MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Habari Madaktari washikilia msimamo na Pinda alainika
BOOKMARK THIS PAGE
Madaktari washikilia msimamo na Pinda alainika  Send to a friend
Sunday, 29 January 2012 10:42

Waandishi Wetu, Dar na mikoani
MATUMAINI ya kurejea kwa huduma za matibabu katika hospitali ya mbalimbali nchini yamezidi kutoweka, baada ya madaktari kuendelea kushikilia msimamo wao wa kutaka kukutana na Waziri Mkuu Mizengo Pinda ili kupata ufumbuzi wa matatizo yao.  

Siku moja baada ya kutokubalina na ujumbe wa Serikali ulioongozwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, madaktari hao jana kwa mara nyingine waliwarudisha patupu maofisa wawili waliofika eneo la kusanyiko lao, Hoteli ya Star Light Dar es Salaam kuwasilisha ujumbe wa maneno wa Waziri Mkuu Pinda kutaka kukutana nao leo na kuwataka kuwasilisha ujumbe huo kwa barua.


Hata hivyo madaktari hao walisema hawawezi kukutana leo na Waziri Mkuu kwa kuwa wamekubaliana kupumzika na kuendelea tena na vikao vyao kesho.Madaktari hao waliwasisitiza maofisa hao kuwapa barua rasmi kutoka kwa Waziri Mkuu Pinda, inayoeleza azma ya kukutana nao badala ya kuwasilisha ujumbe wa maneno matupu.


Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, aliwaambia wanahabari jana kuwa wameueleza ujumbe huo kwamba urudi na kuandaa ujumbe huo wa Waziri Mkuu Pinda kwa maandishi, ili baada ya wao kuusoma, wajibu kwa maandishi.Dk Ulimboka alisema utaratibu huo ukifanyika na wakakubaliana kukutana na Waziri Mkuu Pinda, lazima kwanza waingie mkataba kabla ya kufanya mkutano huo.  

"Tumewarudisha, tunataka waje na maandishi, nasi tutajibu kumjulisha tuliyonayo, ikiwa atatujibu na tutakubaliana, kabla ya kukutana naye (Pinda), lazima tuwekeane mkataba," alisema Dk Ulimboka na kuongeza:
"Sasa hatutaki mawasiliano ya simu au maneno, tunataka maandishi, mawasiliano yoyote sasa ni kwa barua tu."Alisisitiza.

Alipotakiwa kueleza ni mkataba gani wanaotaka kuwekeana kwanza na Waziri Mkuu, kiongozi huyo wa Jumuiya ya Madaktari, alisema lengo la kufanya hivyo ni kuzuia adhabu kwa viongozi wao na madaktari wote kwa ujumla.
"..Kabla ya kukutana na kuzungumza na Waziri Mkuu, tunataka tuwe na mkataba kuzuia adhabu kwa viongozi wetu wa mgomo na wote walio kwenye mgomo, isiwe baada ya mazungumzo, watu wanaadhibiwa wakati walikuwa wakidai haki zao," alisema.

Alidokeza kuwa wameanza taratibu za kuandaa maandamo na kufanya mikutano ya hadhara ili kuujulisha umma ukweli wa kinachoendelea na kufuta upotoshwaji unaoenezwa sasa.Dk Ulimboka alifafanua kuwa maandamao na mikutano hiyo, inalenga kuwafahamisha wananchi juu ya umuhimu wa kupata haki zao ambazo ni matibabu, maeneo mazuri ya kazi na vitendea kazi.


"Tunadhani ni wakati muafaka wa kufanya maandamano na mikutano ya hadhara, kuelezea wananchi matatizo yaliyomo katika sekta ya afya, 'system' (mfumo) imeoza, wizara ina matatizo mengi na juu kuna watu wanaoharibu,"alisema.Aliitaka Serikali iache vitisho katika mgogoro huo badala yake wafuate taratibu za kuumaliza ,akieleza kuwa hawawezi kuvumilia kufanya kazi katika mazingira magumu ambapo wagonjwa wanalala chini.

Wauguzi nao kugoma  
Wakati hayo yakiendelea,huduma za matibabu inatarajiwa kuzorota zaidi kuanzia kesho kufuatia madaktari wengine ambao walikuwa hawakugoma pamoja na wauguzi kujiunga katika mgomo huo.

Uchunguzi wa Mwananchi Jumapili katika maeneo mbalimbali nchini jana ulibaini hatua hiyo ambapo katika baadhi ya hospitali, huduma zinazotolewa ni za dharura pekee yake huku nazo pamoja na kliniki, zikiwa kwenye tishio la kusitishwa .

Kilimanjaro
Katika Hospitali ya Rufaa KCMC iliyopo Moshi mkoani Kilimanjaro, madaktari wamekuwa wakitoa matibabu kwa wagonjwa wa dharura huku wagonjwa wa nje na wale waliopewa rufaa kwenda katika hospitali hiyo, wakishindwa kupokelewa.
 
Ingawa Mkurugenzi Mtendaji wa KCMC,Dk Moshi Ntabaye hakupatikana jana kuelezea hali ilivyo, lakini baadhi ya madaktari walisema hali inatarajiwa kuwa mbaya zaidi kuanzia kesho.
 
“Kuanzia Jumatatu (kesho) ndio athari za mgomo zitaanza kuwa mbaya hapa kwetu (KCMC), kwa sababu tunatarajia kufunga kabisa kliniki zote maana hakuna madaktari,”alisema mmoja wa madaktari wa hospitali hiyo kitengo cha dharura.
 
Baadhi ya kliniki zitakazofungwa KCMC ni za wagonjwa wa kisukari, Ukimwi na watoto wachanga ambapo pia kuna kila dalili ya wauguzi kujiunga na mgomo huo wakati wowote kuanzia kesho kushinikiza kutekelezwa madai ya madaktari.
 
“Bila madaktari wauguzi hawawezi kufanya kazi , ndio maana umesikia wauguzi Muhimbili nao wanataraji kugoma, ikitokea hivyo ni lazima iambukize hospitali nyingine,”alisema daktari huyo aliyeomba asiandikwe gazetini kwa kuwa siyo msemaji wa madaktari.
 
Daktari mwingine ambaye naye aliomba jina lake lisitajwe gazetini, alisema kauli ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ya kutetea ongezeko la posho za wabunge imezidi kuchafua hali ya hewa.
 
“Moja ya mambo tunayodai ni posho za nyumba ambalo ni dai la msingi kabisa lakini, Waziri Mkuu haguswi nalo ila posho za wabunge tena Sh200,000 kwa siku anatetea, huu ni usaliti,”alilalamika.

Mkaoni Arusha
Mkoani Arusha, taarifa zinaeleza kuwa madaktari katika hospitali ya Mount Meru walitarajiwa kujiunga rasmi na mgomo huo kesho.Baadhi ya madaktari wa hospitali hiyo waliohojiwa na mwandishi wa habari hizi, walisema kuwa kwa sasa wanaendelea na mgomo baridi, lakini, Jumatatu  watautangazia umma rasmi kuanza kwa mgomo.

"Tulikuwa tunamsubiri Mganga Mkuu arejee ofisini ili tuweze kufanya vikao naye na kumweleza msimamo wetu wa kugoma kudai haki yetu ya msingi,"alidai daktari mmoja.


Wagonjwa waionya Serikali
Kutoka mkoani Dodoma habari zinasema kuwa wagonjwa katika hospitali ya mkoa huo, wameitaka Serikali kuacha kucheza na maisha ya watu badala yake wakae meza moja na madaktari na kujadili matatizo yao.
Wagonjwa hao wamechukua hatua hiyo wakati vifo vya wagonjwa katika hospitali hiyo vikiongezeka siku hadi siku, hali iliyofanya baadhi ya ndugu wa wagonjwa kuwatorosha.

Stephano Mtoro Baba mzazi wa mtoto Pamela Mtoro,aliyelazwa hospitalini hapo alisema kuwa alifika hapo na mwanawe akisumbuliwa na maradhi ya kujaa tumbo wiki iliyopita, na tangu muda huo, hajapata matibabu yoyote na kwamba hali inazidi kuwa mbaya.

“Hali ni mbaya hapa, tangu nimekuja nimeshuhudia zaidi ya watoto watano wakifariki kwa kukosa matibabu. Mwanangu yuko katika hali mbaya hatujapata huduma tuna wiki nzima sasa, naomba Serikali iwasikilize madai yao, ”alisema Mtoro.

Mgonjwa mwingine Kizia Mkongwa  alisema yeye alifanyiwa upasuaji baada ya mtoto kufia tumboni lakini, kutokana na mgomo huo, hadi sasa bado hajapewa matibabu yoyote.

“Serikali isilete mzaha kwa kweli wawasikilize hawa madaktari maana kila siku tunashuhudia maiti zinatoka wodini halafu wanatuletea wanafunzi wanaojifunza uuguzi na udaktari sasa ndugu zetu si watakufa wote jamani!”alilalamika  Nyange.

Uchunguzi wa Mwananchi umebaini kuwa sasa baadhi ya wagonjwa wamekuwa wakitoroka na ndugu zao kuhofia kupoteza maisha huku baadhi ya madaktari wakiwashauri wagonjwa hao kwenda kwenye hospitali za binafsi, kwa kuwa mgomo huo hautoisha mpaka kieleweke.

Askofu Kilaini
Askofu Msaidizi wa Jimbo la Bukoba, Methodius Kilani alisema inasikitisha kuona wagonjwa wakiteseka hospitalini kutokana na mgomo huo."Kwa namna yoyote ile, wagonjwa wanapaswa kuhudumiwa kwa sababu suala la matibabu linahusisha ni uhai," alisisitiza na kuongeza:

"Inaleta shida kidogo kujua kwa nini Serikali haitatui madai ya madaktari ambayo ni ya msingi, au haina fedha?  Kama Serikali haina fedha iseme ili wahusika na Watanzania wote wajue.’’

Kauli ya LHRC
Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimemtaka  Pinda, kwenda kuonana na madaktari hao badala ya kusubiri wamfuate ofisini.

Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Hellen Kijo-Bisimba alisema haiwezekani Waziri Mkuu aendelee kukaa ofisini wakati anajua kuwa madaktari wanagoma na wagonjwa wanataabika.

“Hakuna haja ya Pinda kusema madaktari wakiwa tayari waende kuonana naye kwa sababu huu ni ubabaishaji. Wao (madaktari) wako tayari na ndio maana wakagoma hadi pale madai yao yatakaposikilizwa sasa yeye (Pinda) akiendelea kuwasubiri ofisini maana yake nini kama sio kuleta vifo?"                                                          Imeandaliwa na Geofrey Nyangoro, Dar, Daniel Mjema, Moshi, Daniel Mwingira, Masoud Masasi na Hamisi Mwesi, Dodoma


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
Last Updated on Sunday, 29 January 2012 12:19
 

Comments 

 
0 #8 2012-02-04 11:03
kwanini abariki ongezeko la posho za wabunge? hii ndio maana madactari wameamua kugoma kwa sababu viongozi hawawaangalii kwa jicho la tatu hawajui umuhimu wao, ila dr ni muhimu sana kupita hata huyo mbunge

Wameamua kupandisha posho kwa sababu mwaka 2015 nusu ya wabunge wa ccm hawatarudi tena bungeni kutokana na kutokubalika majimboni mwao hivyo wanaona wajinufaishe na kujitajirisha kipindi hiki kwa kupandisha posho
Quote
 
 
0 #7 2012-02-03 12:39
hatuna raisi wala waziri mkuu...full ubabaishaji. 2015 ndo maziko yao hawa mafisadi.
Quote
 
 
0 #6 2012-01-30 09:35
sio mchezo mambo ni magumu
Quote
 
 
0 #5 2012-01-29 23:42
Ninachokiona ni zile siku 100 alizopewa kikwete sasa zimeisha kwa hiyo ndo sekeseke limeanza kaa macho tukomboe nchi
Quote
 
 
0 #4 2012-01-29 18:35
Nimelisikia tamko la waziri mkuu leo,akiwaamuru madaktari kurudi kazini kuanzia siku ya jumatatu,kutoku fanya hivyo wataondolewa katika utumishi wa umma.Matamshi kama haya hatukuyao katika ongezeko la posho za wabunge.Kwa maoni yangu ,hivyo ni vitisho, na sioni kama ndio utatuzi wa tatizo lilopo,kwa sababu hii ni TAALUMA yenye kuhitaji akili iliyo timamu,uchaji wa moyo,na uumbaji bila siasa wala uchakachuaji,sa sa sijui kama serikali itawawekea viranja vya kuwasimamia katika kutoa matibabu yenye kukidhi haja,naogopa kama wataburuzwa .kazi nzuri hufanywa kwa moyo mweupe usio na kinyongo.Madaktari mioyo yao sio myeupe, hata kama watarudi kazini.
Kama ilivyodorola elimu nahofia kudorola kwa huduma za Tiba , madhara yake yapo wazi kabisa . Naishauri serikali itumie busara zaidi kuliko ubabe.Wakumbuke wao wanatibiwa nje ya nchi, si katika hospitali zetu za walala hoi.
Quote
 
 
0 #3 2012-01-29 16:11
nadhani madaktari si sekta muhimu kwa jamii ya tanzania; kwa sababu zifuatazo:
jamii inaamini kufa ni mipango ya mungu ambapo kwa nchi nyengine ni uzembe.
vilevile mbunge ambaye amemaliza darasa la saba na kuchaguliwa ama kuteuliwa anapokea hela nyingi kuliko daktari aliyesoma miaka 5 au 7 kama alikuwa urusi.hii inatokana na umuhimu wa elimu katika jamii na kwa vile elimu na taaluma sio muhimu basi hali itaendelea kuwa hivyo mpaka elimu itakapo pata thamani katika jamii ya tanzania.
Mtu anakuwa msemaji wa wizara kama vile afya ya yeye hiyo si fani yake basi kinachotokea ni mkodombwe.
Rais tafadhali chagua watu kutokana na sifa zao za kielimu na sio maji ya bendera.
tujaribu kutofautisha kati ya elimu na siasa kwa ajili ya faida ya umma ambao unateseka bila hatia na mwishoe kifo ambacho kingeweza kuepukika.
kila la kheri tanzania.
Quote
 
 
0 #2 2012-01-29 16:01
pinda hacha ubabaishaji, kutana na Madaktari kusolve tatizo.
Quote
 
 
0 #1 2012-01-29 13:57
Mgomo wa madaktari ni moja ya viashiria vya kutokuwepo amani kwani wagonjwa tutataabika sana.

Nawasihi madaktari wakae chini na kutuliza hasiri,najua wana madai tena makubwa.Hivo Waziri Mkuu akae nao kwani ni watoto wake,washaurian e na kufikia mwafaka.

Mzee (Pinda)nenda kawasikilize vijana wako sisi wajomba zako tunawahitaji watuhudumie.
Tunaumia na magonjwa madaktari wetu wamegoma na wewe baba unangoja wakufuate ofisini.Nenda kaa nao,wasikkilize mshauriane nama ya kuendelea kuto huduma kwa hawa vijana wako (watanzania).

Naomba tusuanze huu mwaka kwa kupoteza wagonjwa wasio ha hatia hko mawodini.

ASANTENI SANA MADAKTARI kwa kusiliza kilio cha watanzania.NAAMINI ninyi ninyi ni wasomi na mnajua hatari inayoweza kutokea iwapo mgomo wenu utaenelea.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner