MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Habari Kilaini: Kikwete bado ni chaguo la Mungu
BOOKMARK THIS PAGE
Kilaini: Kikwete bado ni chaguo la Mungu  Send to a friend
Sunday, 23 May 2010 00:10


LAKINI ATAKA AWATIMUE MAWAZIRI, WASAIDIZI WANAOMUANGUSHA
Julieth Kulangwa
MIAKA minne iliyopita Askofu Methedious Kilaini wa Kanisa Katoliki alimuelezea Rais Jakaya Kikwete kuwa ni "chaguo la Mungu" na hadi sasa hajabadili msimamo wake, lakini anasema wasaidizi wake na mawaziri wake wanamuangusha na hana budi kuachana nao iwapo atachaguliwa tena kuongoza nchi.
“Mwaka 2005 niliwahi kusema kuwa Kikwete ni chaguo la Mungu... kwa maana kwamba kiongozi yeyote anayechaguliwa na watu anakuwa amesimamishwa na Mungu," alisema Kilaini katika mazungumzo na Mwananchi Jumapili.
"Miaka minne baadaye ameendelea kupendwa kwa kiasi kilekile na wananchi kwa kuwa kweli ni chaguo hasa ambalo Watanzania walilihitaji.”


Askofu Kilaini ametoa kauli hiyo wakati Rais Kikwete akiangaliwa kwa mtazamo tofauti katika kipindi ambacho anaelekea kumaliza kipindi cha miaka mitano cha utawala wake, na hasa baada ya kutoa kauli kali dhidi ya wafanyakazi mapema mwezi huu.


Serikali ya JK pia iliingia kwenye mgogoro mkubwa na viongozi wa kidini katikati ya mwaka jana baada ya bajeti kuu kuonyesha kuwa taasisi hizo zimefutiwa msamaha wa kodi uliokuwa unatolewa kwenye vifaa mbalimbali vinavyoingizwa kwa ajili yab huduma, kiasi cha Waziri Mkuu Mizengo Pinda kulazimika kufanya mikutano ya haraka iliyomalizika kwa msamaha huo kurejeshwa.


Lakini Askofu Kilaini anaona kuwa mapungufu yaliyoibuka kwenye serikali ya JK yalitokana na udhaifu wa mawaziri na wasaidizi wake.


“Yapo mambo ambayo hayakwenda vizuri katika kipindi hiki, lakini ukiangalia yeye kama rais hawezi kujua kila kitu... anahitaji kusaidiwa na watendaji wake wa karibu na hawa wamekuwa wakimwangusha mara kwa mara," alisema Askofu Kilaini katika mahojiano na Mwananchi Jumapili.
Kiongozi huyo wa kiroho alisema wapo baadhi ya mawaziri ambao hawajamsaidia rais wala kutimiza wajibu wao kwa nyadhifa walizopewa na kwamba hao ndio waliochangia kuitia doa serikali ya Kikwete.
“Wapo mawaziri ambao hawajafanya chochote tangu alipowateua," alisema askofu huyo ingawa hakuwa tayari kuwataja mawaziri hao.


"Inafikia wakati rais au waziri mkuu analazimika kufanya majukumu yao (ya mawaziri hao). Hawa hawamfai na rais inabidi asiwateue tena baada ya uchaguzi ujao.”


Askofu huyo, ambaye amekuwa hasiti kuzungumzia masuala mbalimbali kila anapotakiwa kufanya hivyo na vyombo vya habari, pia aligeukia wasaidizi wake na kueleza kuwa kwa kiasi kikubwa ndio waliochangia kumwangusha JK.
Alisema rais hawezi kujua kama hoteli anayokwenda kuizindua imejengwa kwenye hifadhi ya barabarani, alisema Kilaini akirejea tukio la hoteli ya kitalii ya Arusha ambayo Kikwete aliifungua rasmi na sikku moja baadaye ofisi ya Wakala wa Barabara (Tanroads) mkoani Arusha ikavunja ukuta wa uzio kwa sababu ulijengwa ndani ya hifadhi ya barabara.
"Ni kazi ambayo ilitakiwa kufanywa na watu ambao wanalipwa mishahara mikubwa inayotokana na fedha za walipa kodi. Hawa wamekuwa wakimwangusha kwa kumuingiza katika mambo yasiyofaa," alisema Kilaini.
Awali akifafanua sababu za kuendelea na msimamo wake kuwa Rais Kikwete ni kipenzi cha wengi, Askofu Kilaini alisema kuwa kiongozi huyo wa serikali ya awamu ya nne amekuwa karibu na wananchi, hivyo si vibaya wakampa tena nafasi ya kuongoza nchi.


Lakini, Kilaini ambaye ni askofu msaidizi wa jimbo la Bukoba, aliliambia gazeti hili kuwa katika kipindi cha utawala wake wa miaka minne iliyopita, Rais Kikwete alijiweka karibu na wananchi  ndio maana ameendelea kupendwa.
Askofu huyo, mwenye msimamo wa wastani dhidi ya serikali, aliongeza kwamba Kikwete anapendwa kwa kuwa ni rais aliyejiweka karibu na jamii tofauti na marais wengine, hali iliyosababisha kupendwa na wananchi.
Kilaini alimsifu Kikwete kuwa ni rais pekee aliyefungua milango ya ukweli na uwazi kwa kuacha kila kitu kizungumzwe na kuchambuliwa kwenye vyombo vya habari kwa mapana yake bila mipaka.


“Ni Rais aliyeruhusu uhuru wa kuongea; vyombo vya habari vinaandika na watu wanazungumza kila kitu bila kuingiliwa au kunyamazishwa. Kwa dhamana aliyonayo angeweza kuzuia mambo haya, lakini anaawaacha watu wachambue mambo yanayowahusu mpaka ukweli utakapopatikana," alisema.
Aliongeza kusema: "Mfano, kuna habari iliwahi kuandikwa na gazeti moja kuwa Rais Kikwete alinilipia matibabu nchini India wakati fulani nilipougua. Haikuwa habari ya kweli, lakini rais hakutaka kulizungumzia na kuwaachia walioanzisha walimalize.”


Alisema kwa uhuru huo alioutoa mkuu huyo wa nchi, umemfanya kuwa mmoja kati ya marais walioandikwa sana na vyombo vya habari na kushambuliwa na vyama vya siasa.


Kilaini aliongeza kwamba Rais Kikwete  anapaswa kuendelea kuongoza hasa kutokana na uwezo mkubwa aliouonyesha katika suala la kuushugulikia mgogoro wa kisiasa wa Zanzibar.
“Suala la Zanzibar lilikuwa gumu na hakuna aliyefikiri kama angeweza kulishughulikia na kulifikisha hapa lilipo katika kipindi kimoja tu... kwa hili amejitahidi na kwa kweli anahitaji msaada ili nchi yetu iendelee kuwa kisiwa cha amani ulimwenguni,” aliasa Watanzania.


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #15 2010-08-21 17:39
Bwana awe nanyi!

Baba askofu ni binaadamu na mchungaji pia. Kuna wakati anatoa maoni kama mtu mwingine na kuna wakati anazungumza katika kiti chake cha uchungaji. Kama binaadamu pia askofu ana haki na uhuru wa kumpigia kura mtu na chama chochote anachokipenda lakini hana haki ya kuwachagulia waumuni wake kiongozi iwe moja kwa moja au kwa taathira. Hata hivyo, kiongozi anaposhinda uchaguzi na kuwa kwa mfano, raisi, askofu pamoja na taasisi yake wakiwa kama subjects ya dola wanawajibika kuikubali na kuitii dola iliyopo madarakani. Ndipo hapo dhana ya viongozi ni chaguo la Mungu inapokuja. Nadhani baba askofu alikuwa anamaanisha dhana hii ya pili.

Kwa ujumla nakubaliana na wachangiaji wote kwamba viongozi wa dini hawapaswi kuwachagulia waumini wao chama au kiongozi. Naamini pia, viongozi wa dini ni mahiri na wameandaliwa zaidi katika anga zao za kidini. Katika fani nyingine kama siasa ni watu kama sisi na wengine hawana elimu na taarifa ya kutosha katika siasa. Waumini tunapaswa kuwaheshimu na kuwafuata katika mambo ya kidini. Wakiingia katika anga za siasa tupambane nao kama watu wa kawaida tu na hamna dhambi yoyote tutakayopata.
Quote
 
 
0 #14 2010-06-04 16:11
Tumsifu Yesu Kristu,Baba Kilaini. Hivi Baba Askofu,ni wewe tu unayejua vizuri mahusiano ya Jk na Mungu? Mbona hatuwasikii maaskofu wengine wakiyasema hayo maneno. Kwenye kongamano la taasisi ya Mchonga,wewe ni kati ya wachangiaji waliokuwa msitari wa mbele kuponda serikali ya Jk na Jk mwenyewe,na leo unatuambia Jk ni chaguo la mungu,Mungu hawezi kutupatia kiongozi mwanamtandao,tu memkosea nini watanzania. Jk anashindwa kuchukua maamuzi kutokana ni mwanamtandao. Baba wewe kama unaajenda yako binafsi,muogope mungu. Kilaini wewe ni msomi mzuri na uwelewa wako ni mpana,usituchan ganye,vipi mfate Slaa tujue moja.
Quote
 
 
0 #13 2010-06-03 11:56
tulimpenda sana rais kikwete na ndio maana tukamchagua,na alipo ingia madarakani kweli aliingia kwa vishindo vikubwa sana vya kutukomboa,na hakujali chochote kile au teyote yule ila alitizama maslahi yetu watanzania wanyonge,lakini cha ajabu amebadilika ghafla na kusahau kwanini yupo ktk kiti cha hukumu(kwani ni majukumu mbele ya mungu kuchukuwa majukumu yetu wanyonge)sasa sijui kipi kimempata raisis wetu amekuwa akielemea kwa viongozi na si raia,hadi kufikia kutoa maneno makali kwa ajili ya mishahara-tunaelewa hakuna hela lakini zinazo ibiwa na kina richmond na wenzake hizo hela zinatoka wapi?na hapo mbona ukali wa rais haukuonekana?je kuna skendo yoyote imebambwa na ndio anakubaliana na yote?ili hiyo skendo isitoke?mimi kwa imani yangu kwa rais wangu nampenda sana ila raisi huyu si yule asiemuogopa mtu ila HAKI(I DONT KNOW WAT HAPEN TO HIM!
Quote
 
 
0 #12 2010-05-28 19:00
Tabu ya Watanzania hamtaki tukiambiana ukweli na ndio maana hatuendi mbele.Mimi mada zangu hamzitoi kwa kuwa nazidisha kusema ukweli.JK sio chaguo la Mungu mimi nakatasa kata kata.
Quote
 
 
0 #11 2010-05-28 15:15
Tafuta wengine wa kuwaambia sisi tunamjua Mungu na hakusema huyo ni chaguo lake. Kama vipi acha uaskofu ingia siasani tujue moja.

Mnapotosha waumini, kwa faida au maslahi binafsi hiyo ni dhambi kubwa. ACHA KABISA KUSEMA NI CHAGUO LA MUNGU.
Quote
 
 
0 #10 2010-05-28 03:35
Mimi nadhani bb Kilaini angefundisha tu imani na mambo ya kanisa asijaribu kuwapeleka watu upande wasiotaka. Huyo chaguo la Mungu juzi tu kawatukana tucta au ndo tuseme Mungu alimtuma?
Nchi haieleweki inaelekea wapi, leo dola ni sh 1400- 1500, sababu kubwa ni pesa za ujanja ujanja za kifisadi kuwepo mtaani chini ya usimamizi wa JK, bora ningekuelewa ungesema Baba wa Taif ni chaguo lakini sio huyu. Tafadhali tafuta cha kufanya kama umekosa acha kabisa siasa.
JK kaja marekani mara ngapi? serikali imelipa kiasi gani? je tumepata faida kwa yeye kuja huku? Walimu, wauguzi wanaumia wewe unasema ni chaguo la Mungu, angalia watu huacha kwenda kusali sababu nyingine ni kama hizi. ACHA KABISA NAKUHESHIMU BABA ASKOFU, ACHA KUMUHUSISHA MUNGU NA WATU WA NAMNA HII. Kuchaguliwa na wengi kwa u[NENO BAYA] sio Mungu, chaguzi zenyewe mizengwe tupu. MIMI UMENIKWAZA SIPENDI.
Quote
 
 
0 #9 2010-05-27 12:34
Nampongeza baba asikofu amesema ukweli kuhusu raisi wetu maana jamani penye ukweli uongo ujitenga suala la zanzibar lilikuwa zito nani asiyekumbuka uchaguzi wa mwaka 2000? ndugu zangu watanzania hima tumpe kura kikwete maana amefanya mengi ila namshauli kama atachaguliwa tena asisahau kuiweka zana iliyobora katika uchaguzi wake wa mawzari wajao zana hiyo ni mweshimiwa Magufuri pia hikibidi awe tena wazari wa miundo mbinu au hata waziri mkuu maana ukweli nikwamba katika mawaziri wote huyo jamaa ni mchapa kazi kweli kweli.
Quote
 
 
0 #8 2010-05-26 15:04
Tumsifu Yesu Kristo Amen.Maskofu ,Mashehe, na Wachungaji msituingize kwenye majaribu.Mwaka ule mkaiponda CCM baada ya kikao na Mheshimiwa mnasema ni chaguo la Mungu.Mimi najua nyie ni binadamu kama binadamu wengine kama mmepewa "KITOCHI" mseme na msijaribu kuingiza Watanzania katika migogoro.Nchi hii ni ya Demokrasia hatujawaomba mtuchagulie RAIS.
Quote
 
 
0 #7 2010-05-25 12:47
Sote tunapaswa kumheshimu Mhashamu Kilaini kama kiongozi wa dini. Hilo halina ubishi. Lakini, matamshi yake ya kisiasa yanayumbayumba. Wakati ule wa kongamano la miaka kumi ya Kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K Nyerere, Baba askofu Kilaini alionekana kuponda uongozi wa Rais wetu. Sasa amegeuka na kusema anaangushwa na wasaidizi!!! Baba Yetu Yesu alipouwawa msalabani kwa ajili ya mateso yetu hakusema ameangushwa na wanafunzi wake. Alikubali kubeba msalaba wake kwa ajili ya wengine wote.

Wengi nadhani wanashindwa kumwelewa Baba Askofu Kilani. Anabadilika badilika kama kinyonga!!!
Quote
 
 
+2 #6 2010-05-25 11:04
Sawa tumekusikia askofu Kilaini, lakini hujatuambia JK ni chaguo la Mungu yupi.
Quote
 
 
0 #5 2010-05-24 13:53
kwako casian, askofu kama kiongozi wa dini anayo haki yakuchambua mambo kama raia na ni haki yake kikatiba kama mtanzania.Na pia unapaswa kujua dini na siasa vilikuwepo kuanzia enzi za utalawa wa dunia naamanisha Roman empire. Na pia dini ina nafasi yake katika utawala wa nchi yeyote, kwa nn akichaguliwa rais awe mkristo au mwiisilamu kabla ya jukumu lolote anaapa kwa imani yake? Jaribu kufikiria kwa mapana zaidi nafasi ya DINI kwenye nchi yoyote ile na pia usisahau vyombo vya kidini ni asasi za kiraia kama zilivyo NGO's .
Quote
 
 
-1 #4 2010-05-24 12:41
Mimi namheshimu Mhashama Kilaini lakini kwa hili naona akili yake inakua laini. Kwa upande moja anaeleza jinsi Kikwete alivyoshindwa kiuongozi na upande mwingine anamsifia. Kikwete is a very weak leader, who selects offcials based on friendship, family ties and other loyalties. Kwa hiyo waziri ambaye ni shemeji yake akitibua hamfukuzi. Tumekua tukisisitiza tunataka viongozi bora na siyo bora viongozi. Kwa hili Kikwete hafai. Kama kumchekea kila mtu kunamfanyia awe karibu na wananchi, huu sio ufumbuzi wa tatizo la TUCTA. Kila mtu anajua tatizo la Zanzibar limetatuliwa na Wazanzibar wenyewe jinsi walivyokua wameashiria wenyewe. Kilaini anampa credit Kikwete kwa vipi? Mhashama tumsifu Yesu Kristu na jaribu kushuhudia ukweli daima. Amina
Quote
 
 
+2 #3 2010-05-24 11:39
Askofu ametoa maoni yake tu kama raia mwingine yeyote. Anachosema ni kile anachoamini yeye. Kwa suala la zanzibar na uhuru wa habari nakubaliana nae. Lkn hayo mengine naomba kutofau[NENO BAYA] nae-with due respect. Kwa nini awaweke hao watendaji wabaya muda wote? Hiyo ni sehemu ya utendaji mbaya kwa anayewateua. Kila anachofanya waziri, kizuri au kibaya, kiko attributable to the appointing authority. Kwa nini Mh Magufuli aliposimamia barabara vizuri sifa alipewa pia mkapa?-kwa sababu ndie aliyemteua."Alter ago" ndo nadharia inayotumika hapa. Asante.
Quote
 
 
0 #2 2010-05-23 15:00
Kwakweli nakubaliana na askofu Method huwezi kupata rais kama kikwete kwasababu suala la Zanzibar nampongeza sana, na mpongeza Rais Karume na Ahmed, hili suala lilikuwa gumu sana, hata Mkapa pamoja na utendaji wake alibaki kwenye msimamo wa kwamba Cuf hawezi kuongonza , hata mwalimu nyerere suala hili haliliacha, lakini nani kama kikwete?kiulaini mgogoro wa Zanzibar huko wapi, wengi walilaumu kwamba walipo kutana Butiama yeye kama mwenyekiti wa CCM alitakiwa kulazimisha ili suala la Zanzibar lipite, lakini wamekuja na stail mpya kabisa wazee wa chama imebidi wakubali, make rais wa nchi, rais wa Zanzibar wamekubali [NENO BAYA]liza shida, watu bado hawataki, lakini tujiulize mgogoro wa zanzibar kwa faida ya nani?na hasara ya nani? Watanzania CHAGUA CCM, CHAGUA KIKWETE.
Quote
 
 
+1 #1 2010-05-23 04:46
Tumsifu Yesu Kristu, bwana askofu samahani kama nitakuwa nimekosea, mie nakushauri uachane na mambo ya siasa ili upate muda wa kutosha wa kumtumikia BWANA MUNGU. imeandikwa katika amri 10 za mungu usiseme uongo, katika nafsi yangu mimi nakuona umedanganya kwa kusema rais kikwete anaendelea kupendwa na wananchi. ni wengi nikiwamo mimi ambao wakati anachaguliwa tulifurahi sana, lakini sasa hivi tunamuomba Mungu atuepushie hili balaa mwezi wa10. unaposema neno linatakiwa liwe na uhakika, sababu wewe ni mtumishi wa mungu. vinginevyo utakuwa unaenda kinyume na agizo la Mungu 'usishuhudie uongo' AMINA.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner