la wananchi. Lakini kama Waziri Mkuu, anaona kuwa alichokisema ni sahihi, lakini mkuu wake amemtwisha mzigo ambao hastahili, uamuzi ni mmoja tu ambao anaweza kuuchukua ambao ni kuachia ngazi. Ni jambo la fedheha sana, Waziri Mkuu Pinda na Makinda na baadhi ya wabunge kufurahia kupandishwa kwa posho zao wakati watumishi wengine wakiwamo madaktari wanaoendelea na mgomo, wakidai kuongezewa mishahara. Lakini jambo lingine ni kwamba, tulidhani kuwa wabunge wetu wangekuwa wanaelewa hali mbaya ya kifedha ambayo Serikali inayo kwa sasa, badala yake wangezungumzia mikakati ya kuibana Serikali ikusanye kodi zaidi. Tulitarajia wabunge wangeibana Serikali ipunguze matumnizi mabaya ya fedha za makusanyo ya kodi ili fedha zitakazopatikana ziweze kuifanya Serikali iwe na uwezo wa kuwapa huduma mbalimbali wananchi wake. Leo wakati wabunge wakitaka kuongezewa posho, zahanati nyingi zilizopo nchini hazina dawa, maabara, watendaji na nyingine zimegeuka kuwa mazalia ya popo. Lakini hata shule za kata ambazo Serikali inakataa kuitwa ‘vodafasta’ au ‘yeboyebo’ nazo hazina majengo ya madarasa ya kutosha, nyumba za walimu, maabara, madawati na walimu. Shule hizi zimebaki kuwa takwimu tu za Serikali kutamba kuwa imejenga shule nyingi za sekondari ambazo zinazalisha wanafumzi wa kidoto cha nne. Tulitarajia wabunge wetu wangeibana Serikali ieleze kwa nini bado inaendelea kutoa misamaha ya kodi mingi kwa bidhaa zinazoingizwa nchini wakati hivi sasa imeshindwa hata kupeleka fedha za ruzuku kwenye halmashari nchini. Kwa mujibu wa Ripoti ya Misamaha ya Kodi ya mwaka 2010, karibu asilimia 20 ya bajeti ya Serikali yote ilikwenda kwenye misamaha ya kodi. Hii ni hatari sana kwa uchumi wa nchi, kwani ni sawa na kujaza pipa la maji lililotoboka chini. Wabunge na Serikali sasa ni wakati mwafaka kupima wanachotaka kukifanya kama ni uzalendo au uporaji dhidi ya wananchi wanyonge. 0754 304336 This e-mail address is being protected from spambots. You need JavaScript enabled to view it |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani














