
| Askofu Kilaini: Tanzania inahitaji Rais kama Kagame | Send to a friend |
| Sunday, 05 February 2012 10:19 |
|
ASKOFU Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Kagera, Dk Methodius Kilaini, amesema ili Tanzania iweze kusonga mbele, sasa inahitaji kiongozi atakayeongoza kwa 'mkono wa chuma' na kumtaja Rais Paul Kagame kuwa ni mfano wa viongozi wanaoweza kuirejesha katika mwelekeo sahihi. Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi Jumapili jana mjini Bukoba, Askofu Kilaini alisema kwa hali ilivyo sasa, taifa linapaswa kumkumbuka aliyekuwa Waziri Mkuu hayati Edward Sokoine, kwani ni kiongozi aliyefumba macho na kuwawajibisha watu waliokosea bila kuwaonea huruma. Askofu huyo, alisema tatizo kubwa linaloikabili Tanzania wakati huu, ni kumpata kiongozi ajaye atakayekuwa tayari kufa kwa ajili ya kuwashughulikia mafisadi bila kuwaonea huruma, huku akisisitiza kuwa Rais Kagame wa Rwanda ni mfano wa viongozi wanaohitajika sasa kuiongoza Tanzania. Alieleza kuwa huu ni wakati wa kuomba kwa bidii kwani ni tatizo kubwa kumpata kiongozi ajaye. Alisema yeye amekuwa akimwomba sana Mungu ili taifa liweze kumpata kiongozi atakuwa tayari kufa lakini haki za Watanzania zipatikane. “Tunahitaji mtu ambaye atajinusuru kwa kusema, nife lakini haki za watu zipatikane, na ndiyo sababu sasa hivi baadhi yetu tunamkumbuka Sokoine (Edward Moringe), labda ndiyo sababu alikufa, alifumba macho hakuona mtu, hili ndilo tunalohitaji sasa, tena wale wenye mali watatuzungusha kwa mali zetu; mali ambazo wameziiba kwetu; wanazitumia kuturubuni nazo. Hakika viongozi wetu wapo tayari kutuuza, uende mkoani uende wilayani wanapewa kile kidogo basi anaachia, hii ndiyo shida tuliyonayo.” Aliongeza kusema; “Kiongozi anayepaswa kuja sasa, hategemei chama ni hulka yake mwenyewe na tunaweza kumuita mkombozi; mkombozi hana sura, chama, rangi wala kabila, akitoka ni kama nabii anashuka kabisa anawasaidia. Hivyo siwezi kusema anatoka CCM, Chadema, CUF ama wapi, watu wote ni Watanzania. Tunahitaji Mtanzania mmoja atakaye inuka na kutunusuru”. Aliongeza kusema kuwa Tanzania anahitajika kiongozi mwenye hulka ya kuchukia mabaya huku akibainisha kuwa viongozi wengi wa sasa wamekuwa wakiahidi mazuri lakini wakipata madaraka hugeuka na kulainika. ‘’Kiongozi anayetakiwa ni yule ambaye hatakuwa na uroho wa kula kwani tukimpata kiongozi kama huyo hawezi kuwadhibiti wanaokula na kutoa mfano wa hayati Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwamba hata nyumba alijengewa baada ya kustaafu. Tulipokosea Askofu Kilaini alisema, tatizo la nchi yetu limekuwa na mizizi ya zamani, halijaanza leo, isipokuwa sasa ugonjwa unakua na usipotibiwa utazidi kukua. Alikemea tabia ya watu wengi kutaka kufanyiwa kila kitu na Serikali pamoja na wafadhili na kutaka kila mwananchi kuchapa kazi. ‘’Ukiwa nje ya nchi utakuta Mtanzania anachapa kazi kweli tofauti na hapa nchini, na kwamba anaporudi nyumbani ni kama amepigwa pasi na hapa ndipo tatizo lilipo, ama katika uongozi wetu kubebana pale mmoja anapoboronga .’’ alisema Askofu Kilaini na kuongeza; “Mtu akifanya kazi ni lazima awekewe viwango, kwamba unafanya kazi ni lazima kufikia hapa asipofika ni lazima aachie ngazi. Hili lilipaswa kufanyika katika ngazi zote kutoka juu hadi chini, sisi hapo hatujafika wenzetu mtu asipofikia kiwango ni lazima wawajibike kwa kuachia ngazi, Alisema tatizo lingine lililopo ni kwamba, inaonekana nchi wafadhili zimetudekeza na kwamba jambo hilo halina nia njema bali linawanufaisha zaidi wao. “Wahisani wamekuwa hivyo kwani wamekuwa wakija na kutupatia kitu kidogo huku wao wakizoa utajiri wetu na kutoweka nao.’’ Wanasiasa kupita makanisani Akizungumzia tabia ya baadhi ya wanasiasa kutumia nyumba za ibada kukidhi malengo yao, alisema kwa mtazamo wake jambo hilo ni hatari kwani linaweza kuliingiza taifa katika vurugu za kidini. Hata hivyo alisema kwa upande mwingine jambo hilo halina tatizo kwa watu au wanasiasa wanaoamua kwenda kwenye nyumba za ibada na kutoa madukuduku au mambo yanayowakwanza, mbele za Mungu. “Kidogo mimi naogopa, kizuri ni kuona makanisa yanakuwa kimbilio la watu. Mtu aliyekwazika na hajui aongelee wapi anapokwenda kanisani, hili ni jambo zuri, unatoa jeraha linalokuumiza na huna mahali popote unapoweza kulitoa isipokuwa kanisani. ‘’ Ila si vyema makanisa kugeuzwa mahali pa mikakati ya kutimiza malengo ya kisiasa. Kama tutakubali makanisa kuwa mahali pa kutumika kisiasa, kwanza viongozi wenyewe wa dini wataanza kulumbana na kupigana.” alionya. kuwa mahali pa kusemea mambo ambayo wanaogopa kwenda kusemea Bungeni, na kwa waandishi wa habari wanajifunga katika koti la Kanisa na kwenda kukiripua pale kwa vile hakuna maswali na kutoka na kuchangia vyema wamebaki kuimbiwa ‘asifiwe asifiwe’ na ‘alhandulilah’ hivyo kuonya unabii wa siasa ufanyiwe kwenye majukwaa ya siasa. Kauli Kikwete ni changuo la Mungu Akizungumzia kauli yake aliyowahi kuitoa mwaka 2005 kwamba mgombea urais kupitia CCM Rais Jakaya Kikwete alikuwa ni chaguo la Mungu , Askofu Kilani alifafanua kwamba alichosema ni kwamba, ‘Sauti ya watu ni sauti ya Mungu,’ kwani mgombea huyo alikuwa amechanguliwa na watu kwa asilimia 80, alichomaanisha ni kwamba mgombea huyo amekubalika na watu. “Mimi nilichosema ni kwamba sauti ya watu ni changuo la Mungu na alikuwa( Kikwete) amechaguliwa na watu wengi, ndani ya CCM wakati ule nikasema huyu ni changuo la Mungu kwa sababu amechaguliwa na watu, halafu baadaye akachaguliwa na asilimia 80 ya Watanzania. Watu sio wapumbavu hawachagui kwa niaba ya shetani… Lakini hata Yuda (aliyemsaliti Yesu) alichaguliwa na Yesu alikuwa chaguo la Mungu?” alieleza Mtheolojia huyo. Alisema ingawa hamtetei moja kwa moja Rais Kikwete, anaamini baadhi ya watendaji wake wanamwangusha na kumtaka kiongozi huyo kuwa imara katika masuala mbalimbali, huku akitolea mfano wa nyongeza za posho za wabunge na kumtaka kutoa kauli ya moja kwa moja kwamba jambo hilo haliwezekani. |

Habari Mpya
Picha
Zenye Mvuto
- Nafasi za Kazi
- Links za wateja na washirika wetu
- Muswada wa madini waitoa jasho serikali
- Bi kizee asafari kilometa 50 kupinga hotuba ya JK, AMUONYA ASITUMIE MADARAKA YAKE VIBAYA
- Mishahara sekta binafsi Tucta yashtukia danganya toto
- Vigogo UVCCM wajiuzulu
- Mwinyi atetea ajira za wafanyakazi, ashauri utu uheshimiwe kudumisha Amani















Comments
Wengi wanajineemesha huku waumini wao wakiteseka iko siku mungu atawahukumu kwa unafiki wenu.
Kagame anaisadidia sana nchi yake kimaendeleo, lakini tatizo ni kwamba style yake ya uongozi ni ya kiubabe sana. ana tuhuma nyingi sana za kuwaua watu wanaompinga kwa kutumia maafisa wake wa usalama. Na pia historia yake hadi kuwa raisi imejaa ukatili na umwagaji damu, kutia dani tuhuma kwamba yeye ndie alietoa amri ndege ya Habyarimana iangushe. Pia anatuhumiwa kuwa na kampeni ya chini nchini ya kupunguza idadi ya Wahutu ili iendane na idadi ya watusi na kwamba katika hili Wahutu wengi wameuwawa. Waandishi wa habari Rwanda hawana uhuru katika kazi zao, na wala wananchi wa kawaida kuikosoa serikali. Sasa japo Rwanda ina maendeleo, style ya uongozi wa namna hiyo haitufai Tanzania.
BILAMKONO WA CHUMA NCHI HII HAIENDI POPOTE KIMAENDELEO
uone makabwela walikua wanafanya kazi nchi za njee wameleta vitu kwa ajili ya familia
yake wanavomyanyasa wanakwambia sheria jee
wale wanaondoka na matani ya dhahabu kwenya migodi nendeni kule kwenye migodi museme sheria.
Ili maendeleo yawepo na uchumi wa nchi kukua, tunahitaji mtu kama kagame, na ikiwezekana damu imwagike.
Daudi alimpiha goriath, ndio heshima ikaja, kwa hiyo hata maandiko yanatambua kuwa, ili amani iwepo, usawa na kuondoa umasikini lazima ncha ya upanga itumike.