MwanzoContactsEmail
Home Jumapili Habari Mgomo wa madaktari bado uko pale pale
BOOKMARK THIS PAGE
Mgomo wa madaktari bado uko pale pale  Send to a friend
Sunday, 05 February 2012 10:15

Geofrey Nyang’oro 

LICHA ya wabunge kuwataka madaktari kusitisha mgomo wao wakati Serikali ikishughulikia madai yao,wataalamu hao wamesisitiza kuendelea na msimamo wao hadi watakapokutana na Kamati ya kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii ili kupatia ufumbuzi tatizo hilo.  

Akizungumza na Mwananchi Jumapili jana Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Stephen Ulimboka, alisema huduma zitakazokuwa zikitolewa ni zile za dharura peke yake.  Alisema kuwa jana walikuwa na kikao kujadili tamko la juzi bungeni la Waziri wa Afya, Dk Haji Mponda ambalo alisema lilijaa siasa.  

Alisema kuwa waziri huyo hakutoa majibu ya madai yao na kufafanua kuwa kauli yake kwamba huduma zinaendelea si ya kweli na inaupotosha umma wa Watanzania.  “Waziri alijikita zaidi katika hoja za Serikali, lakini hakusema Serikali imetoa kiwango gani kwa madaktari ili kunusuru mgomo,” alisema Ulimboka.

Akiwasilisha kauli ya Serikali bungeni, huku akieleza mlolongo wa historia ya mgomo huo, Dk Mponda  alisema Januari 30, mwaka huu, Serikali iliunda Kamati ya kushughulikia maazimio yaliyowasilishwa na madaktari kwa Waziri Mkuu, Mizengo Pinda.

Alisema kamati hiyo itayachambua na kutoa maoni na mapendekezo yatakayosaidia Serikali kumaliza mgogoro huo wa watumishi wa sekta ya afya na kwamba, tayari imeanza kazi.

 Juzi Jumuiya hiyo inayoshughulikia madai ya madaktari nchini ilisema iko tayari kukutana na Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii kujadili hatima ya mgomo wa madaktari unaendelea hivi sasa.  Jumuiya hiyo pia ilieleza dhamira yake ya kuitisha mkutano wa madaktari wote kujadili tamko la Serikali na kufikia uamuzi wa nini kinastahili kujadiliwa pindi watakapokutana na kamati hiyo.  

“Kamati inalishukuru Bunge kwa kuagiza Kamati ya Kudumu ya Huduma za Jamii kuanza kazi mara moja ya kukutana na sisi. Kamati pamoja na jumuiya ya madaktari ipo tayari kukutana na Kamati ya Bunge  na hiyo ni hatua mwafaka ya kufikia maridhiano ya kweli katika kumaliza tatizo hili”alisema Ulimboka.  

Hata hivyo, Dk Ulimboka alisisitiza uamuzi wao wa kukutana na kufanya mkutano wa madaktari kwa kile alichodai ni madaktari waliohudhuria mkutano ndio walioitisha mgomo.  Katika tamko lao la jana pia walikanusha madai yaliyotolewa na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii bungeni kuwa huduma za afya katika Hosptali ya Taifa ya Muhimbili,Taaisisi ya Mifupa (MOI) na hospitali zingine za rufaa nchini zinatolewa kama kawaida.  

“Si kweli kuwa huduma za afya zinatolewa kama kawaida katika hosptali tajwa. Mfano Hosptali ya Rufaa ya KCMC Moshi taarifa za jana zinaonyesha kuwa hali ilikuwa mbaya kiasi cha kusitishwa kwa huduma zote isipokuwa ya ngozi,” alisema.  Alhamisi wiki iliyopita Kamati ya Wabunge wa CCM ilimtaka Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Haji Mponda, Naibu wake, Dk Lucy Nkya na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni, kujiuzulu kwa kile kilichoelezwa kuwa wao ni chanzo cha mgomo wa madaktari unaendelea nchini.

Kauli ya Naibu Spika Akitoa mwongozo wake wiki hii bungeni, Naibu Spika, Job Ndugai, alisema suala la mgomo wa madaktari ni zito na kwamba, tatizo lililojitokeza ni kusikiliza upande mmoja wa Serikali kwa sababu, madaktari hawawezi kwenda kusimama bungeni kueleza madai yao.

“Waziri ametueleza kuwa wameunda kamati ya kupitia madai ya madaktari,  nakumbuka mojawapo ya madai yao ambayo Serikali haikutaja hapa na hiyo nina uhakika hiyo kamati haitasema ni kwamba, Wizara ya Afya kuna baadhi ya watendaji wenye uwezo wa kiutendaji wana kauli mbaya na dharau,” alisema Ndugai na kuongeza;

“Hiyo haimo. Uamuzi wa kuhusu jambo hili nalipeleka Kamati ya Huduma za Jamii, ili ifanyie kazi haraka kwa kuita pande zote zinazohusika ziweze kueleza madai yao na tutapata mwafaka haraka.”
Naye Ibrahim Yamola anaripoti kuwa wakati mgomo wa madaktari ukiendelea, hospitali  binafsi zinakabiliwa na msongamano mkubwa wa wagonjwa.

Wakizungumza na Mwananchi Jumapili  Jijini Dar es Salaam jana kwa nyakati tofauti  Mkurugenzi  Mtendaji wa Hospitali ya TMJ,  Parul Chhaya, alisema ongezeko la wagonjwa limekuwa kubwa hospitalini hapo wakati huu wa mgomo.
“Tangu kuanza kwa mgomo wa madakatri,wagonjwa wengi wamekuwa wakimiminika kuja kupata huduma na hasa wale mahututi wakitokea hospitali ya Taifa Muhimbili,”alisema Chhaya.

Akifafanua, alisema wameanzisha mfumo wa kuwahudumia wagonjwa bila kujali gharama ambazo zinazohitajika ili kuweza kunusuru maisha ya wangonjwa wasio na uwezo.

“Tunapokea wagonjwa wa aina mbalimbali na kuwatibu bila gharama hadi wanapopata nafuu ndipo tutanaangalia kama ana uwezo wa kulipa ama la, kama hana uwezo tutamwacha aondoke,”alisema Chhaya.
    


Add this page to your favorite Social Bookmarking websites
Reddit! Del.icio.us! Mixx! Free and Open Source Software News Google! Live! Facebook! StumbleUpon! TwitThis Joomla Free PHP
 

Comments 

 
0 #1 2012-02-05 12:20
kaza mwendo vijana, mapaka kieleweke, Serikali hawatatui matatizo ya wananchi mpaka migoma ndugu yangu.

Angalia walimu, waligoma ndio wakalipwa amalimbikizo yao.
Quote
 

Add comment

Tumia jukwaa ili kutoa maoni ambayo yatasaidia kulijenga taifa letu. Kumbuka, maoni yako yatapitiwa kwanza kabla hayajarushwa hewani!!!!!!


Banner
Banner
Banner